Na Mwandishi Wetu

Wiki iliyopita, imezinduliwa wiki ya maji hapa jijini Dar es Salaam, maadhimisho hayo yameanza Machi 16 na kuhitimishwa Machi 22, katika uzinduzi huo uliohusisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, viongozi kadhaa walitoa hotuba, kutokana na umuhimu wa sekta ya maji hapa nchini, Gazeti la JAMHURI, linakuletea hotuba za viongozi hao neno kwa neno. Fuatilia…

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo

Idadi ya watu Mkoani kwetu kulingana na sensa ya mwaka 2012, tuko takribani watu milioni moja na laki moja, ssa takwimu tulizonazo za wataalam wetu wanatwambia watu wanaopata maji safi na salama ni takribani laki saba kwa wastani.

Mamlaka za maji ambazo zinaendelea kuwasaidia wananchi wetu wa Mkoa wa Pwani zipo sita na zimegawanywa katika katika makundi mawili, daraja A ni Dawasa na Dawasco hawa wanasaidia sana katika upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Pwani, daraja B, tunazo mamlaka tano, tunazo mamlaka za maji katika wilaya za Rufiji, Mkuranga, Kisarawe na Kilindoni-Mafia.

Wenzetu wa Halmashauri ya wilaya za Kibiti na Chalinze ndio kwanza zimeanzishwa lakini pia wako mbioni kuanzisha mamlaka za maji kwenye maeneo yao.

Hadi kufikia mwezi Disemba mwaka jana, mkoa wetu wa Pwani uliweza kutoa huduma ya maji vijijini kwa asilimia 62.5, mwanzo nilitoa takwimu za wastani kwa ujumla, bado tuko chini ukilinganisha na lengo la kitaifa la kufikia asilimia 85. Hata katika kutoa huduma za maji kwenye miji iliyoko kwenye makao makuu ya halmashauri za wilaya bado hatujafikia lengo la kitaifa ambalo ni asilimia 90.

Wenzetu wa Dawasa na Dawasco, mtaona kwa takwimu hizi bado tuko nyuma na hivyo tunahitaji msukumo wa pamoja, Bodi ya Wakurugenzi way a Dawasco na menejimenti inabidi itazame namna ya kutatua changamoto hii ya ukosefu wa maji.

Dawasco ndiyo yenye jukumu kuu la huduma ya utoaji wa maji safi na kushughulikia maji taka kwa jiji la Dar es Salaam, Kibaha na Bagamoyo katika mkoa wa Pwani. Shirika la Dawasco ni wadau wakubwa katika mkoa wetu wa Pwani, katika kutoa huduma ya maji katika maeneo ya Bagamoyo mjini, Mlandizi, Kibaha Mjini pamoja na maeneo ya pembezoni ya maeneo hayo niliyotaja.

Niwapongeze sana Dawasco kwa kuona umuhimu wa kupeleka maji katika maeneo ya Chalinze, Lugoba, Mboga. Mkoa wetu unategemea Dawasco kutoa huduma ya maji katika wilaya za Kisarawe na Mkuranga, hata hivyo bado kuna tatizo la upatikanaji wa maji katika mji mkongwe wa Kisarawe.

Nimeona taarifa ya Dawasco ya upatikani wa maji Kisarawe, wananchi wale wanataka maji, Kisarawe tunataka maji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, sasa tumesubiri miezi tisa, tena tusubiri miezi 15? Hapa mgeni rasmi sijafurahi. Kama tumeweza kujenga ukuta wenye kilomita 25 huko Mererani kwa muda mfupi, leo tunataka tuaminishwe kwamba tusubiri miezi 15 kuanzia Aprili kupata maji Kisarawe.

Najua utandikaji wa mabomba unahitaji utaalam, maana hata mimi ni mhandisi, lakini maji pale yapo ni kutoboa bomba tu…sijui kuna ujenzi wa miundombinu mingine, sisi tunataka maji tu Kisarawe tena yapatikane haraka na si katika kipindi cha miezi 15 kama inavyosemwa.

