Ifuatayo ni hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), aliyoitoa kwenye Ukumbi wa Idris Abdul Wakil, Zanzibar, Machi 9, 2022

Kwanza kabisa, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu; mwingi wa rehema kwa kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha kuifikia siku ya leo ya Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa mara ya kwanza hapa Zanzibar tukiwa salama. 

Kadhalika, napenda kuwapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwahabarisha Watanzania bila kuchoka kuhusu  masuala mbalimbali nchini mwetu na nje ya nchi, hali iliyoimarisha umoja, amani, mshikamano, maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Hii ndiyo misingi mikubwa na muhimu ya maendeleo ambayo Watanzania wanaendelea kuyashuhudia katika sekta zote nchini, ikiwamo na hasa hasa vyombo vya habari. Natoa shukurani zangu za dhati kwako; Ndugu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri; Bwana Deodatus Balile, kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hii ya uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania kwa mwaka huu wa 2022.

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Nimejulishwa kwamba, tangu mwaka 2009, Jukwaa la Wahariri Tanzania lilipoanzishwa mmekuwa na utamaduni wa kuwa na mkutano mkuu mwaka hadi mwaka. Nafahamu kuwa kwa muda wote huo, wahariri hamjawahi kufanyia mkutano mkuu Zanzibar na kwa mara ya kwanza mwaka huu mmefanya uamuzi sahihi kuleta mkutano huu hapa Zanzibar. Nasema karibuni sana, na mjisikie mko nyumbani.

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Katika wadhifa wangu wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na mtu niliyeitumikia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi za uwaziri, natambua na kuheshimu sana nafasi na umuhimu wa vyombo vya habari kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nafahamu kwamba vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa katika kujenga umoja wetu, amani yetu, udugu wetu, uchumi wa watu wetu, taifa letu na mshikamano wetu.

Mafanikio ya kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji, hutegemea kuwapo kwa taarifa sahihi kwa wananchi katika wakati mwafaka, zinazofuata misingi ya utawala wa sheria na uhuru wa vyombo vya habari. Ni dhahiri kuwa ustawi wa wananchi wetu, pamoja na mambo mengine kwa kiasi kikubwa unategemea kuwapo kwa vyombo vya habari huru vinavyosimamia ukweli kwa kufikishia wananchi taarifa sahihi na kufikisha taarifa za wananchi kwa viongozi wao; yaani serikalini.

Kwa hivyo, wananchi wanatarajia kuwa vyombo vyetu ya habari vinasaidia kuwainua na kufanikisha shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Kuwapo kwa vyombo vya habari vyenye ubora wa hali ya juu, ndiko kutafanikisha uchumi wao, biashara zao na shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato.

Nimefurahi pia kuona Jukwaa la Wahariri linaendelea kukua na kukuza ushirikiano kati yake na serikali, wadau wa maendeleo – zikiwamo taasisi zetu hapa nchini kama ZSSF, NSSF, ZRB, TRA; benki kama NMB na CRDB na wengine, huku tukiwa na mataifa jirani ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi na Zimbabwe ambayo wahariri kutoka nchi hizo sita wako hapa. Ushirikiano huu ni muhimu na naomba muuendeleze. Nasema hongereni sana.

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Nafahamu Kaulimbiu ya Mkutano huu ni “Uchumi wa Buluu na Mawasiliano ya Umma.” Kaulimbiu hii inatutia hamasa, inatutia moyo, imani na kutuongezea nguvu kwamba hata vyombo vya habari sasa vimeona umuhimu na kuitupia jicho ajenda ya Uchumi wa Buluu. 

Nasema asanteni sana. Dhana ya Uchumi wa Buluu ilianza kushika kasi mwaka 2012 katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo Endelevu katika mji wa Rio de Janeiro nchini Brazil (Maarufu Mkutano huu ukijulikana kama ni Rio +20). 

Huu ulikuwa ni wakati wa kuiangalia bahari katika hali yake ya upekee katika masuala ya uhifadhi na maendeleo ndani ya mfumo mzima wa Uchumi wa Kijani ulimwenguni. Tangu wakati huo, nchi mbalimbali duniani zimeitupia jicho bahari na kuanza kuwaza uwekezaji mkubwa katika bahari pamoja na kuzidisha jitihada za kuyahifadhi mazingira yake.

Mtakumbuka kuwa tangu enzi, bahari imekuwa ikitumiwa katika sekta mbali mbali za maisha ya binadamu. Hii ikiwamo uvuvi na mazao ya baharini,   kusafirisha abiria,  bidhaa za chakula na kibiashara,  pamoja na uimarishaji wa usalama wa watu na hekaya zao. 

Haya ndiyo matumizi makubwa ya bahari yanayofahamika kwa watu walio wengi katika zama hizo. Lakini baadaye, na baada ya ukuaji wa teknolojia, baadhi ya nchi zikaanza uchimbaji wa mafuta na uvunaji wa gesi katika kina kirefu cha bahari hapa duniani. 

Leo, sambamba na mafuta na gesi, nchi nyengine tayari zipo mstari wa mbele katika kuzalisha nishati mbadala na uchimbaji wa madini  kutoka bahari hiyo hiyo.  Na wengine tukaanza kutumia ubunifu wa ikolojia ya bahari na maliasili zake za majini na fukweni kukuza sekta yetu ya Utalii.  Lakini hakukupata kuwapo msisitizo wa uwekezaji kiuchumi katika bahari, sawa na inavyofanyika katika ardhi ya nchi kavu, kama ilivyo leo.

Ni kweli, uwekezaji wa baharini unahitaji teknolojia maalumu, ujuzi, mitaji mikubwa na hamasa kwa wananchi ambao kwa muda mrefu hawakujipa muda kufikiri iwapo baharini kuna uwezekano wa kuchimba madini, kufuga samaki, kulima mazao ya biashara kama mwani na shughuli nyingine nyingi za kiuchumi. Na kama ulivyosema Mwenyekiti, bahari ni sehemu pekee ambayo haina migogoro mingi ya viwanja kama ilivyo kwa ardhi ya nchi kavu.

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Kwa upande wa Zanzibar kwa mfano, dhamira ya serikali ya kujenga uchumi wa kisasa unaozingatia matumizi sahihi ya rasilimali za bahari au kama unavyofahamika Uchumi wa Buluu, ni jitihada za dhati kabisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga uchumi utakaowasaidia wananchi wa Zanzibar. 

Ni dhahiri kuwa kufanikiwa kwa dhamira na jitihada hizi za serikali yetu, kutategemea uwezeshi na mchango mkubwa wa sekta ya habari, hasa kuwafikishia wananchi taarifa sahihi za fursa zilizopo kwa wakati mwafaka. Taarifa sahihi kupitia vyombo vya habari zitajenga hamasa kwa wananchi kushiriki katika Uchumi wa Buluu kwa vitendo.

Kwa hivyo, natumia fursa hii adhimu ya uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania wa mwaka 2022, kutoa wito kwa wahariri, waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari kuielewa na kuifanyia kazi mipango yetu mikuu ya uchumi na kuwa huru kutoa ushauri wenu serikalini kwa lengo la kuifanikisha. 

Tunatambua kuwa zipo sheria ambazo huenda zikawa ni kikwazo cha kufikia matarajio yetu ya kiuchumi na ustawi wa jamii. Sheria hizo zitahitaji kufanyiwa mabadiliko ili zifanikishe mipango yetu ya uchumi wa kisasa. Kwa hivyo, tumieni utaalamu wenu kuishauri serikali yetu kuchukua hatua za kurekebisha sheria ambazo zina kasoro, nasi tutafanya hivyo kwa masilahi mapana ya nchi yetu na Watanzania wote. 

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Katika hotuba yangu ya tarehe 11 Novemba, 2020, nilipokuwa nikilizindua Baraza la Kumi la Wawakilishi Zanzibar, niliweka wazi dhamira yangu ya kuijenga Zanzibar mpya, yenye uchumi wa kisasa wa Buluu (Blue Economy). Uchumi wa Buluu ni matumizi endelevu ya rasilimali za bahari. Huu ni uchumi unaofungamanisha kwa pamoja sekta za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini. 

Katika hotuba yangu hiyo, niliwakumbusha wawakilishi kwamba Zanzibar ina haja ya kufanya mabadiliko ya kiuchumi kwa kuzitumia ipasavyo rasilimali za bahari kutokana na kuwapo kwa udogo wa ardhi huku idadi ya watu wake ikiendelea kuongezeka. Katika hotuba hiyo nilisema, nina nukuu:

“Zanzibar hatukujaaliwa ardhi kubwa. Nchi yetu ni visiwa. Idadi ya watu wetu imeongezeka mara tano katika kipindi cha miaka 56. Mwaka 1964 Wazanzibari tulikuwa laki 3 tu, leo tuko takriban milioni 1.6. Wakati huo huo visiwa vyetu havipanuki wala kuongezeka. Ndiyo kusema, ardhi yetu inazidi kuwa finyu mwaka hadi mwaka. Ahueni tuliyonayo ni kuwa na eneo kubwa la bahari. Hivyo sisi Wazanzibari hatuna budi tuigeuze bahari hii kuwa ndilo shamba letu. Huko ndiko fursa na ajira za Zanzibar mpya zilipo. Huu ndio msingi wa dhana nzima ya Uchumi wa Buluu.”

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Ni matumaini yangu kuwa, wahariri na waandishi mkielewa dhana ya Uchumi wa Buluu, tutakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na za kimaendeleo katika kujenga uchumi wa Buluu kwa upande wa Zanzibar. Kwa lugha nyingine, wananchi wako tayari, wanachosubiri ni taarifa sahihi za kuwaonyesha fursa za Uchumi wa Buluu zilipo. Mimi binafsi nitafurahi sana kama wahariri na waandishi, mtakuwa na mijadala ya dhati kuhusu Uchumi wa Buluu ni nini, fursa zinapatikana wapi, iwapo kuna vikwazo mkatujulisha ni vipi tuviondoe na mengine mengi ya aina hiyo, kwa lengo la kufanikisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Awamu ya Nane ya ujenzi wa Uchumi wa Buluu.

