Taharuki sadaka ya kuchinja 

*Mamia ya kondoo yachinjwa, wanafunzi shule za msingi walishwa nyama, wapigwa picha

*Wazazi washituka, wazuia watoto wasiende shuleni wakidai ni aina ya kafara isiyokubalika

*Mkuu wa Wilaya aingilia kati, aitisha kikao cha dharura

Arusha

Na Mwandishi Wetu

Taharuki imewakumba wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule za msingi kadhaa jijini Arusha baada ya kuibuka kwa kikundi kinachodaiwa kutoa sadaka ya nyama shuleni; JAMHURI linataarifu.

Wiki ilyopita kikundi hicho kilikwenda katika Shule ya Msingi Suye na Shule ya Msingi Daraja Mbili, kisha wakachinja kondoo na mbuzi mbele ya wanafunzi.

Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Darajambili (jina linahifadhiwa) ameliambia JAMHURI kuwa asubuhi ya siku hiyo walikuta mifugo shuleni kwao na kupigwa butwaa.

“Baadaye wakaja watu, wakatuita, tukaandikisha majina na kusimama wengine nyuma ya kondoo na wengine mbuzi. Wakasoma dua na kutupiga picha wakituambia kuwa wanatupa sadaka.

“Wakawachinja wale wanyama mbele yetu, wakapika nyama na wali kisha tukapewa ili tule,” anasema mtoto huyo.

Alipoulizwa iwapo alikuwa na hofu yoyote na kama mgawo wa sadaka uliwatenga watoto kutokana na imani yao, amesema hakuna aliyekuwa na hofu wala hakuna aliyetengwa kwa imani yake.

“Wote tulikula wali na nyama huku tukipigwa picha. Baadaye tukaendelea na masomo,” anasema kijana huyo.

Sadaka ya kuchinja imetolewa katika kata za Kimandolu na Baraa zilizopo Arusha Mjini huku wananchi wakipokea matukio hayo kwa hisia tofauti; wengi wakidai kuwa ni utoaji wa kafara.

Mtazamo huo ulisababisha baadhi ya wazazi kuwazuia watoto wao kwenda shuleni ili kuwaepusha kushiriki sadaka wasiyoifahamu.

Mmoja wa wazazi amezungumza na JAMHURI akiomba kutotajwa gazetini na kusema: “Hii inashangaza sana. Kwa nini waende shuleni? Nani amewaruhusu? Ni sadaka kwa ajili ya nini?

“Kwa nini mifugo ichinjwe hadharani mbele ya watoto? Kwa nini wanaandika majina ya watoto wetu kwenye karatasi zenye idadi ya mifugo waliyoichinja?

“Maswali ni mengi sana na ina kera mno. Kwa nini wanawashikisha karatasi zenye majina na kuwapiga picha? Hizo picha wanazipeleka wapi? Kama kweli ni sadaka, kwa nini wakati wa kula wanawapiga picha? Sadaka na picha za watoto wetu vina uhusiano gani?”

Wazazi wa madhehebu na dini mbalimbali waliopo ndani ya kata za Kimandolu na Baraa wanalalamika wakisema kitendo hicho kinawaingiza watoto kwenye maagano ya imani tofauti na ya wazazi wao.

“Kama ni msaada waseme tutawaelewa, lakini kutuambia kuwa ni sadaka! Haiingii akilini,” anasema mzazi mwingine.

Tayari watoto wa shule za Darajambili, Suye na Murieti wamekwisha kulishwa sadaka ya nyama na kupigwa picha kabla watoa sadaka hawajakwama kutekeleza utoaji wao katika shule za Moshono na Baraa.

Wakazi na wazazi wa watoto wanaosoma shule za msingi Moshono na Baraa wamekikatalia kikundi hicho kwa hoja kuwa hakina kibali chochote cha kulisha wanafunzi huku taarifa zake zikikosekana katika mamlaka za serikali.

JAMHURI linafahamu kwamba Jumatano ya wiki iliyopita kondoo 135, mbuzi 10 na ng’ombe mmoja walipelekwa Shule ya Msingi Baraa na kufungiwa madarasani wakisubiri kuchinjwa siku inayofuata.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo hakuelewa ni nini kinaendelea, hivyo akapiga simu ngazi za juu kuomba mwongozo.

