Yah: Mwongozo wa Spika, lini serikali itahamia Dodoma?

Wanangu, leo ni siku nyingine ya Jumanne katika wiki hii ambayo ni nadra sana kuifikia, kama hujui kwamba kesho ni mtihani mkubwa kwako kutokana na siri kubwa aliyonayo Mwenyezi Mungu juu yako; ni yule ambaye si muumini wa dini yoyote ndiye anayeweza akawa kichaa asijue hilo. Nimefarijika mno na demokrasia inayoendelea hapa nchini kwa mambo ambayo kama si kigezo, yanaweza yakatutoa siku moja hapa tulipo na kutupeleka kule tutakako kwa nia njema na ya dhati kutoka kwa hao waitwao watawala wenye nia njema ya maendeleo.

Sisi tuliozaliwa zamani tuna matatizo mengi. Mosi, tuna mawazo ya zamani sana; pili hatutaki kubadilika kwenda na wakati wa dotcom – hili tunalijua lakini wakati mwingine tuna maana kubwa ya kutobadilika kutokana na kile tunachokiamini katika ukweli.

 

Tanzania ni nchi kubwa, mipaka tuliyowekewa na mkoloni ilikuwa kama tunu au zawadi kutoka kwao wakiongozwa na nguvu za Mwenyezi Mungu. Tunaamini hivyo kwa sababu wangeweza kuifanya Tanzania kuwa ndogo kama Rwanda au Burundi, lakini sababu ya msingi hasa ya kulifanya litanzania likawa hivi haijulikani.

 

Baada ya uhuru kuupokea tulikaa miaka kadhaa na tukafanya tafakari ya kizamani ambayo hadi leo huwa sielewi kama ilikuwa ya kijinga au la! Tuliiangalia Tanzania yetu na ukubwa wake na tukafikiria maendeleo katika ukubwa huo na ndipo tulipokuja na hoja nzito ya kupeleka maendeleo kwa wananchi kutokana na ile siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea. Ilikuwa ni katika kikao cha chama ambako tulikuwa tukiamini fikra za mwenyekiti wa chama wakati huo hata kama uamuzi huo ulikuwa ni wa wajumbe wengi, lakini kauli ya mwenyekiti ikitamkwa ndiyo iliyochukuliwa kuwa uamuzi wa busara na unaotakiwa kufuatwa na kila kiongozi na kila mwananchi.

 

Tuliamua kwa pamoja ndani ya vikao vyetu vya chama kwamba makao makuu yawe katikati ya nchi, lengo ni kuhakikisha tunasogeza huduma ya kijamii kwa watu wote bila kubagua kanda fulani au eneo fulani. Kwa pamoja na kwa kushirikiana na Mwenyekiti wetu Mwalimu Julius tukasema makao makuu ya nchi yawe Dodoma. Tukaanzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa lengo hilo na tukasema makao makuu ya chama na serikali yawe Dodoma ili kila mkoa uweze kufika na kupata huduma haraka, pasi na kuchelewa, lengo hasa tutumie muda mfupi na tuondokane na umasikini kwa kasi kubwa.

 

Tukaanza ujenzi mara moja tukashirikisha vijana wetu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makutopora, viongozi wa chama kila walipokutana hapo kwa ajili ya vikao walitafuta fursa ya kushiriki katika kazi za ujenzi wa makao makuu na wananchi walioko Dodoma nao kwa uzalendo ule ule wa kujitolea walifanya kazi. Kazi ilifanyika usiku na mchana, na nathubutu kutamka kuwa hata Nyerere alifyatua tofali siku kadhaa ili kujenga ofisi ya chama na serikali.

 

Kwa mawazo yetu ya kijinga kwamba makao makuu yawe Dodoma tukathubutu kujenga Ikulu kule Chamwino ili Rais wetu awe na makazi ya uhakika katikati ya nchi. Tukagawa viwanja kwa wizara, taasisi, idara, balozi na kurugenzi mbalimbali na hatimaye tukathubutu kutamka kuwa tukimaliza kazi hiyo, basi serikali na chama vitakuwa Dodoma ili mikoa mingine ipate faraja ya ukaribu.

 

Miaka ilipozidi kusogea na nguvu zetu kupungua kutokana na ugumu wa kazi ile ya kufyatua tofali na kuchora ramani za viwanja vya mawizara, taasisi na idara tukajikuta hatuna uwezo tena wa kuhoji utekelezaji katika kizazi cha dotcom. Makao makuu ya serikali yakaendelea kuwapo Dar es Salaam. Hakuna anayekumbusha suala la kuhamia Dodoma.

 

Shughuli za serikali na chama zikaendelea kufanyika Dodoma, lakini watumishi wote wakiwa ni wageni kutokea Dar es Salaam. Wakaendelea kulipana ma-posho makubwa makubwa kwa kisingizio cha Dodoma kuwa makao makuu ya nchi bila wao kuwapo hapo.

