Malkia wa Tembo amefungwa jela miaka 15. Hii ni habari njema kwa wahifadhi. Sijasikia wanaobeza hukumu hiyo, japo wapo wanaoona ni ndogo ikilinganishwa na tembo 430 waliotoweka kutokana na mwongozo wake.

Kwenye kesi hii waliofungwa ni wawili. Huu ni “utani”. Haiwezekani tembo 430 wauawe na watu wawili tu. Hatujaambiwa madereva, walenga shabaha, wapagazi, wasafirishaji na wengine wote kwenye mtandao huu wako wapi. Haiwezekani Malkia wa Tembo akawa ndiye aliyefanya kazi zote hizo. Haiwezekani. Ujangili ni mtandao. Unawahusisha watu wengi – kuanzia kwa watu wa kawaida kabisa hadi kwa mabilionea. Ujangili ni kama mti unaochipuka. Mzizi, tawi – kimoja kati ya hivyo kina uwezo wa kuchipuka.

Kufungwa jela kwa Malkia wa Tembo si mwisho wa ujangili. Kama tunadhani ujangili utapungua, basi ni wa tembo lakini ujangili wa wanyamapori wengine, rasilimali misitu na rasilimali zilizo ndani ya maji ungali juu.

Wiki mbili zilizopita katika eneo la Loovilukuny wilayani Ngorongoro, majangili waliua wanyamapori 83, wengi wao wakiwa pundamilia. Hii ni habari mbaya kabisa kwenye uhifadhi.

Kando ya Hifadhi ya Serengeti katika mikoa ya Mara na Simiyu mamia ya wanyamapori wanauawa kila wiki. Ujangili wa kitoweo na biashara japo tunadhani si hatari kama ulivyo ujangili wa tembo au faru, bado ni tishio kubwa kwa uhifadhi na uendelevu wa rasilimali hii.

Tunavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimama imara kulinda rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya taifa letu.

Ulinzi wa wanyamapori ni jambo muhimu kutokana na ukweli kwamba utalii ndiyo uliobaki kuwa chanzo cha uhakika cha mapato ya fedha za kigeni.

Kufungwa kwa Malkia wa Tembo kuwe chachu ya kuendeleza mapambano haya. Tunatambua ukweli kuwa ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama wako wachache wanaoshiriki dhambi hii. Hao hatuna budi kuwabaini na kuhakikisha wanawekwa kando ili kunusuru wanyamapori.

Vita hii haitazaa matunda mazuri endapo ushirikishwaji wa wananchi kwenye ulinzi wa rasilimali hii utakuwa wa kusuasua. Wananchi washirikishwe kwa kupewa elimu ya uhifadhi kwa lengo la wao kutambua faida zake.

Lakini si hivyo tu, bali faida zinazotokana na uhifadhi sharti zionekane moja kwa moja kwa wananchi wanaozunguka maeneo yote ya hifadhi.

Wananchi wakipata huduma za elimu, afya, maji safi na salama, umeme na huduma nyingine muhimu kwa maisha yao ya kila siku, ni wazi kwamba watakuwa wasimamizi wazuri wa rasilimali hizi.

Endapo wataachwa au wataonjeshwa tu faida za uhifadhi, dhima hii ya kulinda utajiri huu itakuwa ngumu. Serikali pekee haiwezi kushinda vita ya ujangili.

Sambamba na hili, vyombo vya uhifadhi viwe tayari kuwatuza wananchi wema wanaoshiriki kutoa taarifa zinazofanikisha kuzima au kuwakamata majangili. Wapo wananchi wema wengi walio tayari kutoa taarifa za kufanikisha mapambano haya, lakini mara kadhaa wamevunjwa moyo kwa kutopata ‘asante’ kutoka kwa mamlaka zinazohusika.

Pia ni katikati kundi hilo hilo ambamo watu wenye mapenzi mema wametoa taarifa za majangili na kujikuta wamejulikana kwa wabaya. Hali hiyo imewafanya baadhi yao wakimbie makazi au waishi kwa hofu kubwa.

Utunzaji siri za watu wanaosaidia kukamatwa kwa majangili uwe sehemu ya kiapo cha viongozi na watendaji wanaojihusisha na ulinzi wa rasilimali za nchi.

Mwisho, nawapongeza wasimamizi wa vyombo vya utoaji haki nchini kwa kusimama imara kuhakikisha kuwa malkia huyu wa ujangili anapatikana na anatendewa haki kulingana na matendo yake.

Wote walioshiriki kwenye kesi hizi na kutoa adhabu zenye mwelekeo wa uzalendo hatuna budi kuwapongeza na kuwahimiza kuendelea na moyo huo kwa ajili ya manufaa ya leo na kwa kizazi kijacho.

Ulinzi wa rasilimali hizi ni dhima yetu sote. Kila mzazi na mlezi ajione ana haki na wajibu wa kuielimisha jamii pale alipo ili hatimaye tuwe na kizazi kilicho tayari kulinda kwa nguvu zote utajiri huu.

Kufungwa kwa Malkia wa Tembo hakuna maana kuwa sasa wanyama wetu wako salama. Kifungo hiki ni kengele tu ya kutukumbusha wajibu mkubwa tulionao sisi sote katika kuwalinda wanyamapori wetu.

Please follow and like us:
Pin Share