Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wanawake katika sekta ya kilimo; fursa, changamoto na suluhisho. Kimsingi, wanawake si wazalishaji wa chakula peke yake bali ni wadau muhimu katika uchumi wa kilimo lakini bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazowazuia kunufaika.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), asilimia 45 ya nguvu kazi ya kilimo katika nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania ni wanawake ila wanakosa haki sawa kama ilivyo wanaume.

Kutokana na hali hiyo huku tukielekea kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Wabunge Wanawake wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu unaotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 2 hadi 5, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Bajeti Kuu ya Mwaka wa Fedha wa 2026/2027, imeziagiza mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga asilimia 15 ya mapato ya ndani badala ya asilimia 10 ya awali kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kupitia mikopo hiyo, wanawake sasa wataanza kutumia fursa za kilimo kujipatia maendeleo.

Fursa zilizopo katika kilimo kwa ajili ya wanawake ni nyingi zikiwamo uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, kilimo cha kisasa na matumizi ya teknolojia, usindikaji na kuongeza thamani ya mazao, biashara ya pembejeo na zana za kilimo, masoko ya ndani na nje ya nchi, vikundi vya ushirika na upatikanaji wa mitaji na ajira.

Changamoto zinazowakabili wanawake katika kilimo ni ukosefu wa umiliki wa ardhi, mitaji, masoko, mila na mfumo dume.

Wataja suluhisho

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, anasema uwezeshaji wa wanawake katika kilimo ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji wa chakula, lishe, afya ya mifugo, usalama wa chakula na utunzaji wa mazingira.

Akizungumza jijini Roma, Italia katika Kikao cha Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima kilichofanyika Septemba 2026, anasema wanawake bado wana changamoto za upatikanaji wa ardhi, fedha, teknolojia, huduma za ugani, masoko na nafasi za kufanya uamuzi.

Anasema serikali inaendelea kuwawezesha wanawake na vijana kupitia Mpango wa Kujenga Kesho Bora (BBT) unaolenga ifikapo mwaka 2030 kuunda ajira milioni 1.6, kusaidia biashara 200,000 za kilimo zinazomilikiwa na vijana na wanawake na kunufaisha watu milioni 10 katika vijiji 12,000.

Pia anasema hadi Juni 2026, Sh bilioni 1.59 zimetolewa kwa wanufaika 47 kupitia BBT huku wanawake ni 17 sawa na asilimia 36.

Mbali na Mwigulu, Oktoba 31, 2026 kwa nyakati tofauti, wadau wengine wametaja suluhisho baada ya kufanya mahojiano maalumu na mwandishi wa makala hii.

Mwenyekiti wa Bodi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Dk. Ananilea Nkya, anatoa ushauri kwa akina baba kwamba kama wanamiliki rasilimali mashamba wahakikishe wanawagawia watoto wao wa kike na kiume.

Kwa sababu gani? Anasema ukiangalia mwenendo wa siku hizi ndoa zinavunjika na kama mtoto wa kike ataachika lakini akiwa na ardhi ya kulima anakuwa na mamlaka nayo tofauti na atakavyoikuta kwa mmewe.

“Kama ana mashamba anaweza hata kuichukulia mkopo. Wanawake wana vikundi wanakopeshana na kuchangia maendeleo ya nyumbani na kama ana ardhi yake anaweza kuifanyia kazi kwa kulima na kuzalisha.

“Kama shamba ni lake anaweza kulima na kuvuna tofauti na likiwa la mwanamume kwa sababu wanawake wana vipaumbele zaidi kuliko wanaume. Wanawake wakiwa na kitu anachokimiliki na kukisimamia anaweza kufanya maendeleo,” anasema.

Familia nyingi anasema zina maendeleo kama mama anakuwa na uamuzi lakini hali hiyo ni tofauti kwa sababu wengi hawana.
“Wanawake wakiwa na uamuzi katika ardhi za kilimo wanaweza kufanya maendelo na kuwa makubwa. Pili, wanawake wenyewe wawe na kipaumbele cha kununua ardhi za kilimo kwa mkopo na hiyo ardhi itakuwa msaada mkubwa kwake lakini unakuta wanawake haiweki ardhi kama rasilimali muhimu.

“Unakuta mwanamke anakopa fedha ili amfanyie mwanaye sherehe ya kifahari lakini hakopi kwa ajili ya kununua ardhi ya kilimo. Ardhi ni rasilimali muhimu na afadhali sasa hivi wanawake waanze kuwanunulia watoto wao mashamba kama zawadi wakati wakiolewa kuliko kuwanunulia vyombo au makabati,” anasema.

Anawashauri wanawake wenzake kuondoka katika mfumo huo anaoutaja wa kimaskini na kuanza kuwaza maendeleo kwa kununua ardhi ya kilimo kwa sababu ndiyo rasilimali kubwa.

Pia anasema serikali hasa katika maeneo ya vijijini isaidie kuwapa kipaumbele kwa kuwapa mashamba wanawake huku mifumo ya kutomiliki ardhi inapaswa kubadilika ili waweze kuchangia maendeleo ya nchi na familia kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, anasema changamoto wanazokutana nazo wanawake ni kulima kwenye mashamba si yao.


“Unakuta labda ya baba yake au mme wake. Kwa sababu sheria nyingi za kimila huko vijijini haziruhusu mwanamke kumiliki ardhi kwa sababu wanajua ataolewa.


“Akiolewa atalima ya mme wake na asipoolewa atalima ya baba yake na akifariki baba yake, ataachiwa kaka na yeye ataazimwa mashamba kulima,” anasema.

Anatoa mfano wa Mtwara kwamba wakati wa mavuno ya korosho wanaume ‘wanasafisha ghala’ kwa kufukuza wake zao wa ndoa na kuoa wanawake wa pili.

“Wanatumia fedha za mavuno na zikiisha wanaanza kurudi kwa wake zao. Wake wakubwa kazi yao ni kulima na kupalilia mashamba ila wakati wa kuuza anaenda mwanamume kwa sababu ndie mwenye vitambulisho na akaunti ya benki.

“Fedha ikiingia anapotea na kwenda kuoa mwanamke mwingine na fedha zikiisha anarudi. Hata Mbinga ipo, kule wanalima kahawa na iko hivyo hivyo na migogro mingi inapatikana wakati wa mavuno,” anasema.

Katika ardhi, anasema sheria iko vizuri japo utekelezaji si mzuri kwa sababu mwanamke anatakiwa kuruhusiwa kurithi mashamba na akitaka ayauze au kuchukulia mkopo na si haki ya kuyatumia peke yake.

Hata kuuza mazao, anasema mwanamke hatakiwi kukatazwa bali ni mambo ya kimila tu yametawala kutokana na mfumo dume.

“Mwanamke analima lakini mwanamume anatambulika ni mmiliki wa hayo mazao unakuta wakati mwingine hata hakuwapo wakati mkewe analima. Tunatakiwa kubadilisha mtazamo wetu,” anasema.
Fursa ya mikopo anasema ipo na kuna baadhi ya benki zina madirisha maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wakulima.

“Kwa hiyo fursa zipo ila kuzijua ziko wapi na zinapatikanaje hilo ni jambo jingine na fursa itawasaidia zaidi wanawake ikiwa wanamiliki mashamba yao wenyewe,” anasema.

Ofisa Mikopo Mwandamizi wa Benki (jina linahifadhiwa kwa sababu si msemaji wa benki hiyo), anasema changamoto kubwa kwa wanawake ni umiliki wa mashamba.


“Kwa muundo ulivyo hasa maeneo mengi vijijini wanawake si wamiliki wa ardhi za mashamba na fursa nyingi za mikopo hazipatikani bila kuwa na dhamana ya ardhi. Sasa wanawake kuwezeshwa na kupata mikopo inakuwa ngumu.

“Kwa sababu taasisi nyingi za fedha zitawaambia waweke dhamana ambazo ni mashamba au nyumba. Lakini hawana umiliki wa moja kwa moja wa hizo dhamana kwa sababu ziko katika majina ya wanaume wao na hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa wao kukosa mikopo kwa kigezo hicho,” anasema.

