Rais John Magufuli alipoingia madarakani alionyesha wazi kutoshabikia suala la ‘semina elekezi’ kwa wateule wa ngazi mbalimbali.

Alipotangaza Baraza la Mawaziri alisema wazi kuwa hana mpango wa kuendelea na semina elekezi, bali lililo muhimu ni kwa wateule kuchapa kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni.

Bila shaka uamuzi wa rais ulilenga kupunguza matumizi mabaya ya fedha za umma kama ilivyopata kuonekana kwa mtangulizi wake.

Lakini kadiri siku zinavyokwenda, hata yeye mwenyewe naamini anaanza kuona umuhimu wa semina elekezi – hata kama si kwa staili ile iliyotumia fedha nyingi za walipa kodi.

Kwenye salamu za mwaka mpya wa 2019, akilihutubia taifa, rais aligusia jambo muhimu sana. Lilihusu utendaji kazi wa baadhi ya wateule walioamua kutumia kisingizio cha “maagizo kutoka juu” katika utendaji kazi wao.

Alisema: “Na mara nyingi maagizo yanakuwa hayapo, bali ni utekelezaji wa wajibu wa sheria, wajiamini na wasiwaonee watu lakini watimize wajibu wao.”

Maneno haya ya mkuu wa nchi ndani yake yamebeba ujumbe mzito. Mosi, kinachoanza kuonekana hapa ni ukosefu wa semina elekezi kwa wateule, kiasi cha kutunga maneno yasiyo ya kweli pale wanapotekeleza wajibu wao, ama wa haki, au wa uonevu.

Pili, kuna kutojiamini kwa baadhi ya wateule hao, ndiyo maana anawataka wajiamini, watekeleze wajibu wao kwa mujibu wa sheria bila kuonea mtu.

Tatu, na pengine muhimu zaidi kwenye maneno ya Ndugu Rais, ni angalizo lake la kuwataka viongozi watekeleze wajibu wao bila “kuonea mtu”. Hapo ndipo kwenye mambo.

Ni ukweli ulio wazi kuwa hii sentensi ya “maagizo kutoka juu” imetumiwa mno na viongozi wa umma, wanasiasa na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwanyanyasa na kuwaonea watu wengi.

Tumesikia visa vingi vya watu kunyimwa dhamana kwa kisingizio cha maagizo kutoka juu. Mtu anaweza kuwekwa rumande kwa tuhuma nyepesi kabisa, lakini akateswa rumande kwa wiki au zaidi. Ndugu na jamaa wanapofuatilia majibu wanayopewa ni kwamba kuwekwa kwake ndani mtuhumiwa ni “maagizo kutoka juu.”

Hili la “maagizo kutoka juu” linawatesa watu wengi sana. Tutalimalizaje? Bahati mbaya, kwa mfano, mkuu wa mkoa anaweza kumweka mtu rumande kwa sababu ya chuki binafsi au kwa hoja mufilisi, na anaweza kujenga mazingira ya kuwatisha viongozi wote wa vyombo vya ulinzi na usalama katika mkoa wake kwa kuwaambia “haya ni maagizo kutoka juu.”

Bahati mbaya uongo huu unapoenezwa na mtu kama mkuu wa mkoa, hakuna RPC, Kamanda wa Takukuru wa Mkoa, Mkuu wa Uhamiaji wa Mkoa au Ofisa Usalama wa Mkoa anayeweza kupiga simu huko “juu” kuuliza kwa lengo la kupata ukweli.

Tumewaona wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama ngazi za wilaya na mikoa wakipata shida mno kuwaweka watu rumande kwa kigezo hiki hiki cha “maagizo kutoka juu.”

Hii ni njia rahisi ya wanasiasa na watumishi wengine wa umma kuwaonea watu kwa sababu wanajua OCD au RPC hawezi kumpigia simu waziri, waziri mkuu au rais kumuuliza kama kweli ametoa maagizo ya kumweka mtu fulani rumande. Matokeo yake watu wengi wameendelea kuumizwa kwa ubabe wa viongozi, hasa wanasiasa.

Inapotokea kiongozi amechukizana na mtu, njia anayoitumia ni hiyo ya “maagizo kutoka juu.”

Tufanye nini? Kwa kuwa si rahisi kwa mkuu wa kituo cha polisi, au ofisa usalama wa wilaya au mkoa na kadhalika; kuwasiliana na viongozi wa ngazi za juu serikalini, basi uwepo utaratibu wa kuwawezesha ndugu au jamaa wa watu wanaoteswa kwa staili hii kuuliza na kupata majibu kutoka huko “juu”.

Kwa mfano, kunaweza kuwepo namba ya simu kwa idara za usalama kupokea maswali au malalamiko ya aina hii. Mtu anaweza kuandika kueleza namna ndugu au mtu fulani anavyoteswa kwa sababu tu eti kuna maagizo kutoka juu.

Hilo linawezekana, lakini jingine muhimu ni kwa wananchi wenyewe kuwa na jeuri ya kutambua haki na wajibu wao na kuhoji mambo, maana wao hawahitaji kutumia itifaki kama ya watumishi wa umma.

