Tenga ajiandaa kuleta mageuzi katika soka

Aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Chilla Tenga, amesema jukumu lake la kwanza katika majukumu yake mapya katika kamati ya usimamizi wa leseni za klabu za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ni kuhakikisha ustawi wa klabu na timu za taifa.
Akizungumza na JAMHURI mara baada ya kupata nafasi hiyo, amesema soka katika bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto nyingi kiasi cha kuhitaji ushirikiano wa pamoja miongoni mwa wadau  wote.
“Moja ya majukumu yangu kama kiongozi ni kuhakikisha nahamasisha uwepo wa timu za vijana, kila klabu kuwa na viwanja vya mazoezi na vya kuchezea mpira, na hilo ninatarajia kuanza nalo mara moja,” amesema Tenga.
Amesema mabadiliko yaliyopatikana ndani ya taasisi za soka duniani kuanzia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) hadi Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ni kielelezo kuwa mabadiliko ndani ya mchezo huu hayawezi kuepukika, kwa hiyo tunapaswa kubadilika ili kuendana na mawazo na fikra hizi mpya.
“Nitatumia ujuzi na uzoefu nilionao katika ya mchezo huu, kuhakikisha tunatoka hapa tulipo na kuanza safari ya kuelekea waliko wenzetu waliotutangulia – hasa wenzetu wa Afrika Magharibi na Ulaya kwa ujumla,” amesema Tenga.
Amesema changamoto kubwa anayotarajia kukumbana nayo katika kipindi kijacho cha uongozi wake, ni pamoja na umasikini ndani ya klabu, klabu nyingi kukosa viwanja vya kuchezea na mazoezi pamoja na ukosefu wa timu za watoto.
Amesema bila kuwa na mipango ya muda mrefu na mifupi ya kuwekeza katika timu za vijana, michezo yote bado itakuwa ni kazi bure pamoja na ongezeko la timu za kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia bila mipango.
Kwa upande wake, Mjumbe wa kudumu wa CAF, Said El Maamry, amesema katika kipindi hiki ambapo kumekuwa na mabadiliko makubwa ya uongozi FIFA, Rais wake mpya, Gianni Infantino, Watanzania wapenzi wa soka na bara zima la Afrika hawana budi kuwa na matumaini ya kuanza kupata maendeleo katika soka.
Akizungumza kuhusu nafasi mpya ya Tenga, El Maamry ameliambia JAMHURI kuwa Tenga ni mtu mwenye maono ya mbali linapokuja suala la mchezo wa soka, matumaini ya wengi kuwa atautumia ujuzi wake kuhakikisha ustawi wa mchezo wa soka la bara la Afrika.
“Wote tulikuwa ni mashuhuda, ni katika kipindi cha uongozi wa Tenga ndani ya TFF  ndipo tulipoanza kukubalika na hata mipango mingi ya muda mrefu tunayoiona leo ni ile iliyoasisiwa na Tenga, kwa hiyo kikubwa ni kumpa ushirikiano,” amesema El Maamry.
Amesema ni wakati mwafaka kwa klabu hadi timu za taifa kuanza kuwekeza katika mipango ya soka la vijana, huku akisisitiza hilo litawezekana kama wanaoongoza soka watakuwa na nia ya kufika huko.
El Maamry amesema nchi haiwezi kupata maendeleo katika mchezo wowote endapo hakutakuwa na mipango endelevu katika timu za vijana ambao ndiyo wanaoweza kuwa wawakilishi katika mashindano mbalimbali.
Hivi karibuni katika kufanya mabadiliko, FIFA imeongeza idadi za timu zitakazoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
FIFA pia imeongeza idadi ya timu kutoka katika bara la Ulaya kutoka 13 za sasa hadi 16, huku Amerika Kaskazini na Kusini zikiwa timu sita kutoka tatu za awali.
Oceania nao wamepewa nafasi moja ya uwakilishi wa moja kwa moja wakati hapo mwanzo iliwapasa wacheze mchezo wa mtoano na timu za Amerika Kusini, ili kufuzu kupata uwakilishi katika fainali za Kombe la Dunia.
Hii itawafanya New Zealand kuwa na nafasi kubwa ya kushiriki Kombe la Dunia kila mara kutoka na kutokuwa na upinzani mkubwa hasa baada ya Australia kuanza kushiriki michuano ya bara la Asia.

854 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons