Kwa nini kigugumizi Ngorongoro, Loliondo?

Hivi karibuni kumezinduliwa sinema ya Tanzania Royal Tour. Ni sinema nzuri ingawa dosari kubwa niliyoiona ni kukosekana kwa vivutio vya utalii vingi zaidi.

Mathalani, ni dosari kubwa ya kiufundi kwenye sinema hiyo kutoonyesha nyumbu wanavyosafiri au wakati wakiwa wamejaa na kustaajabisha katika maeneo kama ya Ndutu, Nabi, Seronera na kadhalika.

Shaka yetu ni kwamba endapo majirani zetu wataandaa ‘royal tour’ yao, watajimilikisha kivutio hicho cha utalii. Lakini pia hatuwezi kusema Oldupai ndipo mahali ‘panapodaiwa’ kuwa chimbuko la binadamu. Alimradi hadi leo hakujatangazwa mahali pengine penye sifa ya upendeleo kama hiyo, tuseme wazi na kwa kujidai kwamba Oldupai ndipo kwenye chimbuko la binadamu wote wa ulimwengu huu. Utafiti wa kisayansi wa vinasaba umethibitisha hilo pasi na shaka.

Ukiacha dosari hizo na nyingine ya kutokuwapo vivutio kama vile vya mchanga unaosafiri, Oldonyo Lengai, jabali la Nasera, kreta ya Empakai, Kitulo, na kadhalika; bado sinema hii itabaki kuwa chachu ya kuwavuta watalii wengi zaidi ili ikiwezekana mwaka 2025 idadi yao ifike milioni tano.

Rais Samia Suluhu Hassan ana nia njema na utalii. Anatambua wazi kwamba nia hiyo njema inabebwa na kitu muhimu sana –uhifadhi wa mazingira. Tofauti na nchi kama Misri ambayo utalii wake unatokana na mambo yaliyofanywa na wanadamu (mapiramidi, miili ya mafarao), utalii wetu kwa sehemu kubwa unatokana na kazi ya Mungu. Watalii wanaokuja Tanzania wanakuja kuhushuhudia uumbaji wa Mungu. Ndiyo maana Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuhimiza uhifadhi katika maeneo kama Ngorongoro na Loliondo.

Mara zote wahifadhi wameeleza na Rais Samia amewaelewa kwamba huwezi kuwa na Ngorongoro yenye kuwavutia watalii endapo kasi ya shughuli za kibinadamu na ongezeko la watu na mifugo vitaendelea kwa kasi hii hii tunayoishuhidia sasa. Ile modeli ya kuwa na wanadamu, mifugo na wanyamapori pamoja imefeli, na kwa maana hiyo sharti jawabu lipatikane mapema ili kunusuru hazina hii ya uchumi wa nchi yetu.

Tunapongeza juhudi zilizokwisha kutangazwa na serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, za kuwahamisha kwa hiari baadhi ya wakazi wa Ngorongoro na mifugo yao na kwenda kuishi popote ndani ya Tanzania.

Sambamba na Ngorongoro, Rais Samia, ameelezwa na kutambua kuwa bila uwepo wa Pori Tengefu la Loliondo, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti itatoweka, maana hilo pori ndilo chanzo cha maji yanayoingia humo hifadhini kwa asilimia takriban 50. Loliondo ndilo eneo la mazalia ya nyumbu na wanyamapori wengine. Loliondo ndipo kwenye ushoroba wa nyumbu unaokamilisha mzunguko wa Serengeti-Maasai Mara.

Kwa kutambua umuhimu huo, serikali imetangaza mpango wa kubaki na kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi, na kilomita nyingine 2,500 waachiwe wananchi wazitumie kadiri ya mipango watakayojiwekea. Licha ya kuwapo nia hiyo njema, kumeibuka ukinzani mkubwa kiasi cha kulifanya eneo hilo kuonekana kama ni jamhuri ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na nia nzuri ya serikali, bado kasi ya kuyaokoa maeneo haya si ile iliyotarajiwa na wahifadhi. Kwa suala la Ngorongoro kunaweza kuwapo hoja ya kwamba bado kuna makazi yanaandaliwa Handeni na kwingineko ili wananchi wanaohama wafikie huko. Hiyo ni kazi inayohitaji muda na fedha. Lakini suala la Loliondo ambalo gharama yake kubwa ni ya kuweka vigingi sidhani kama lilipaswa kuwa la kusuasua muda wote huu.

Mambo yenye manufaa mapana kwa umma yana gharama zake. Miongoni mwa gharama hizo ni malalamiko ya wananchi wanaoguswa. Lakini serikali ambayo ni wajibu wake kujenga ustawi wa sasa na wa miaka ijayo haiwezi kuogopa au kukwepa gharama pindi inapokabiliana na hali kama hii ya sasa.

Wananchi wanaweza kulalamika, lakini baadaye wakawa ndio wanufaika wakuu wa hicho kinachofanywa sasa. Isitoshe, ni wajibu wa serikali na wadau wengine kuulinda urithi huu adhimu ili vizazi vya miaka mamia kwa mamia ijayo vinufaike. Hatuwezi kuwa wabinafsi kwa kusimamia uharibifu wa rasimali hii muhimu. Mataifa ya Ulaya na Marekani yalikuwa na wanyamapori wengi kama tulivyo sisi leo. Walikuwa na hizo ‘Serengeti-Maasai Mara’ nyingi.

Kulikuwa na misafara (shoroba) kubwa na ndefu kati ya Amerika Kusini na Amerika Kaskazini, lakini walifanya uzembe mkubwa na hatimaye utajiri huo ukatoweka. Serengeti-Maasai Mara ndio msafara pekee mkubwa uliosalia katika sayari hii na ndiyo maana hao vijukuu vya wachafuzi wa mazingira walioua uhondo huo vinakuja kushuhudia kile kilichotoweka kwao. Tusifanye makosa yaliyofanywa na wenzetu.

Rais Samia anapotumia akili na nguvu kuvutia watalii wengi zaidi ili taifa linufaike, jeuri yake inajengwa juu ya uwepo wa wanyamapori na misitu. Anatambua kuwa bila hao wanyamapori, ujio wa watalii utakuwa shakani. Anajua mito ikikauka, misitu na nyasi vitatoweka na kwa maana hiyo viumbe hai – wanyamapori, ndege, samaki na kadhalika vitatoweka. Hakuna mtalii atakuja kuwashangaa ng’ombe, kondoo au mbuzi.

Kama hivyo ndivyo, serikali ichukue hatua za haraka kunusuru hali hii. Kasi ya kuandikisha wananchi wa Ngorongoro walio tayari kuhama iongezwe. Uwekaji vigingi Loliondo ufanywe sasa ili kunusuru eneo hilo na wakati huo huo kuwavutia wageni walete manufaa kwa nchi.

Endapo serikali inafeli kutekeleza uamuzi wake, basi wajue hii itakuwa ‘case study’ itakayotumiwa na Watanzania wengine kugomea mambo ya msingi na yenye manufaa kwa wananchi na nchi yenyewe kwa jumla. Wale wanaopinga mpango huu halali wanatamba kwenye mitandao kwamba wamepata watetezi wao serikalini kwa hiyo hakuna kitakachotokea. Inawezekana haya yakawa maneno ya kutiana faraja, lakini ukitafakari ulegelege wa utekelezaji wa uamuzi unaweza kuamini kinachosemwa na hao hao. Serikali isiweke mwanya wa kudhihakiwa kiasi hicho.