Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Morogoro

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wamekutana kupitia kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TMA kilichofanyika katika ukumbi wa NSSF, Morogoro Aprili 30, 2024, kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Mamlaka kwa kuzingatia maazimio ya Baraza lililopita pamoja na kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025. Baraza hilo lilifunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari.

Mhe. Jaji Mshibe aliwapongeza watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya utoaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa wakati, taarifa ambazo zimesaidia wananchi na Taifa kwa ujumla kuchukua hatua stahiki. Pongezi hizo zilitolewa pia na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Emmanuel Mpeta, viongozi wa TUGHE Taifa, Wizara na TMA.

“Kwa namna ya pekee niendelee kuwapongeza Menejimenti na wafanyakazi wote wa TMA kwa kuendelea kutoa na kusambaza kwa wakati utabiri bora ambao unasaidia kuokoa Maisha ya watu na mali zao, ambapo kwa mvua za vuli zilizoambatana na EL NINO kiwango cha usahihi wa utabiri kilikuwa asilimia 98”. Alisema Mhe. Jaji Mshibe.

“Aidha, naendelea kuwakumbusha utendaji kazi wenye weledi na unaozingatia sheria na taratibu za kazi, sisi sote tukashirikiane kutimiza majukumu yetu ili kwenda sambamba na falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ya “Kazi Iendelee”.” Alisisitiza Jaji Mshibe.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza kuwa lengo la kikao hicho cha Baraza ni kujadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kufanya tathmini ya utendaji wa Mamlaka katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Aidha, taarifa ya utendaji kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 imeainisha kazi zilizotekelezwa katika kipindi tajwa, mafanikio yaliyopatikana, changamoto na mikakati ya kutatua changamoto husika.

“Mafanikio yaliyopatikana yamechagizwa na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania katika kuijengea Mamlaka uwezo wa kitaasisi, ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu, kununua vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa, pamoja na uboreshaji wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha Kigoma.” Alizungumza Dkt. Chang’a.

Baraza hili limejumuisha wajumbe kutoka vituo vyote vya TMA Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji kwa vitendo wa falsafa ya “Kwa maendeleo endelevu ya TMA, Tushirikishane, Tuimarishane na Tutegemezane” na pia ni utekelezaji wa Dira ya TMA “Kuwa kitovu bora cha huduma za hali ya hewa zinazowasaidia WADAU wote kufikia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii”.

By Jamhuri