PEMBA

Na Yusuph Katimba

Nenda uendako, lakini ukifika katika Kisiwa cha Kojani, kilichopo Mkoa wa Kaskazini Pemba, utastaajabu maisha yao, kama si kuugumia maumivu, basi unaweza kumwaga machozi.

Ukiwa kwa mbali, fikra za haraka unaweza kudhani Kojani ni kisiwa kilichohamwa, lakini kadiri unavyosogea unaanza kuona maisha ya Watanzania wenzetu yakiendelea.

Nimefika Kojani nikiwa katika timu ya wahariri 10 iliyotembelea kisiwa hicho. Ilikuwa baada ya kumaliza Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uliofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil, kuanzia Machi 9 – 11, 2022.

Mkutano huo uliohudhuriwa na wahariri wawakilishi kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Zimbabwe, Malawi na Burundi, ulifunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Turejee katika mada ya makala hii; taswira ya Kisiwa cha Kojani inafifisha nuru ya macho, inaondoa matumaini ya kesho na inaashiria uchovu wa wakazi wake kutokana na hisia za kutengwa katika maendeleo, Kisiwa cha Kojani kinahitaji kutazamwa kwa jicho la pekee.

Kisiwa cha Kojani kilicho na shehia mbili; Shehia ya Kojani na Shehia ya Mpambani, kimekosa alama nyingi za maendeleo; hakina barabara ya lami, hakina kituo cha polisi, hakina zahanati na amini usiamini, Kojani hakuna pikipiki (bodaboda) wala gari!

Baadhi ya wakazi wake hawajui hata mlio wa gari unafananaje! Lakini kina umeme na maji ya msimu. Kwa kusema ukweli Kojani bado haijaingia karne ya 21.

Kwa mujibu wa Amina Ahmed (wa Idara ya MAELEZO, Pemba), ni takriban dakika 15 kwa mwendo wa miguu au dakika tano kwa usafiri wa daladala au wa gari binafsi kutoka Madenjani hadi kufika katika barabara kuu iendayo Bandari ya Likoni kuelekea Kisiwa cha Kojani.

Eneo la Madenjani ni lango kuu la kuingilia na kutoka katika miji maarufu ya Kisiwa cha Pemba kama Chake Chake, Wete na Micheweni, ambapo barabara hiyo ndiyo ya kuelekea Kisiwani cha Kojani.

Ukiwa hapo Madenjani, utaacha njia zote na kufuata barabara iendayo Micheweni, ndipo utakutana na bango kuuubwa linalokuashiria njia ya ndani ya kuelekea Kisiwa cha Kojani.

Ni umbali wa dakika 10 hadi 20 hivi kutoka Bandari ya Likoni hadi kufika ndani ya Kisiwa cha Kojani kwa kutumia vivuko vya majini ambavyo ni ngalawa, mashua, dau au boti.

Unapovuka maji (Bahari ya Hindi) kwenda upande wa Kisiwa cha Kojani na kukisogelea, utaanza kuona dalili zote za maisha ya watu waliochoka hata kabla ya kukanyaga ardhi yao.

Utaona nyumba zilizofungamana mithili ya watu mkutanoni, zikiwa zimeezekwa kwa nyasi huku fito za kuta zikibaki uchi baada ya udongo uliojengewa kuporomoka.

Kisiwani Kojani itakukuchukua muda mfupi sana kuhesabu nyumba zilizoezekwa kwa bati, utashuhudia uchafu uliozagaa kandokando ya Bahari ya Hindi na ukiwa mtulivu, unaweza kuona kinyesi kikielea juu ya maji ya bahari.

Ladha na thamani ya Kisiwa cha Kojani inapotea zaidi pale unapoanza kupenya kwenye vichochoro vyake, unakaribishwa kwa macho ya mshangao ukiwa si miongoni mwao.

Ukifika Kojani muhimu ujitambulishe, usipofanya hivyo huenda yakakufika makubwa. Hisia za wakazi wa Kojani kwa serikali ni ‘tumetengwa.’ Unapozungumza nao, wanaamini hawathaminiki.