Dawasa mtueleze vizuri kama wananchi wa Tanzania wameona na kusikia mambo ya ujenzi wa ukuta pale Mererani katika muda mfupi, je, kinashindikana kitu gani kupeleka maji Kisarawe?

Hivi karibuni kulikuwa na upanuzi wa Ruvu juu, ambao mimi nilishiriki katika uzinduzi wake, upanuzi wa mradi huo ilikuwa ni ndoto iliyosubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa mkoa wa Pwani, hususani wilaya ya Kibaha na sehemu kubwa ya jiji la Dar es Salaam.

Ndani ya muda mfupi tangu mitambo ianze kufanya kazi wananchi wapya zaidi ya1500, katika maeneo ya Mlandizi, Misugusugu wameunganishwa kwenye huduma za maji. Tunatoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais John Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano katika kutatua changamoto za kero ya maji.

Kwa sasa Dawasco wanaendelea na uhamasishaji wananchi wengi zaidi ili waweze kuunganishiwa maji, maboresho ya mitambo hiyo ya uzalishaji maji itasaidia sana upatikanaji wa maji katika viwanda vilivyoko Pwani. Bado ninawaomba Dawasco na Dawasa kupitia upya ramani zao za utoaji huduma za maji ili kuendana na hali ya sasa hasa kwenye viwanda.

Niliwaelekeza wakuu wangu wa wilaya kwamba ni lazima tufike katika mkutano huu ili tupate majibu kuhusu matatizo ya maji kwa wananchi wetu na kuhakikisha wanapata maji safi na salama, lakini pia katika maeneo ya uwekezaji wa viwanda kupatiwa maji, maana huko wana mahitaji mahsusi. Kwa mfano Kisarawe wana eneo lenye ekari 1600 la uwekezaji limeshapimwa na lina kila kitu, lakini wawekezaji hawawezi kwenda kwa sababu wanasema hakuna maji.

Mkuu wa wilaya ya Kisarawe angependa kupata majibu sahihi ili akikutana na wawekezaji apate jambo la kuwaambia, hata Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo atahitaji kujua namna ambavyo upatikanaji wa maji utawesaidia viwanda zaidi ya 100 vitakavyojengwa Bagamoyo. Baada ya kipindi cha miaka 5-10 kutakuwa na uendelezaji wa eneo la ekari 2200 kwa ajili ya jiji la viwanda (industrial city) maji yako wapi?

Kuna eneo la Kamal pale Kerege Bagamoyo, kuna kila kitu isipokuwa maji, ndio maana tunataka maji ili kupambana na uwekezaji mkubwa. Sasa tunahitaji kupata maji kwa ajili ya wananchi wetu pamoja na viwanda.  Lakini napenda kuwapongeza sana dawasco, baada ya kuona mpango mkakati wetu wa uwekezaji viwanda Pwani, wamefumua bajeti yao.

Suala la ulinzi na usalama wa miundombinu pamoja na vyanzo vya maji, hivyo sisi jukumu letu kubwa ni kulinda vyanzo hivyo. Maana tusipolinda Dar es Salaam na Pwani haitakuwa na maji na hiyo ni hatari zaidi.

Naomba nihitimishe kwa masuala sita, upanuzi wa bomba la maji umefanyika lakini wananchi wengi walioko ndani ya eneo la mradi huo bado hawajaunganishwa na huduma ya maji kwa hiyo naomba kazi inayofanywa sasa hivi dawasco iongezewe kasi ili wananchi waweze kupata maji. Ninadhani eneo linapopita bomba la maji kutoka Ruvu mpaka Dar es Salaam, mita 12 kila upande, wananchi walioko eneo hilo wapate maji.

Jambo jingine ni dawasco kuchukua miradi ya maji vijijini ambayo chanzo chake cha maji kinatokana na bomba linalohudumiwa na dawasco, maana kumekuwepo na changamoto kadhaa kwa wananchi ambao wanahudumiwa na miradi ya maji vijijini.

