Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tabora
Watu watatu wakazi wa Kijiji cha Iyombo-Nyasa, katika Kata ya Utwigu Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.wamepoteza maisha kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba walimokuwa wamelala usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo usiku wa kuamkia Aprili 26 mwaka huu kutokana na mvua kubwa iliyonyesha nyakati za usiku hivyo kuangukiwa na ukuta wa nyumba yao.
Ametaja waliofariki katika tukio hilo kuwa ni Rashidi Matoma (26), Chiku Mihayo (19) na Hamis Rashidi (2) ambao walipoteza maisha papo hapo baada ya kulaliwa na ukuta wa chumba walimokuwa wamelala.
Kamanda amebainisha chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mvua kubwa iliyonyesha kwa muda mrefu na kusababisha ukuta wa nyumba kuwaangukia.
Aleleza kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Wilaya hiyo na uchunguzi wa Daktari ulibainisha vifo hivyo kusababishwa na majeraha makubwa waliyopata kichwani na kutokwa na damu nyingi.
Ameongeza kuwa damu ilivujia kwenye ubongo hivyo kupelekea ubongo kushindwa kufanya kazi ikiwemo michubuko na kuvunjika maeneo mbalimbali ya miili yao kutokana na uzito wa ukuta huo.
Ametoa wito kwa wananchi kuwa makini hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zimeendelea kunyesha kwa wingi na kwa muda mrefu pasipo kukatika, na kuwataka kuchukua tahadhari ikiwemo kuhakikisha watoto wao hawachezi kwenye eneo lenye madimbwi.
Kamanda amebainisha kuwa kwa ujumla hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa huo ipo vizuri na wameendelea kufanya doria nyakati za usiku ili kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.