Pia anasema ni benki au taasisi chache za fedha zinatoa mikopo bila kuzingatia masharti hayo ya dhamana.

Suluhisho la kukabiliana na changamoto hiyo, anasema ni urasimishaji wa ardhi kwa wanawake waweze kupewa hati za kimila.

“Ni rahisi kusema kwamba hati za kimila zinapatikana lakini mchakato wake ni mgumu. Wanawake nao wawe na mwamko wa kumiliki mashamba au ardhi kwa majina yao wenyewe,” anasema na kuongeza:

“Isiwe inatokea anapata fursa ya kumiliki ardhi halafu anasema amwandike jina la baba yake. Kama ni yake aandike jina lake, halafu benki zisijikite kutazama kwamba ardhi ndiyo kigezo cha mwanamke kukopesheka.

“Kwa sababu mkopo wa biashara unalipika kwa uwezo au mwenendo wa biashara husika na si uwapo wa dhamana kwani unaweza ukawa na dhamana lakini biashara haifanyi vizuri na hiyo dhamana unaweza usiiuze kwa ajili ya kufidia mkopo.”
Diwani Kata ya Mikocheni (CCM), Rehema Mandingo, anasema kwa sasa hivi kuna wanawake wanamiliki ardhi na mashamba.

Anasema mwamko upo japo inategemea ni kwa namna gani hasa maneo ya vijijini kutokana na mifumo dume na baadhi ya wanawake wanakubaliana na hali hiyo.

Kwa sasa anasema jamii inapaswa kukaa chini na kukubaliana kwamba ni haki ya kila mtu kumiliki ardhi ya mashamba ama iwe mwanamke au mwanamume kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo.

“Ni kweli bado tuna changamoto kubwa kwa baadhi ya maeneo katika vijiji kutowapa kipaumbele wanawake. Nadhani wengi wanaona wanawake wakimiliki mashamba watakuwa hawana nidhamu kwa waume zao.

“Ushauri wangu ni jamii yenyewe ikubali na kuona hali imebadilika hasa kwa wanawake waliochwa nyuma kwa muda mrefu katika masuala ya kumiliki mashamba na sasa hivi waachwe wamiliki,” anasema.

Mkulima wa Kata ya Kisangura wilayani Serengeti, Chacha Mtiti, anasema wanawake katika jamii nyingi hawana mamlaka ya kumiliki mashamba na anashauri elimu ianze kutolewa ili waanze kuyamiliki.

Kando na hiyo pia anasema mikopo kwa wakulima wanawake nayo ni changamoto pamoja ukosefu wa mitaji.
“Wanawake wakipata mitaji wanaweza kukodi mashamba na kuanza kufanya shughuli za kilimo maana ninapoishi ekari moja inakodishwa kwa Sh 60,000.

“Lakini kiwango hicho cha fedha kumilikiwa na mwanamke ni changamoto kubwa lakini akipata mtaji akakodi shamba atakuwa amesaidiwa kwa sababu mashamba yanakodishwa kwa miezi sita,” anasema.

Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Esther Mbusi, anasema fursa katika kilimo zipo ila wanawake wanashindwa kujitoa na kuzichangamkia kwa sababu ni waoga.

“Mikopo sasa hivi inapatikana kwa watu wote muhimu tu utimize masharti ya benki. Kuhusu kumiliki mashamba ni kweli kuna maeneo ni ngumu kutokana na kasumba tu ya mfumo dume lakini kwa sasa wanawake wapo wanaomiliki mashamba,” anasema.

Kwa zao la mkonge, anasema wanawake wako wengi katika shughuli ya kuongeza thamani ya bidhaa za zao hilo kuliko wanaume.

Pia anasema katika kilimo hawako wengi kwa sababu kuandaa shamba la mkonge ni kazi ngumu inayohitaji uvumilivu na wanawake wengi wanaogopa na kukata tamaa mapema ndiyo maana wanaume ni wengi.