Kama kuna wakati nimepokea arafa nyingi za wasomaji wa barua yangu basi ni wiki jana, kila
mmoja na mawazo yake, wapo waliodiriki kusema ninaegemea upande fulani kwa maslahi
binafsi na wapo walionielewa na kupongeza juu ya waraka wangu ule wa wiki jana juu ya
maandamano, nirekebishe; jambo muhimu lililobeba lawama zote ni kwamba mimi sikupinga
maandamano bali nilizungumzia dhima na haki ya maandamano kama inafaa.
Nimeamua nianze kwa kuwaomba radhi walioshindwa kunielewa, na niombe radhi kwa
walionielewa lakini wakidhani kwamba nina itikadi ya watu Fulani, lakini niwapongeze
walionielewa hasa niliposema kuwa na mimi niliwahi kugoma kazi TAZARA miaka ile kwa lengo
la kuongezewa mishahara, lakini walionielewa nilizungumzia pia maandamano ya kupongeza
jitihada za wakati wetu kwa mambo yetu na watu wetu.
Sasa nadhani naweza nikasalimu na kuwatakia siku njema baada ya kutoa donge langu
lililonikwaza siku zote kupitia waraka ule ambao baadhi ya watu walikwazika na baadhi yao
walinielewa, leo ni siku nyingine ambayo nimeamua kuwaandikia waraka tofauti na ule ili
nisifanye makwazo zaidi.
Hata hivyo, waraka wangu wa leo umenikwaza mimi Zaidi, iwapo kutakuwa na mtu
atakayekwazika zaidi yangu, basi naomba aniwie radhi kwa kuwa sipendi kuishi na makwazo
kwa umri wangu, bora nitapike nitakuwa nimepunguza mzigo katika kifua changu.
Siku nyingi nimekuwa nikihudhuria shughuli za kijamii, hasa misiba na sherehe mbalimbali,
pamoja na mambo mengine jambo ambalo limekuwa ni tatizo kwangu ni pale ninaposhiriki
msiba wa mtumishi wa umma, au kiongozi wa jamii mwenye wadhifa wa chini kidogo.
Huwa nasikia taarifa nyingi za marehemu kabla ya kuzikwa, huwa najua wadhifa wa mtu kabla
ya kuzikwa, huwa najua umuhimu wa mtu kabla ya kuzikwa na hili ndilo huwa tatizo langu
kubwa kwa hao waandikaji wa hizo taarifa za marehemu, huwa nakereka kwa sababu pamoja
na taarifa zote nzuri anazotajwa nazo marehemu, lakini anazikwa kama mtu ambaye hakuwahi
kulitendea jambo lolote la maana Taifa hili.
Inanikera kwa kuwa huku kwetu vijijini ndiko walikotoka wanetu na kwenda kufanya kazi mjini
wakiwa na nguvu nyingi na kisha hupoteza maisha wakiwa wazee na kurudishwa kuzikwa huku
makwetu, safari yao ya mwisho huwa naamini inatakiwa iakisi uhalisia wa walichokiishi, lakini
ukweli ni kwamba naona kama kiini macho na huwa naona kama marehemu alikuwa mtu
mzururaji au tapeli huko alikofia.
Sina hakika kama waandikaji wa risala huwa wanachukua maneno ya watu wengine ama la,
huwa sielewi wanatumwa kuja kuumiza wafiwa ama nini lakini kitendo cha kusema pengo
kubwa la marehemu haliwezi kuzibika ilhali hata chakula cha msiba ni tatizo ndipo
ninapokwazika zaidi.
Haya maneno yanakera wanafamilia, tupo tunaojua uadilifu wa baadhi ya watumishi hao hadi
kifo kinapowaumbua kwa kufa masikini kwa kuitumikia jamii, tunajua baadhi ya familia ambazo
zimeshindwa kuhimili maisha baada ya wategemezi wao kuwakosa ndugu zao waliotangulia
mbele ya haki, huku wakiwa watumishi waadilifu makazini.
Inasikitisha zaidi unapoona familia inasahaulika pindi mtokapo makaburini na kuagwa kwa
mbwembwe nyingi na hao waitwao wawakilishi wa sehemu alipokuwa akifanya kazi, inaumiza
unapoona familia ikiteseka huku mtumishi huyo akiwa mbele ya haki na malipo yake huku
nyuma yakisuasua sanjari na hotuba nzuri yenye sifa kemkem juu ya utumishi wake uliotukuka.
Ninaumia sana ninapoona familia inadai malipo au fidia kwa miaka mingi hadi familia
inasambaratika kutokana na urasimu wa utekelezaji wa jambo katika ofisi yoyote aliyofanya

marehemu, hapo ndipo ninapokumbuka baadhi ya watumishi ambao huamua kumalizana moja
kwa moja na wahusika ama kwa kuiba au kufisidi mali ya umma.
Sijafanya utafiti lakini nadhani watu wote walioamua kuchukua chao mapema wamewahi kuona
matatizo haya kutoka katika familia ambazo zimetelekezwa, lakini nadhani pia kizazi kipya
ambacho kinaona yanayowatokea wazazi wao au ndugu zao wameamua kuacha uzalendo.
Ningependa kumbukizi ziakisi ukweli wa mtu – kama alikuwa mtumishi mwaminifu na pengo lake
haliwezi kuzibika basi na tuzikumbuke familia zao katika maisha yao, nakerwa sana na sifa hizi
ikiwa ni pamoja na kuzisahau familia zao.
Wasaalam,
Mzee Zuzu
Kipatimo

947 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!