 

Wanangu, naaandika barua hii nikiwa katika taharuki kubwa ya kutaka kujua nini hasa kinachowasigeni kwenda Dodoma, ambako tulipanga kuwa makao makuu ya nchi kwa nia njema ya kusogeza huduma kwa wananchi. Mzee Zuzu hadi leo sielewi Dar es Salaam kuna nini hadi mshindwe kwenda Dodoma, sasa mji wenu umebanwa na kuleta hasara ya mabilioni ya shilingi kila mwezi, kutokana na ufinyu wa miundombinu na ofisi kuwa chache kutokana na kuanzishwa kwa ofisi nyingine mpya.

 

Wizara zimeongezeka na zinachipukia Dar es Salaam, hali kadhalika taasisi na idara za serikali zinaongezeka, watumishi wanaajiriwa upya Dar es Salaam, mji unazidi kujaa siku hadi siku, kisa wafanyakazi wa serikali hamtaki kuhamia Dodoma ambako tulipanga yawe makao makuu ya nchi  tulikochora ramani nzuri ambazo zisingeweza kuleta mtafaruku wa miundombinu.

 

Tuliipanga Dodoma vizuri. Tulianzia na Chamwino kwamba hapo angekaa mkuu wa nchi, lakini pia tuliyagawa maeneo mengi kwa ajili ya wizara na taasisi zake kama Nzuguni, Ihumwa, Mnadani, Mazengo, Airport, Area A, C, D; Hombolo, Chinangali West, Chimwaga, Mvumi, Mirembe na kadhalika. Maeneo haya hadi leo yapo na yana nafasi kubwa za ujenzi wa kile tulichokikusudia kama utekelezaji ambao sisi wazee tulipanga enzi za akili ya ujana wetu wa kijinga, kwamba huduma tuzisogeze kwa wananchi.

 

Tuliweza kupanga nafasi ya jengo la Bunge tukafanikiwa kujenga japo kwa kususua, lakini jengo la Msekwa likaisha na likahama kutoka Karimjee na kwenda Dodoma. Ile ndoto kwamba siku moja idadi ya wabunge itaongezeka kutoka 72 na kuwa zaidi ya 300 hatimaye ikatimia na matunda yake tunayaona. Wabunge wetu wapo pale na wanawawakilisha wananchi mbalimbali wa majimbo ya nchi hii kutoka kusini hadi kaskazini, mashariki hadi magharibi nao wanakubaliana na mawazo ya kizazi kipya kwamba serikali iendelee kubaki Dar es Salaam na si Dodoma tena kama tulivyokuwa tumepanga.

 

Mzee Zuzu huwa najiuliza maswali mengi sana, sina hakika kama sina wazee wenzangu ambao mnakumbuka ugumu wa kazi tuliyoifanya wakati huo na malengo mazuri tuliyokuwa tukitarajia. Nilitarajia kizazi kipya sasa kiamue kwa nguvu moja kwamba makao makuu si tu yahamie Dodoma, bali yawepo Dodoma mara moja. Wenzetu walioiga mpango wetu kama Waganda waliweza kutenga Kampala kuwa mji wa biashara kama ambavyo sisi tulikusudia iwe hivyo Dar es Salaam na wakaweza kuamua kuwa Entebbe yawe makao makuu ya serikali, walithubutu, wakaweza na sasa wanasonga mbele.

 

Jiji letu la Dar es Salaam ni la kibiashara. Limejaa makontena kila kona, limejaa baa na makasino, limejaa na kufura maji machafu, limejaa gereji za magari, mabohari ya vyuma chakavu, limejaa wafanyabiashara ndogondogo wanaofuata wateja walipo, nao sasa ni miongoni mwa wale wanaoshinda katika ofisi za serikali na vyama. Utendaji wa kazi umedorora. Foleni kila mahali; wafanyakazi wanaamka saa 10 alfajiri na kuanza safari ya kwenda ofisini wanafika saa tatu hadi nne kutokana na foleni. Wanatoka ofisini saa 10 na wanaingia nyumbani kwao saa 3 usiku – kisa foleni za magari na miundombinu mibovu.

 

Serikali imeamua kuboresha miundombinu Dar es Salaam ili kurahisisha usafiri na watumishi wa umma waweze kufika ofisini kwa urahisi, lakini swali linabaki palepale – Dodoma yetu mmeitupa na siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea? Mnadhani mtaendelea kujichanganya hapo Dar es Salaam hadi lini? Kuna nini kinachowasumbua hadi mshindwe kuhama?

 

Wabunge mnalikumbuka Azimio letu au ndiyo yapo ya muhimu zaidi kuliko hili ambalo lingeweza kuombewa mwongozo wa Spika? Mimi ningekuwa mbunge ningesimama na kuuliza “Mwongozo wa Spika lini serikali itahamia Dodoma?” Leo nakumbuka fikra za mwenyekiti, kwa hakika zidumu fikra za mwenyekiti na TANU oyeeeee.

 

Wasalaam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

315 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons