Kamishna lawamani kutaka kumega ardhi

MOROGORO

Na Aziza Nangwa

Taasisi ya Tretem Network of Schools Limited imemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, kuingilia kati kitendo cha Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Morogoro, Frank Minzikuntwe, kutaka kumega eneo lao kisha apewe mtu mwingine.

Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Julius Chami, amesema eneo hilo wanalimiliki kihalali lakini Frank amewaandikia barua ya siku saba kutaka hati ibadilishwe na limegwe kipande.

Amesema kitendo cha kumwachia mvamizi eneo lao wamekipinga hadi wakaenda mahakamani na ulitolewa uamuzi waendelee na ujenzi na wavamizi waondoke na wakaondoka, lakini mmoja anayekingiwa kifua na Frank amebaki ndiye anawashinikiza waachie eneo hilo.

Pia amesema eneo hilo walilipata kihalali kupitia Manispaa ya Morogoro baada ya kubadilishana nao kiwanja chao kilichokuwa Kata ya Kilakala, eneo la Kigurunyembe lenye ekari tano ili wapewe mbadala kwa ajili ya kupisha ujenzi wa shule ya sekondari ambayo kwa sasa inafanya kazi.

Amesema kiwanja hicho kilitolewa kwa serikali kwa matumizi ya umma na wao walikinunua mwaka 1995 na mwaka 1997 walianzisha Chuo cha Uandishi wa Habari Morogoro (MSJ) kikiwa chini ya mwavuli wa Tretem.

Vilevile amesema baada ya kujenga vyumba vitatu na wakati wanaendelea na ujenzi alikuja Diwani wa zamani wa Kata ya Kilakala, Anthonia Sanga, ambaye aliwaomba eneo hilo kwa ajili ya kujenga shule ya sekondari ya kata na wakafanya mazungumzo wakiwamo watu wa manispaa.

Amesema baada ya mjadala wa muda mrefu walikubali kupewa eneo mbadala lililopo Tungi.

“Tuliamua kukubali kwenda mbali ya mji kwa sababu ya kuzingatia masilahi ya umma, hasa watoto wasiende mbali. 

“Sababu kubwa ni eneo lao halisi lililokuwa lijengwe sekondari, lilikuwa kata nyingine, kwa hiyo tuliona hoja yao ina mashiko, tulikubali kuwaachia kwa makubaliano maalumu ya kisheria yaliyosimamiwa na maofisa ardhi wa manispaa,” amesema.

Aidha, amesema baada ya hapo viwanja hivyo vilibadilishwa kisheria na wao wakapewa hati ya ofa na Manispaa ya Morogoro inayosomeka Plot 477, Kitalu E, Tubuyu, Postcode 67122 Tungi Morogoro na kiwanja kina ukubwa wa hekta za mraba 2.697, kimewekwa vigingi namba BAJ321-329 na kilikuwa na hati ya umiliki wa miaka 99.

Amesema baada ya kupewa kiwanja mbadala katika eneo jipya la Tungi hawakufanya ujenzi kwa kipindi hicho.

“Wakati tumeacha bila kujenga tukitafuta fedha, maofisa ardhi wa manispaa wakaanza kuingiwa tamaa na kukimega kipande cha eneo letu na kuuza. Sisi hatukuwa na taarifa, tukakuta watu wamejenga katika eneo letu, tulichukua hatua ya kuwakamata na kuwapeleka mahakamani.

“Mahakama ya Mwanzo nao wakatushusha katika Baraza la Ardhi la Wilaya, huko mwenyekiti akatoa uamuzi kiwanja kipimwe upya, sisi tulikataa na kukata rufaa kwenda Mahakama Kuu Kitengo ya Ardhi kupinga kiwanja chetu kumegwa.

“Na tulitaka kiwe vilevile kama awali, kwa sababu tuliamua kuacha kiwanja chetu cha mjini, tulikwenda kijijini Tungi kuanza upya, pia tukaacha jengo na vifaa vya ujenzi katika eneo hilo kwa manufaa ya umma,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi – Morogoro iliamuru kiwanja chao wapewe vilevile na wavamizi wahame na kuwalipa fidia ya Sh milioni 10.