Suala jingine ni ujenzi wa viwanda Pwani, tunajenga kwa kasi kubwa, kama ambavyo tumeomba umeme na mahitaji yetu yanafahamika, vivyo hivyo tupate maji na maji yale tuyapate sasa. Haiwezekani tunahamasisha wawekezaji lakini mpango tulionao ni kuleta maji katika kipindi cha miaka 5-10.

Maeneo ya mkoa wa Pwani, yanayohudumiwa na dawasco yana changamoto ya uondoaji wa maji taka, tunaomba watusaidie kushughulikia suala hili ili kutoruhusu madhara yatokanayo na kutoshughulikia vema maji taka. Ikitokea kuna kukatika kwa maji basi taarifa zitolewe kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wilaya pamoja na vyombo vya habari ili kutoathiri shughuli za uzalishaji viwandani lakini pia kuondoka kero kwa watumiaji wa majumbani.

Mradi wa Stigler’s Gorge

Nimesikiliza uwasilishaji wa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja, kwamba mtaweza kutoa maji Rufiji ifikapo 2032, nimeshangaa wakati sasa tunajenga Stigler’s, kwa nini tusijenge mtandao wa maji utaokwenda sambamba na mradi huo wa umeme. Maana wakati mnasubiri 2032, mtakuta mahitaji yameongezeka sana.

Mmesema kuhusu mradi wa Kidunda na Mpera, bado mimi naona hiyo ni miradi midogo midogo tu, tunatakiwa kwenda kwenye miradi mikubwa ambayo itakuwa suluhisho la matatizo ya maji. Kama tumeweza kutoa maji Ziwa Victoria hadi Shinyanga na baadaye Tabora, tunashindwa kitu gani kutoa maji kwenye mradi wa Stigler’s gorge hadi Chalinze?

Kwanza nimeambiwa kwamba hilo bwawa la mradi wa Stigler’s litakuwa na mita 3000 kutoka usawa wa bahari, hata bila mashine maji hayo yanaweza kusukumwa kwa nguvu za asili mpaka Chalinze na wananchi wakapata maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Dawasco Mhandisi Cyprian Luhemeja

Kwa sasa upatikanaji wa maji jijini Dar es Salaam ni asilimia 75, huku ikitarajiwa kupanda hadi asilimia 95 mwaka 2020.

Shirika la Dawasco kwa sasa lina uwezo wa kuzalisha maji lita za ujazo milioni 502 kwa siku. Huku mahitaji halisi kwa wakazi wote wa Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa sasa ni lita za ujazo milioni 544 kwa siku.

Kiwango cha upatikanaji wa maji ni sawa na asilimia 92 ya mahitaji halisi ya wakazi wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambao wako zaidi ya Million 7.2   inayohudumiwa na Dawaco, tofauti kati ya uzalishaji na mahitaji halisi ni lita za ujazo milioni 42 kwa siku.

Changamoto kubwa zinazolikabili sharika la Dawasco ni usambazaji wa huduma maji katika jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Dawasco tumetenga kiasi cha Shilingi bilioni 62, kwa ajili ya kupanua mtandao wa maji katika eneo la utendaji kazi wake.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19, Dawasco itatumia wataalamu wa ndani katika kuwekeza katika upanuzi wa mtandao wa maji. Utaratibu huu utatumia pesa ya ndani ambayo shirika limetenga jumla ya Shilingi bilioni 62.

Kiwango hiki kitatumika katika maeneo yenye ufinyu wa mtandao. Maeneo yafuatayo yatapewa kipaumbele kikubwa: Tabata (Kisukuru,Kinyerezi,Kanga) Temeke na Kigamboni (uendelezaji wa visima vya Kimbiji na Mpera kwa awamu) Kimara na Kibaha (nguvu kubwa itaelekezwa katika maeneo ya viwanda).

Dawasco imepata Jumla ya Kiasi cha Fedha cha Shilingi bilioni 114 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya upanuzi wa mtandao. Kazi hii ya upanuzi itaanza mwezi Juni 2018.

