Na Isri Mohamed

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeifungia klabu Yanga Sc ya Tanzania kusajili mpaka itakapomlipa aliyekuwa mchezaji wake Lazarus Kambole baada ya mchezaji huyo kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo.

Taarifa ya shirikisho la soka Tanzania (TFF) imebainisha kuwa Kambole raia wa Zambia alifungua kesi FIFA akidai malipo ya malimbikizo ya mishahara na fidia ya kuvunjiwa mkataba.

Young Africans ilitakiwa iwe imemlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini haikutekeleza hukumu hiyo.

“Wakati FIFA imeifungia klabu hiyo kufanya uhamisho wa wachezaji kimataifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) nalo limeifungia kufanya uhamisho wa ndani.” imesema taarifa ya TFF.

“TFF inazikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.” TFF.