Na Samwel Kasori

CHATO

Alhamisi ya Machi 17, mwaka huu ni mwaka mmoja tangu nchi yetu iondokewe na Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Joseph Magufuli.

Hiki ni kipindi cha kutafakari mambo mengi, hususan jinsi Dk. Magufuli  alivyojitoa sadaka katika kuijenga Tanzania yetu kwa misingi ya kujiamini, kujitegemea na kwa kujenga uthubutu mkubwa kwa yale yote ambayo kwa miaka kadhaa kwa bahati mbaya sana tulikuwa tumekwisha kuyakatia tamaa kuwa kamwe hayatawezekana.

Kumbukizi hii ya mwaka mmoja tangu kuondokewa kwa Dk. Magufuli ni kipindi ambacho kinatupatia sisi Watanzania nafasi ya kutafakari juu ya mambo mengi, hasa yaliyosaidia kuijenga nchi yetu ya Tanzania kwa misingi ya kujiamini na kuthubutu, hata kwa yale ambayo tulikuwa tukiona kwamba hatuyawezi. 

Yeye, Dk. Magufuli, kwa kujituma kufufua fikra za ujenzi wa uchumi wetu kwa falsafa ya kujiamini na kujitegemea, huo ni urithi mkubwa aliyotuachia na ni muhimu kitaifa tujenge nidhamu stahiki kwa kuuenzi, hasa tunapoendeleza jitihada za kuijenga nchi yetu katika nyanja zote za kimaendeleo. 

Narudia kuwa, kujiamini na kujitegemea hizo ni tunu maalumu alizotuachia hayati Dk. Magufuli na tunapaswa kujituma kuziendeleza kwa nidhamu maalumu.

Kwa heshima na taadhima, ninasema tuzidi kumshukuru Mungu wetu kwa kuendelea kuitunza familia ya Dk. Magufuli, pia kwa kuendelea kudumisha haki na amani katika nchi yetu, hasa katika kipindi hiki cha mpito.

Katika kitabu cha Mathayo 28:20, Mungu alituahidi kwamba daima hatatuacha hadi ukamilifu wa dahari, hivyo tusikate tamaa katika kuijenga nchi yetu kwa kuzingatia misingi mizuri iliyojengwa na kiongozi wetu mpendwa, Dk. Magufuli, ambaye sasa hatuko naye.

Huu ndio utakuwa urithi mzuri na wa maana kuuendeleza kwa vizazi na vizazi, kila wakati tutakapokuwa tukikumbuka mchango wake hayati Dk. Magufuli kuhusu maendeleo ya taifa letu la Tanzania.

Katika kitabu cha Mtakatifu Mathayo imeandikwa kuwa: “Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya kuitetea haki.”

Hapa nipende kuuliza kuwa hivi katika heri zote zilizotajwa katika kitabu cha Mathayo, sura ya tano, je, ni kweli hakuna heri hata moja ya Kristo yenye kulingana na kujitoa sadaka kwa hayati Dk. Magufuli wakati wa uongozi wake alipokuwa rais wa nchi ya Tanzania?

Nasema iwe iwavyo kwa yote aliyoyatenda Dk. Magufuli, tulio hai hatuna wajibu kuziangalia tabia zetu.

Mungu aendelee kumpa Dk. John Pombe Magufuli pumziko la amani, milele na milele. Amen.

Mwandishi, Kasori S. H., ni Katibu Myeka (mstaafu) wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

By Jamhuri