Na Cresensia Kapinga, Songea.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeombwa kuona umuhimu wa kukifanyia ukarabati chuo cha Afya na Sayansi shirikishi cha Songea ambacho kipo katika hali mbaya kufuatia majengo ya chuo hicho kuwa chakavu.

Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho ambao waliomba majina yao yahifadhiwe walisema kuwa hali ya majengo ya chuo ni mbaya kwa kuwa yamechakaa na hayajafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.

Wanachuo hao walidai kuwa mabweni wanayotumia yamekuwa na matatizo mengi yanoyosababisha chumba kimoja kulala zaidi ya wanachuo wawili kwa kuwa Kuna huaba mkubwa wa mabweni.

Moja wapo ya majengo ya chuo cha Afya na Sayansi shirikishi kilichoko Songea

Walisema kuwa madarasa yaliyopo hayakidhi mahitaji ya wanachuo waliopo kwani baadhi yao wamelazimika kusomea kwenye bwalo la chakula jambo ambalo linaonekana kuwa ni kero kubwa kwa wanachuo hivyo wameiomba serikali namna ya kusaidia kuyakarabati na kuongeza kujenga madarasa mapya ili kuondokana na adha iliyopo.

Walisema kuwa chuo hicho cha Afya na Sayansi shirikishi ambacho kilijengwa tangu mwaka 1973 kimekuwa kikidhalisha wataalam wengi sana wa Afya hapa nchini lakini hakina uzio jambo ambalo linahatarisha usalama wa wanachuo na mali za chuo hicho.

” Tunaomba serikali kupitia Wizara ya Afya ikipe kipaumbele chuo kwenye maswala ya ukarabati pamoja na kuongeza kujenga madarasa kwani Elimu bure imekuwa chachu kwa wazazi wao kupeleka watoto shule na wengi wanapomaliza masomo yao ya Sekondari wanakuwa hawana uwezo wa kuwapeleka vyuo vya binafsi ambavyo vinaada kubwa ambayo wazazi wetu wengi hawana uwezo wa kumudu gharama”

Baadhi ya walimu wameonesha kuwa na masikitiko makubwa kona chuo hicho kulivyokuwa na idadi kubwa ya wanachuo huku chuo hicho kikiwa na majengo chakavu hivyo wameiomba serikali kutenga bajeti kwaajiri ya ukarabati na ujenzi wa madarasa mapya ambayo yatakidhi mahitaji ya wanachuo.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha afya na sayansi shirikishi Dkt. Godfrey Mdede amekiri kuwepo kwa matatizo yanayolalamikiwa na wanachuo na kwamba tayari amewasilisha kero zote zinazokikabili chuo hicho wizarani na kwamba bajeti ya mwaka huu ya wizara ya Afya inaweza ikafanyia kazi.

Hata hivyo alifafanuwa kuwa baadhi ya changamoto ya chuoni hapo zimekuwa zikitatuliwa kutokana na fedha za mapato ya ndani ambazo zinatokana na ada za wanachuo kama kulipia maji, umeme, ukarabati mdogo pamoja na shughuli za kila siku.

Aidha amesema kuwa chuo hicho ambacho kimejengwa mwaka 1973 kinauwezo wa kuchukuwa wanachuo zaidi ya 300 lakini kwa Sasa kutokana na ubovu wa baadhi ya majengo na uchache wa vyumba vya madarasa wanachukuwa wanafunzi 250 jambo ambalo limekuwa ni kero kubwa kwa wazazi wanahitaji watoto wao kusoma chuoni hapo .

By Jamhuri