Changanyikeni, Jumla ya kilomita142.4 zitalazwa na tunatarajia kuunganisha kaya 3,000, Vikawe, jumla ya kilomita136.5 zitalazwa na tunatarajia kuunganisha kaya 1000, Goba jumla ya kilomita 60.6 zitalazwa na tunatarajia kuunganisha kaya 3000, Bunju, Wazo, Kunduchi, na Salasala jumla ya kilomita 546.2 zitalazwa na tunatarajia kuunganisha kaya 60,000, Bagamoyo jumla ya kilomita 61.6 Km tunatarajia kuunganisha kaya 3000.

Ujenzi wa Mifumo Mifupi ya Usambazaji kutumia visima virefu. 

Jumla ya fedha Shilingi bilioni 12 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huu. Utaratibu huu utahusu maeneo yaliyoko mbali na Mtandao wa Maji kutoka katika mitambo ya Ruvu Juu na Chini. Tathmini imekwisha anza na maeneo yafuatayo yatapewa kipaumbele katika utaratibu huu.

Ponde Water Supply Project katika kata ya Toangoma-Ponde na Malela, yenye wakazi 3236 itapata Shilingi milioni 300, Kilima Hewa iliyoko kata ya Toangoma yenye wakazi 5920 itapata shilingi milioni 400, Mwanamtoti-Butiama water supply project iliyoko kata ya Kijichi yenye wakazi 15833, itapata shilingi milioni 400, Dovya-Chamazi Water Supply Project iliyoko kata ya Chamazi yenye wakazi 20,000 itapata shilingi milioni 400 na Mwembe Bamia Water Supply Project iliyoko kata ya Chamazi yenye wakazi 3910 itapata shilingi milioni 200.

Katika Manispaa ya Ilala mradi huo utatekelezwa Zingiziwa Water Supply Project katika kata ya Zingiziwa-Ngobedi, yenye wakazi 32,073 itapata shilingi milioni 750, Zingiziwa Water Supply Project katika kata ya Kimwani yenye wakazi 1520 itapata shilingi milioni 100, Buyuni Water Supply Project katika kata ya Mgeule, yenye wakazi 3196 itapata shilingi milioni 100, Msongola Water Supply Project katika kata ya Msongola yenye wakazi 8500 itapata shilingi milioni 200, Yange yange Water Supply Project katika kata ya Msongola yenye wakazi 4188 itapata shilingi milioni 250.

Mbopo iliyoko katika kata ya Mabwepande yenye wakazi 3972 itapata shilingi milioni 450, Mbezi Ndumbwi katika kata ya Mbezi Juu yenye wakazi 8199 itapata shilingi milioni 250, Mbezi Mtoni katika kata ya Mbezi Juu, yenye wakazi 7850, itapata milioni 200, Kilimahewa Juu iliyoko kata ya Wazo, yenye wakazi 8136 itapata shilingi milioni 350, Nyakasangwe iliyoko kata ya Wazo yenye wakazi 7650, itapata shilingi milioni 300 na Madale iliyoko kata ya Wazo yenye wakazi 6750 itapata shilingi milioni 300.

Katika mwaka wa fedha 2018/19 shirika limepanga kutumia bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni 159. Katika kiwango hiki asilimia 40 sawa na shilingi bilioni 64 zitatumika katika kupanua mtandao na hivyo kusogeza huduma kwa wananchi.

Miradi ya mifupi ya uondoshaji majitaka

Tofauti na Mfumo rasmi wa uondoshaji maji taka unao tumia bomba (Sewerage System) Dawasco imebuni utaratibu wa uondoshaji maji taka kwa kutumia mfumo mdogo (off Grid sanitation system)

Mfumo huu utahusiana sana na maeneo yenye Msangamano wa watu na ambayo hayajapimwa kama Buguruni, Tandale, Vingunguti maeneo ambayo hayajapiwa. Jumla ya Kiasi cha shilingi bilioni 25 kimetengwa kwa ajili ya maboresho haya.

 

By Jamhuri