Mabilionea wa kimataifa wafaidika na vita 

Na Nizar K Visram

Vyombo vya habari vimechangamka kutupatia habari za vita ya Ukraine. Hata hivyo, ni nadra kwao kutueleza jinsi matajiri wa kimataifa wanavyotajirika zaidi kutokana na vita hii. Jinsi kampuni zinazotengeneza na kuuza silaha zinavyofurahia na kuishangilia vita hii.

NATO ikiongozwa na Marekani tayari imetuma Ukraine makombora 17,000 ya kushambulia vifaru na makombora 2,000 aina ya Stmger kwa kushambulia ndege za kivita. 

Nchi nyingine zinazotuma silaha ni Uingereza, Australia, Canada na Uturuki. Na Ujerumani nayo imeipa Ukraine makombora 1,000 ya kupiga vifaru na makombora 500 ya Stinger. 

Umoja wa Ulaya (EU) umeahidi kutoa silaha za dola milioni 459. Israel nayo imo. Gazeti la Haaretz limetoa mfano wa Kampuni ya silaha ya Elbit Systems nchini humo ambayo bei ya hisa yake imepanda kwa asilimia 18 katika siku mbili tu. Hii inatokana na vita.

Majeshi ya Marekani yanatumia dola bilioni 768 kila mwaka, na hii ni asilimia 10 ya bajeti ya serikali. Hakuna serikali duniani inayotumia kiasi hiki cha fedha katika majeshi yake. Pia inauza nje silaha za mabilioni ya dola. Papa Francis alipohutubia Bunge la Marekani alisema: “Tunapaswa kuzuia ushindani huu wa silaha duniani, kwa sababu fedha mnazopata zimeloa damu inayomwagika vitani, ni damu ya watu wasio na hatia.”

Maneno ya Papa hayakuwagusa wabunge kwani tayari Rais Biden amelitaka Bunge (Congress) kuidhinisha silaha za dola bilioni 6.4 kwa ajili ya Ukraine. Kabla ya hata vita kuanza, mwaka jana, zaidi ya dola bilioni moja zilitumika kutuma silaha Ukraine. Ni silaha zilizotengenezwa hasa na  kampuni za Lockheed Martin na Raytheon.

Licha ya silaha zilizokwisha kutumwa, Mei 8, mwaka huu Rais Biden alisaini bajeti ya dola bilioni 33 kwa ajili ya misaada ya kijeshi kwa Ukraine. Nao wabunge wamependekeza kuongeza dola bilioni saba. 

Yote haya maana yake ni kutengeneza faida kwa kampuni za silaha. Na silaha zinazotumwa Ukraine zaidi ni makombora aina ya Stinger yanayotengenezwa na Raytheon. Wakishirikiana na Lockheed Martin wanatengeneza Javelin. Kampuni nyingine ni Boeing, General Dynamics na Northrop Grumman. Hawa ndio wanaochota mabilioni ya fedha kutokana na mikataba inayotolewa na makao makuu ya jeshi la Marekani (Pentagon).

Kila mwaka Pentagon inawapa mikataba ya dola bilioni 150. Mwaka jana tu Lockheed Martin walichota dola bilioni 75. Hii ni zaidi ya bajeti nzima ya Wizara ya Mambo ya Nje. Sasa kampuni hizo zitafaidika zaidi kutokana na vita ya Ukraine. 

Hata kabla ya vita kuanza, wakuu wa kampuni hizi walikuwa wakizungumza jinsi watakavyotajirika zaidi. Januari mwaka huu mkuu wa Raytheon Technologies, Gregory Hayes aliwaambia wanahisa wa kampuni yake kuwa migogoro ya Ulaya Mashariki, Bahari ya China na kwingineko ni fursa nzuri ya kuuza silaha. 

Na Machi, Hayes aliliambia jarida la Harvard Business Review kuwa vita ya Ukraine itainufaisha kampuni yake kwa muda mrefu.

Tangu vita kuanza, bei ya hisa ya Lockheed imepanda kwa asilimia 16 na Raytheon asilimia 3. Northrop Grumman nayo imefaidika. Na nchini Uingereza Kampuni ya BAE hisa zake zimepanda kwa asilimia 26.

Fursa nyingine kwa kampuni hizi inatokana na vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Urusi.  Matokeo ya vikwazo ni kuwa kampuni za Urusi zitapata shida katika kununua bidhaa ghafi kwa ajili ya utengenezaji wa silaha. Na kwa vile Urusi ni muuzaji mkubwa wa silaha duniani, itawawia vigumu kuuza kutokana na ukosefu wa vipuli na ukosefu wa soko. Maana yake kampuni za silaha za Marekani na Ulaya zitanyakua soko la Urusi.

Hata hivyo, haitakuwa rahisi kwa kampuni za Magharibi kulinyakua soko la Urusi kwa sababu, kama ilivyosema ripoti ya Bunge la Marekani, silaha za Urusi zina bei nafuu na pia ni rahisi kuzitumia na kuzitunza tofauti na silaha za Magharibi. 

Kampuni ya silaha inayoongoza nchini Urusi ni Almaz-Antey ambayo inauza silaha za dola bilioni 6.6, ikifuatiwa na  United Aircraft Corp (bilioni 4.6)  na United Shipbuilding Corp (bilioni 4.5). Urusi imekuwa ikipanua viwanda vyake vya silaha tangu mwaka 2014 walipowekewa vikwazo na nchi za Magharibi. Ndipo walipoanza sera ya kujitegemea kwa kuunda vitu vyao badala ya kutegemea nje. 