Watambue kuwa mtu anayekabiliwa na kosa la aina fulani anapaswa kuwekwa rumande muda gani kabla ya kufikishwa mahakamani. Ikitokea, kwa mfano, mtu anayetuhumiwa kuiba kuku akawekwa rumande kwa wiki nzima kwa kigezo cha “maagizo kutoka juu”, mwananchi atambue kuwa hakuna kiongozi wa kweli anayeweza kutoa amri ya aina hiyo, maana sheria haimpi nguvu hizo. Wananchi wakijenga tabia ya kuhoji na kutokata tamaa, huu msamiati wa “maagizo kutoka juu” utasalia vitabuni tu.

Katika kukoleza suala hili, naomba nimnukuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika. Akizungumza bungeni siku chache zilizopita, alisema: “Mkuu wa mkoa saa zake ni 48, anaweza akamweka saa 24 akipenda, lakini ninachotaka kusema si lazima wewe umweke mtu ndani, kama ni criminal offence (kosa la jinai) OCD yuko. Kama ni suala la uhamiaji, ofisa uhamiaji yuko. Kama amekwepa kodi mtu wa TRA yuko; si lazima utamke wewe. Haya mambo lazima utamke wewe [?] Tuache ‘kujimwambafai’, yaani wewe uonekane mwamba. Nawaomba huko mliko msiniharibie kazi yangu, mimi ndiye mwenye title ya utawala bora. Mimi ndiye waziri mwenye nafasi ya utawala bora. Ukiendesha mambo kinyume na utawala bora unaniharibia mimi kazi.”

Maneno ya busara sana. Bunge letu halionyeshwi ‘live’, kwa hiyo inawezekana haya maneno yakawa yamewapita kando walengwa.

Maneno ya Komredi Mkuchika ukiyatafakari unaona yanarejea kule kule kwenye ukosefu wa semina elekezi kwa baadhi ya viongozi wa umma.

Kwa kweli kinachofanywa na baadhi ya watawala ni kutaka kuonyesha mabavu yao ya uongozi. Busara inatumika kidogo mno. Wapo watawala [si viongozi] ambao kwa kukosa maadili ya uongozi wanadhani kila kitu ni lazima maguvu yatumike.

Kama alivyosema Komredi Mkuchika, mtu anadaiwa kodi, kuna sababu gani ya DC au RC kuagiza polisi wamkamate, wamweke rumande? Na je, hao wanaotoa madai dhidi ya wengine mara zote wamekuwa sahihi?

Kuna tatizo la uhamiaji, kwanini DC au RC asiagize mamlaka husika ziwahoji watuhumiwa? Hii weka ndani, weka ndani ina nini zaidi ya kilichosemwa na waziri kuwa ni ‘kujimwambafai?’

Kwenye sheria tunaambiwa kuna kitu kinaitwa ‘natural justice’. Hii ni ile hali ya kumpa mtuhumiwa au upande wa pili haki ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa. DC, RC au waziri anapojazwa mambo ya kuambiwa, kwanini asitumie busara ya yeye au vyombo husika kukutana na upande unaotuhumiwa ili kupata ukweli?

Ukifuatilia sana hawa wanaofanya haya mambo ni wale wanaopenda sana msemo wa “maagizo kutoka juu” alimradi tu kuwaonea watu wasiokuwa na hatia.

Ahadi ya 5 ya Mwana TANU ambayo baadaye ilirithiwa na CCM ilisema: “Cheo ni dhamana, sitakitumia cheo changu au cha mtu mwingine kwa faida yangu.” Haya ni maneno ya maana sana. Kwa mambo yanayofanywa na baadhi ya viongozi wetu, ni wazi kabisa kuwa ahadi hii hawajawahi kuisoma.

Cheo ni dhamana. Ndiyo maana alikuwapo rais wa awamu ya kwanza, leo yupo wa awamu ya tano. Ndiyo maana huyu ambaye sasa ni mkuu wa mkoa kabla yake walishakuwapo watangulizi wake. Hali ni kama hiyo kwa wakuu wa wilaya na viongozi wengine wote.

Kitu pekee kinachoweza kumpa mtu maisha ya heri na fanaka baada ya kustaafu ni kutenda haki tu. Kutenda haki hakuna maana watu wasihukumiwe kadiri ya makosa yao, la hasha! Mtu anayehukumiwa kwa haki kamwe hawezi kuwa na dua mbaya kwa aliyemhukumu. Anayeadhibiwa kwa wizi au kwa kuua, ni mara chache atakuwa na hasira dhidi ya yule aliyemhukumu.

Lakini hawa wanaodhani kwa kuwa DC, RC au waziri basi wana haki ya kuwaonea watu wasio na hatia, ole wao. Wajifunze kwa baadhi ya waliowatangulia. Wapo mitaani wakiwa hawana hata wa kunywa nao kahawa. Haki ndiyo shina linaloshikilia maisha ya furaha baada ya kutoka madarakani.

Kwa kuyatazama haya na mengine ambayo sikuyaainisha hapa, tunaona kabisa umuhimu wa kuwa na semina elekezi, pia kuwapa mafunzo viongozi wetu ili wawe watenda haki kwa mujibu wa katiba, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali.

469 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!