DAR ES SALAAM

Na Abbas Mwalimu

“Wengine tunaapa mdomoni tu, wengine tunaapa ndani ya moyo. Heshimuni viapo vyenu.” Mwisho wa kunukuu. 

Hii ni kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Aprili 2, 2022 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma baada ya kuwaapisha mawaziri, Mwenyekiti wa Baraza la Maadili na wajumbe wake, sambamba na Kabidhi Wasihi Mkuu na msaidizi wake.

Kauli hii ya Rais inaonyesha dhahiri kuwa baadhi ya viongozi wa umma wanamuangusha kwa kutoheshimu viapo vyao, hivyo kujikuta wanaangukia kwenye changamoto mbalimbali, ikiwamo kashfa ya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Bila shaka kauli hii inatokana na Rais kuchukizwa na taarifa za rushwa zilizoibuliwa katika ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Machi 30, 2022. 

Ikumbukwe kuwa ripoti ya TAKUKURU imebaini miradi ya maendeleo 222 yenye thamani ya Sh bilioni 79.14 yenye viashiria vya ufujaji na ubadhirifu wa fedha, ni wazi kuwa hali hii imemkera Rais, hivyo amewaapisha wajumbe wa Baraza la Maadili na Mwenyekiti wao ili kuipa nguvu Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kushughulika na watendaji wa umma wasio waadilifu.

Lakini je, uwepo wa Baraza la Maadili na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma pekee ni suluhisho la kuwa na watendaji waadilifu na wenye kuheshimu viapo vyao?

Na je, tatizo la msingi linalosababisha kuongezeka kwa vitendo vya rushwa katika utumishi wa umma ni lipi hasa?

Binafsi baada ya kuchunguza kwa kina nimebaini kuwa suala la kuongezeka kwa vitendo vya rushwa lipo kwa wananchi.

Katika makala hii nitaeleza sababu za kwa nini naona tatizo lipo kwa wananchi wa Tanzania.

Nitatumia nadharia ya utawala ijulikanayo kama ‘Principal-Agent Theory’ au kwa Kiswahili kisicho rasmi ‘Nadharia ya Mkuu-Wakala’ katika uendeshaji wa taasisi.

Nadharia hii imetazama uhusiano uliopo baina ya Mkuu dhidi ya Wakala wake katika usimamizi na uendeshaji wa taasisi kwa niaba ya Mkuu.

Nadhari hii inabainisha kuwa tabia na utendaji kazi wa Wakala hupimwa na Mkuu/Wakuu na hao ndio wenye kuweza kutoa adhabu dhidi ya utendaji mbovu wa Wakala (Rejea alichoandika Baez-Camargo, 2011:6).

Nadharia ya Mkuu-Wakala inafafanua kwamba ‘Wananchi’ ndio ‘Wakuu’, ambapo wananchi hawa hukabidhi mamlaka na madaraka kwa ‘Serikali’ ambayo huwa ndio ‘Wakala’ ili Serikali hiyo iweze kufikia azima ya hao wananchi. 

Baez-Camargo na Jacobs (2013) wao wamesisitiza zaidi kuwa serikali kama ‘Agent’ ina wajibu wa kutoa huduma zote za msingi kwa ‘Principal’ ambao ni wananchi.

Kwa kifupi nadharia hii inaweka bayana kuwa uwajibikaji wa serikali hutokana na ukali wa wananchi.

Katika kukazia hili, Achen na Bartels (2002), Healy na Malhotra (2010), Lens (2012) na Lupia na mwenzake McCubbins (1998) waliweka bayana kwa kusema: “Public accountability is a function of the capabilities of principals to judge the performance of their agents.”

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi ni kwamba: “Uwajibikaji katika utumishi wa umma ni zao la uwezo wa Wakuu kutoa uamuzi/kuamua dhidi ya utendaji wa Wakala wao.”

Kwa kuzingatia nadharia hii ya Principal-Agent na kwa mujibu wa Ibara ya 8, Ibara ndogo ya Kwanza, Kifungu ‘a’ cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inafafanua kwamba: “(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.” Hivyo, raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye ‘Principal’, ambao wamekabidhi madaraka na mamlaka kwa ‘Agent’ ambayo ndiyo serikali yao inayoongozwa na Rais Samia.

Kwa mantiki hiyo, ninaamini raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wana wajibu mkubwa wa kumsaidia Rais Samia katika kupambana na viongozi wasio waadilifu na wala rushwa na si kumuachia peke yake.

Hivyo binafsi ninaamini tatizo la kuongezeka kwa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watumishi wa umma nchini linatokana na wananchi wa Tanzania kutojua wajibu wao ambao umeainishwa kwenye ibara ya 8(1,a) ya Katiba ama kwa bahati mbaya au kwa kutoelezwa kinagaubaga juu ya wajibu wao huu mkubwa kwa nchi na wale waliokabidhiwa wajibu wa kuwaeleza ukweli.

Umuhimu huu wa wajibu wa wananchi unatokana na ukweli kwamba rushwa inaathiri sana utoaji na utolewaji wa huduma za msingi, haki na inaathiri vibaya ukuaji wa maendeleo ya nchi.