Mara nyingi tunafikiri kuwa vikwazo vimeanzishwa hivi majuzi na Rais Biden. Ukweli ni kuwa hata kabla ya vita Uingereza ilijitoa kutoka ubia wake na Urusi katika kuunda silaha za takriban dola bilioni 4.5.

Baada ya Marekani nchi ya pili katika kuuza silaha duniani ilikuwa Urusi. Kati ya 2016 na 2020 biashara ya Urusi ikaanguka kwa asilimia 22. Pigo kubwa ni pale India ilipopunguza kununua silaha kutoka Urusi, ingawa iliongeza mauzo yake China, Algeria na Misri.

Kwa hiyo, kampuni za silaha Marekani zimefaidika kutokana na soko jipya na kubwa la Ukraine, pia kutokana na vikwazo dhidi ya Urusi. Ni kisu chenye makali pande mbili.

Ukiachia hizo kampuni za silaha kuna vigogo wanaojaza mifuko yao kutokana na vita ya Ukraine, nao ni wabunge wa Marekani. Kwa mujibu wa gazeti liitwalo Business Insider wabunge hao wasiopungua 19 wamewekeza katika kampuni za silaha. 

Kati yao kuna waliowekeza hivi majuzi tu walipohisi Urusi huenda ikaishambulia Ukraine. 

Kwa mfano, Mbunge wa Chama cha Republican, Marjorie Taylor Greene, alinunua hisa za dola hadi 5,000 katika Kampuni ya Lockheed Martin. Alifanya hivyo Februari 22, yaani siku mbili tu kabla ya mashambulizi. Baada ya siku mbili akaandika katika ukurasa wake wa Twitter: “Vita ni biashara kubwa kwa viongozi.”

Wengine walijitosa katika biashara hii ya vita ni Diana Harshbarger (Republican) na mumewe ambao wamenunua hisa za Raytheon zaidi ya dola 15,000 na Lois Frankel (Democratic) aliyenunua hisa za Lockheed Martin.

 Wakati huohuo kuna ujanja unaotumiwa na vyombo vya habari kama CNN. Watawaalika wale wanaojiita ‘wataalamu’ wa kivita ili kuwaelimisha watazamaji wao.

Kwa mfano CNN ilimwita Leon Paanetta mara nne. Huyu alikuwa waziri wa majeshi wa Marekani. Akampongeza Biden kwa kuongeza silaha huko Ukraine na kusema vita lazima iendelee.

Lakini CNN haikuwaambia watazamaji kuwa Panetta kwa hivi sasa ni mshauri mkuu wa Beacon Global Strategies, kampuni inayoishauri Raytheon inayounda silaha.

Na shirika la utangazaji la MSNBC likamualika Jeh Johnson, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani. Watazamaji hawakuambiwa kuwa yeye kwa sasa yumo katika bodi ya Lockheed Martin. Alipoulizwa kuhusu kazi yake hiyo alijibu: “Sina la kusema.” 

Jeremy Bash alikuwa mnadhimu mkuu wa Pentagon na CIA chini ya rais Obama. Mara kwa mara huwa anaalikwa na MSNBC na NBC ili kutoa uchambuzi wa vita ya Ukraine. Naye akamsifu Biden kwa kutuma silaha Ukraine. 

Watazamaji hawaambiwi kuwa kwa sasa Bash ni mkurugenzi mkuu na mwanzilishi wa  Kampuni ya Beacon Global Strategies inayoshirikiana na Raytheon!

Kuna Admiral (mstaafu) James Stavridis ambaye ni mshauri wa Beacon Global Strategies. Yeye pia amekuwa akialikwa katika runinga ya MSNBC. Pia ni naibu mwenyekiti wa Kampuni ya Carlyle Group ambayo imewekeza katika kampuni za silaha kama Raytheon. Naye akahubiri vita iendelee lakini watazamaji hawakuambiwa kazi yake ya sasa.

Jenerali (mstaafu) Barry McCaffrey naye hualikwa na MSNBC, naye huisifu NATO inavyopigana vita. Huyu ndiye aliyewaamrisha askari wake kuwapiga mabomu na kuwaua raia na watoto wa Iraq hata baada ya vita kusimamishwa. Sasa anamiliki Kampuni ya ushauri ya  BR McCaffrey Associates LLC. Kazi yake ni kushirikisha sekta binafsi na serikali ili kuzipatia mikataba kampuni za kuunda silaha.

Mkurugenzi mstaafu wa CIA na jenerali mstaafu wa majeshi, David Petraeus, amekuwa akizungumza katika CNN akitaka silaha zaidi zipelekwe Ukraine. Wasichokisema ni kuwa Petraeus ni mbia katika kampuni kubwa ya KKR inayoshughulikia biashara ya silaha na zana za kivita. 

Jenerali mstaafu Wesley Clark pia huonekana katika CNN akizungumzia vita. Asichokisema ni kuwa yeye anazishauri kampuni za silaha kupitia Kampuni yake ya Wesley K. Clark & Associates.

Michèle Flournoy, naibu waziri mstaafu wa majeshi aliyefanya kazi chini ya Obama ameonekana mara kadha katika CNN akihubiri vita zaidi huko Ukraine. 

Hakusema kuwa hivi sasa yeye ni mbia anayeendesha Kampuni ya WestExec Advisors ambayo inazishauri kampuni za silaha kama Boeing. Pia yumo katika bodi ya Booz Allen Hamilton ambayo ni makandarasi wa silaha.

[email protected]

+1 343 2048996