Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Kibaha

Manispaa ya Kibaha imefanikiwa kufikia asilimia 80 ya utoaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni, huku wazazi na wananchi wakihimizwa kushiriki kikamilifu katika kuchangia chakula ili kufikia asilimia 100.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Catherine Saguti, amesema utoaji wa chakula kwa wanafunzi ni jukumu la pamoja kati ya Halmashauri, wazazi na jamii, hivyo ushirikiano wa wadau wote ni muhimu kuhakikisha kila mwanafunzi anapata chakula cha kutosha akiwa shuleni.

Alieleza hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Lishe cha robo ya kwanza ya mwaka kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jengo la Utawala, Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo.

Amesisitiza kuwa lishe bora ni msingi muhimu katika ukuaji wa watoto, afya zao na maendeleo ya kitaaluma, huku akiwataka wazazi kutambua umuhimu wa kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao wanapokuwa shuleni.

Kikao hicho kimejadili mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa afua za lishe, changamoto zilizojitokeza pamoja na mikakati ya kuboresha huduma za lishe kwa wananchi, hususan wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Imeelezwa kuwa utoaji wa chakula shuleni unachangia kuboresha mahudhurio ya wanafunzi, afya zao na mazingira ya kujifunzia, huku lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wote wanapata chakula wakiwa shuleni.

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha inaendelea kuhimiza ushiriki wa wazazi na jamii katika kuhakikisha huduma za lishe shuleni zinaimarika na kufikia kiwango cha asilimia 100.