Lakini licha ya ukweli huu kuwa mwananchi ana umuhimu mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa, Gailmard (2012) na Baez-Camargo (2010) wao wanasema rushwa hutokana pia na mifumo dhaifu ya ufuatiliaji na utekelezaji hafifu wa sheria za nchi husika. 

Hili lina ukweli kiasi gani? Bila shaka tafiti za kina zinapaswa kufanyika kubaini ukweli.

Kwa upande mwingine inawezekana wananchi hawa hawajawezeshwa kwa kina kuweza kujua majukumu yao dhidi ya viongozi wao.

Ni ukweli ulio wazi kuwa wananchi huwa hai (active) sana katika mapambano dhidi ya rushwa endapo wakipewa nyenzo ambazo ni rahisi kutumia, zenye kuaminika na zinazoonekana kwa ushiriki wa mwananchi kama alivyobainisha Elers na wenzake (2010).

Je, wananchi wa Tanzania wana nyenzo? Kama zipo zina urahisi kiasi gani wao kuzitumia kufikisha taarifa? Je, wanaziamini hizo nyenzo? Nadhani haya ni maswali ya msingi kwa serikali kujiuliza.

Kama nyenzo zipo na bado zinaonekana hazikidhi haja ya mahitaji, basi bila shaka kuna mwanya (gap) kati ya mifumo iliyopo ya kupambana na rushwa na mtazamo wa wananchi dhidi ya mifumo hiyo. Ripoti ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na utofauti wa aina hii iliyojulikana kama ‘Crime and Culture’ imebainisha hali hiyo pia.

Njia ya kupita

Mwaka 2004 Benki ya Dunia ilibainisha vipengele vitano vya uhusiano wa kiuwajibikaji baina ya Principal (Wananchi) na Serikali (Agent), vipengele hivi ni mamlaka, rasilimali, utendaji, taarifa kuhusu utendaji na utekelezaji.

Kwa kuzingatia Katiba, mamlaka iliyopewa serikali na watendaji wake kwa niaba ya umma au wananchi katika kusimamia vema rasilimali za umma yanahitaji taarifa juu ya utendaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Kwa hoja hiyo, mrejesho kwa wananchi unatakiwa katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi. Kimsingi mrejesho huo unatakiwa uwe kwa uwazi na wenye kueleweka.

Hivyo, ili kuleta uwajibikaji na uadilifu katika utendaji wa shughuli za umma kwa niaba ya wananchi yafuatayo yanafaa kufanywa na serikali.

Mosi, kuwekeza kwenye ‘Uwajibikaji wa Jamii’ au ‘Social Accountability’ ambao utawezesha ufuatiliaji wa rushwa na viashiria vyake kupitia wananchi wenyewe (Rejea taarifa ya Benki ya Dunia, 2004).

Hili litafanyikaje?

Linaweza kufanyika kwa mambo matatu ambayo ni:

(i) Kutumia Ukaguzi wa Jamii (Social Audit) ambapo serikali kwa kushirikiana na wananchi itakuwa na uwezo wa kufuatilia, kuchakata taarifa zilizokusanywa na kufanyiwa upembuzi wa kina kwa ushirikiano na wananchi.

Kwa msingi huo hapa kunatakiwa kuwe na  nyenzo au mfumo ambao utakuwa ni rahisi na wenye kuaminika kwa wananchi kutoa taarifa za rushwa na ubadhirifu wa fedha na mali za umma.

Kwanza, ni kutumia mfumo shirikishi wa uandaaji Bajeti (Participatory Budgeting) katika ngazi za halmashauri.

Wananchi washirikishwe katika uandaaji, ufanyaji uamuzi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti ili kuleta dhana ya ushirikishwaji kwa mapana. Pili, kuwekeza kwenye teknolojia.

Kuandaliwe ‘App’ au Tovuti (Website) ambayo wananchi wataweza kutoa taarifa za rushwa na ubadhirifu wa mali za umma pasipo kujulikana (anonymous). Tovuti hiyo iwe rahisi kutumia kwa kila mwananchi.

Pia itumike kama kanzidata ya kukusanya taarifa mbalimbali za rushwa na upimaji wa utendaji kazi wa watumishi wa umma.

Tatu, serikali iandae Mikataba ya Utendaji Kazi (Performance Contracts) kwa watumishi mbalimbali kama vile mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya,  makatibu wakuu na wakurugenzi na wapimwe kwayo.

Wananchi wakijua kiongozi fulani amepewa mkataba afanikishe jambo fulani wataweza kumsukuma atekeleze hilo jambo, ni kama vile makocha wa timu za mpira wa miguu wanapoajiriwa na kuambiwa lengo la kwanza la klabu iliyomuajiri ni kuchukua ubingwa au afike hatua fulani katika ligi ya mabingwa.

‘Performance contracts’ husaidia kuchechemua ubunifu kwa watumishi  wa umma, hivyo kuleta ufanisi katika utendaji wao.

Nadhani kama yakifanyika hayo yataweza kuipa nguvu TAKUKURU, Baraza la Maadili na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika utendaji wao. Lakini pia yataweza kuirahisishia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya kazi zake kwa wepesi.

+255 719 258 484

By Jamhuri