Amesema baada ya muda waliporudi kuendeleza eneo hilo, wakatokea watu wa kanisa nao wakadai kuuziwa eneo hilo na maofisa ardhi wa Manispaa ya Morogoro kabla yao.

“Kanisa hilo lilitupeleka mahakamani na sisi lengo letu tulitaka manispaa ishirikishwe katika kesi ili itoe kauli kiwanja ni cha nani, lakini haikuwa hivyo, badala yake manispaa iliomba wote watatu tuzungumze nje ya mahakama.

“Mwisho, manispaa walikiri kufanya uovu huo na wakatuamuru sisi tuendelee na ujenzi na shirika hilo walipewa kiwanja mbadala, hivyo manispaa ikalazimika kuandaa hati mbili,” amesema.

Pia amesema wakiendelea kuwatoa watu katika kiwanja chao, manispaa ilikata sehemu ya eneo lao na kumpatia mvamizi mmoja ambaye hadi sasa bado yupo akidai amri ya mahakama si halali.

“Baada ya mvamizi kuendelea kukaa katika eneo letu huku tukiendelea na ujenzi, tulikwenda mahakamani kukazia hukumu ili aondoke, lakini yeye alikwenda kwa Frank ambaye naye ametuandika barua ya amri, inayotutaka kwenda manispaa kubadilisha hati yenye kasoro ya hekta za mraba 2.166 ili kiasi kinachobaki tumwachie mvamizi.

“Kwa kweli amri hiyo hatukuridhika nayo, tukaandika barua kwa waziri mwenye dhamana ili atusaidie kutatua mgogoro wa kudhulumiwa kiwanja chetu na kamishna akishirikiana na maofisa ardhi wa manispaa,” amesema.

Aidha, amesema Ofisa Ardhi wa Manispaa, Valency Huruma, amesema ni kweli manispaa ilitoa kiwanja kwa Tretem lakini suala la kupunguza eneo wao hawana mamlaka ila mwenye uwezo ni kamishna wa ardhi wa mkoa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Tungi, Ibrahim Chombo, amesema awali eneo hilo walipewa Tretem ili kujenga chuo na kuhusu wavamizi amesema  hawakufuata sheria na wameuziwa na madalali.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Tungi, Ramadhani Kambi, amesema eneo hilo ni la Tretem na lina vigingi na wanalimiliki kihalali na wavamizi waliuziwa na matapeli.

Majirani

Mwanaidi Rajabu amesema eneo hilo ni la MSJ kwa miaka mingi na linatambulika. Anahoji, waliovamia wamepata wapi ruhusa?

Naye Joseph John amesema anafahamu muda mrefu eneo hilo ni la Tretem na si la mwingine.

Kwa upande wake, msimamizi wa eneo hilo, Mohamed Juma, amesema amekuwa akipelekwa polisi na mvamizi kwa sababu anataka aendelee kukaa katika eneo hilo wakati si lake.

Kamishna ajibu 

Frank amekiri kutoa barua ya kuitaka Tretem kubadilisha hati ndani ya siku saba lakini amedai ameshaagiza manispaa kuhakiki upya na kama wana haki wapewe, na amesema shauri hilo limekwenda wizarani na wanasubiri uamuzi.

Diwani wa zamani

Sanga amesema eneo hilo ni la Tretem na wana haki ya kuachiwa kiwanja chao cha awali kwa sababu wamewasaidia watu wa Kilakala.

“Tulikuwa hatuna eneo la kujenga shule, kwa jitihada zangu nilikwenda kuwabembeleza Tretem wahame mjini na kwenda Tungi.

“Mwisho, walivyokubali tuliwapeleka kule kisheria na wakapewa hati halali na wameacha kiwanja cha thamani kwenda kijijini, naomba waachwe kwa sababu wametusaidia watoto walikuwa waende mbali kusoma, lakini wao wametusaidia,” amesema.