Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa amesema miradi mingi ya umwagiliaji inatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18, hivyo kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa skimu zinazoendelea kujengwa katika kipindi cha mwaka 2022/2023 – 2023/2024 kutaongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 983,465.46 sawa na asilimia 81.9 na kufanya eneo la umwagiliaji kufikia hekta 1,200,000 ifikapo mwaka 2025 ambapo pia kutaongeza ajira 1,352,127.

Aidha Bw, Mndolwa amesemaTume ya Taifa ya mwagiliaji imefanikiwa kununua vitendea kazi kwa ajili ya watumishi wa Tume ikiwemo magari (48), mitambo 15 na magari makubwa (heavy trucks) 17 kwa ajili ya usimamizi, ufuatiliaji na ujenzi wa miradi ya umwagiliaji.

Aidha, Tume imefungua ofisi 121 za Wilaya za Umwagiliaji na kuajiri Watumishi 320 kwa ajili ya kusimamia miradi ya umwagiliaji katika ngazi ya mikoa na wŵilaya.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema mikakati ya serikali ni kuanza kutumia maji ya ziwa Tanganyika katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji ambapo hatua ya kwanza itaanza katika Mikoa ya katavi na Rukwa.

Bashe amesema kuwa baada ya Bunge la bajeti kumalizika kutafanyika upembuzi wa kina na yakinifu ili maji hayo yasafirishwe hadi Simiyu ambapo kuna ukame na Tabora.

“Baada ya Bunge la bajeti kukamilika tunatarajia kuanza kuyatumia maji ya ziwa Tanganyika katika shughuli za kilimo na uzuri mitambo tunayo naamini Jambo hili litafanikiwa,”amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule alisema serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia ametoa fedha zaidi ya sh.bilioni 67 kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji ambayo yatahudumia ekari zaidi ya 35,000.

“Mabwawa haya ni muhimu kwa Mkoa wa Dodoma kwasababu asilimia 72 ya wananchi wanaishi kwa kutegemea kilimo hivyo yataenda kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo na kuinua pato la Taifa na mwananchi mmoja mmoja,”amesema

By Jamhuri