Wana Kojani wanasimulia kwamba, ladha na fahari ya kuitwa Wazanzibari inawatoka na wanatamani kukumbukwa katika ‘ufalme’ wa Rais Dk. Mwinyi.

Wanaeleza viongozi wakuu hawana mawasiliano na Kojani, hawafiki Kojani na huenda taarifa wanazopata kutoka Kojani haziendani na uhalisia wao.

Kumbukumbu zao kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, hazionyeshi mahala kiongozi wa nchi au wasaidizi wake wa karibu (mawaziri), waliowahi kukanyaga ardhi ya Kojani.

Wanasema: “Hapa alikuwa akija mke wa Rais Aman Karume tu. Si viongozi wakuu au mawaziri wanaokuja huku. Wamebaki huko na taabu zetu huku hawazijui.

“Kwa kuwa tupo kisiwani, basi tunafanywa kuwa kisiwa kisichohitaji ushirikiano na serikali, tunaamini serikali siku ikiamua, kisiwa hiki kitabadilika.”

Mzee Rashid (si jina halisi) anasema: “Mie nipo hapa muda wote, nimeona tawala zote kabla ya mapinduzi, lakini sioni viongozi wakubwa wakija hapa. Tunawasikia tu huko.”

Imeelezwa kuwa kisiwa hicho kina zaidi ya wakazi 13,000 ikiwamo wanaoishi nje ya kisiwa lakini wenye asili ya Kojani.

Kwa sasa kisiwa hiki kimefanywa kituo cha dawa za kulevya, wanaosafirisha dawa hizo, huona wapo salama Kojani kwa kuwa hakuna Kituo cha Polisi wala askari wa aina yoyote.

Hawakumbani na hekaheka zozote, kwao ni salama kwa kuwa Kojani hakuna ‘serikali.’ Wanaingia na kutoka wakiwa huru.

Hata wana Kojani wakiwaona, watawafanya nini? Wakazi wa kisiwa hicho wanajilinda na kujilea wenyewe.

Taarifa za Kojani zinaeleza kuwa dawa za kulevya zimekuwa zikivushwa kutoka Tanga na wahusika wanapofika Kojani wanakuwa huru kwa kuwa hakuna polisi.

“Watoto wetu wamebaki salama kwa kuwa hawatumii, ni kwa kuwa hawana pesa, vinginevyo wangeangamia wote,” anaeleza mkazi wa Kojani.

Kisiwa cha Kojani kina shule (skuli) mbili; moja ya sekondani iliyojengwa na Rais (mstaafu), Amani Abeid Karume, ingawa yeye mwenyewe wala hajawahi kuiona mpaka sasa!

Shule nyingine ni ya msingi (Skuli ya Msingi Kojani), ambayo watoto wote wanarundikwa hapo. Mwalimu Amri Suleiman (si jina halisi) wa skuli ya msingi anasema: “Ninafundisha wanafunzi 109 katika darasa moja. Ninajitolea.”

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inazo au imepata fedha za UVIKO-19, lakini fedha hizo bado hazijaacha athari yoyote chanya katika kisiwa hicho, wananchi wake hawajui kinachoendelea na serikali haijanyoosha mkono wake kupafikia Kojani.

Unapopita katika vichochoro vya Kojani, unaweza kukutana na mabinti wenye umri wa miaka 17 wakihudumia nyumba zao.

Kojani ina tatizo kubwa la ndoa za utotoni na uzazi usio wa mpango, hakuna elimu ya kutosha kwa kuwa hawafikiwi na watoa elimu. Kisiwa cha Kojani kimeachwa na kutelekezwa katika mambo mengi kama si mambo yote.

Wazazi wa Kojani wanawazuia binti zao kuendelea na masomo. Kaulimbiu yao ni ‘ndoa kwanza’. Vijana wanatimkia baharini kuvua samaki, hakuna anayekuwa mfano kwao ili kusisimua mwamko wa elimu. Taswira ya Kojani ya leo, afadhali ya jana.

By Jamhuri