JAMHURI limeelezwa kwamba mwalimu huyo alimpigia simu Diwani wa Kimandolu, Abraham Mollel, kumueleza kuwapo kwa mifugo ndani ya vyumba vya madarasa.

Kesho yake Mollel na Ofisa Elimu wa Kata walifika shuleni na kushuhudia madarasa yakigeuzwa kuwa mazizi ya mifugo kabla ya kuchinjwa.

“Nikawahoji watu waliopeleka ile mifugo, wakaniambia wanafanya shughuli kihalali kwa kushirikiana na taasisi moja ya Misiri.

“Kwamba wanachofanya ni kutoa sadaka kwa shule zilizopo mkoani Arusha,” anasema Mollel ambaye hata hivyo akawataka kusitisha suala hilo kwa muda hadi watakapopata vibali stahiki kutoka kwa Ofisa Elimu wa Wilaya au Kata.

Mollel anasema watu hao waliondoka shuleni na mifugo yao, wakaenda Shule ya Msingi Mshono ambako walikumbana na upinzani kutoka kwa wananchi.

Inadaiwa kuwa kikundi hicho hupokea fedha kutoka kwa wananchi wa Misri na ni hao ndio hutoa maelekezo namna ya kugawa sadaka kwa wahusika.

“Nadhani ili kuwahakikishia kuwa fedha zao zimetumika kadiri ya maekelezo, ndiyo maana wanawapiga picha watoto wakati wakila,” anasema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Baraa, Ozwin Mosha, amesema taharuki iliyojitokeza ni kwa sababu ya kikundi hicho kutofuata utaratibu.

“Suala hili limefika kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha. Kwa ufupi ni kwamba hapakuwa na ushirikishwaji kwenye jambo hili,” anasema Mwalimu Mosha.

Amedokeza kuwa baada ya kikundi hicho kukumbana na pingamizi kutoka kwa wananchi kimelazimika kuzihusisha mamlaka za serikali na jana walitarajiwa kuzindua programu hiyo.

“Tunatarajia kuwa mkuu wa wilaya na mkurugenzi watalifafanua vema suala hili na wananchi watalielewa,” anasema Mwalimu Mosha.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda amezungumza na JAMHURI na kusema taarifa hizo alizipata baada ya kupigiwa simu na Ofisa Tarafa.

“Ni kweli taarifa hizi zilizua taharuki kwa wananchi na kwa viongozi, suala hili lilikuwa halifahamiki kwa  viongozi wa juu wa wilaya.

“Aliyetoa kibali ni Kaimu Ofisa Elimu wa Wilaya. Nadhani ugeni wake ofisini ulisababisha kutoelewa namna nzuri ya kutoa miongozo ya kutekeleza suala hili,” anasema DC Mtanda.

Anasema kutokana na taharuki iliyojitokeza amewazuia kuendelea kutoa sadaka ya chakula na kuwaita ofisini kwake kujieleza na kuhakiki taarifa zao akishirikiana na viongozi wengine wa wilaya.

“Tukabaini kuwa kikundi hiki kimetoka kwenye taasisi halali nchini. Kwa hiyo Jumatatu (jana) nitakwenda kuzungumza na wazazi, viongozi wa kidini na wadau wengine kisha tutazindua rasmi shughuli zao kwa kufuata taratibu stahiki,” anasema.

Tayari Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha imefikia makubaliano na kikundi hicho kutoa msaada wa chakula kwa shule kadhaa kama sadaka kwa kipindi cha miaka miwili.

“Hatutaki tena masuala ya kuwapiga picha wanafunzi kisa wanataka kuwaridhisha watoa fedha.

“Mifugo yote watakayoleta kwa ajili ya sadaka itapelekwa kiwandani kuchinjwa. Tuna kiwanda chetu cha usindikaji nyama hapa, shuleni watapiga picha na wanafunzi wakati wa kula na si vinginevyo,” anasema Mtanda na kuongeza kuwa sheria hairuhusu kuchinja wanyama shuleni.