Nafahamu na hapa leo nimeshuhudia mada mbili zikiwasilishwa na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, na ile aliyowasilisha Mzee Salim Said Salim kwa niaba ya wahariri. Naamini mtakaa pamoja na kuzichambua kwa kina mada hizi, muulize maswali na mpewe majibu sahihi, kwa nia ya kuwawezesha kuandika habari za Uchumi wa Buluu mkiwa na uelewa mpana, hivyo kuwasaidia wananchi kuielewa ajenda hii.

Lakini pia naomba kusisitiza umuhimu wa wahariri na waandishi wa habari kusimamia na kuyaishi maadili ya uandishi wa habari. Uandishi bora unaendana na uadilifu, kutovunja sheria, kuwa wakweli na wawazi. Nia ya msingi na shabaha ya habari mnazoziandika, ilenge katika kuimarisha mshikamano, kujenga umoja katika nchi, utulivu na amani. 

Amani ni mtaji mkubwa katika kufikia kila lengo la maendeleo. Ndiyo maana Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) niliyoiunda hapa Zanzibar imemaliza misuguano ya kisiasa iliyodumu kwa muda mrefu, nchi ina amani na utulivu na sasa ajenda yetu ni moja tu kama taifa; kuwaletea wananchi maendeleo.

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Nawashukuru kwa kutambua umuhimu wa mikutano ninayoifanya kila mwezi na wahariri na waandishi wa habari. Hata mimi na serikali yangu tumeanza kuona tija ya mikutano hii. Nimeona kila mnapouliza maswali nikayatolea majibu, mambo mengi yanayokuwa yamekwama yanakwamuliwa. 

Wananchi kwa sasa wanaifuatilia kwa karibu mikutano hii, na kama mnavyosema ninyi, wanapoona mambo hayaendi, wanakutafuteni kuwaeleza matatizo yao mnifikishie. Hili ni jambo jema, kwani nami linanirahisishia kazi yangu katika uendeshaji wa serikali. Nawahakikishia kuwa nitaendelea na mikutano hii ya wahariri na waandishi kila siku ya mwisho wa mwezi.

Wito wangu kwa mawaziri na watendaji mbalimbali ni kwamba waendelee kutoa taarifa mara nyingi kadiri inavyowezekana na kwa uwazi. Kama nilivyosema, waziri au mtendaji mwenye wajibu wa kusimamia wizara au taasisi ya serikali nikibaini kuwa hatoi taarifa, hicho kitakuwa moja ya vipimo vya ufanisi wake kazini. Maana kama mtu amefanya utekelezaji wa shughuli mbalimbali atakuwa nalo la kusema na kama hajafanya lolote, huyo atakuwa hana la kusema,  hivyo ni wazi kiongozi wa aina hii atakuwa anakwamisha kasi ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar, na kamwe sitamvumilia.

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Nimelisikia ombi lenu juu ya mabadiliko ya Sheria zinazohusiana na masuala ya habari kwa nia ya kupanua wigo wa uhuru wa habari nchini. Sheria inayosimamia Utangazaji ya The Zanzibar Broadcasting Commission Act, 1997 na Sheria ya Usajili wa Magazeti inayofahamika kama The Registration of News Agent, Newspapers and Books Act No. 5 of 1988.

Pia nimeyasikia hayo malalamiko kuwa sheria inayopendekezwa inaanzisha vyombo vingi badala ya kuundwa kwa chombo kimoja cha kusimamia Sekta ya Habari nchini kama ilivyo kwa Wanasheria wa Zanziabr (ZLS), Baraza la Madaktari Zanzibar (ZMC), Bodi ya Wagavi na Wahasibu (NBAA) na taaluma nyingine nyingi nchini. Hili nimelichukua nitalifanyia kazi.

Hata hivyo, naelekeza idara zinazosimamia sheria hizi zikae na wadau wa habari, mwelezane na mkubaliane misingi bora ya utungaji wa sheria hizi itakayozaa sheria bora zinazoimarisha na kukuza uhuru wa vyombo vya habari. Nataka ndani ya miezi 6, tumalize suala hili lililokaa miaka mingi sasa. Mkae, mjadiliane na kuhakikisha ndani ya miezi sita tunafanya marekebisho ya sheria hizi. Sheria hizi zikiwa nzuri, hata uandishi juu ya ajenda yetu ya Uchumi wa Buluu utaimarika. Tutafunga vichaka vya watu kuficha habari na hii itasaidia kuongeza kasi ya maendeleo.

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Nimefurahi sana kusikia kuwa wazo la kufufua Jukwaa la Wahariri Tanzania Kanda ya Zanzibar mmelifanyia kazi. Jukwaa la Wahariri ni chombo muhimu kwa mawasiliano kati ya vyombo vya habari na serikali na wadau wengine. Ni matumaini yangu sababu zilizoliua mwanzo, hazitarejea tena na kuliathiri baada ya mimi kulizindua leo.

Ndugu wahariri na wageni waalikwa,

Mwanzo nimeeleza kuvutiwa kwangu na ushirikiano mlionao kama Jukwaa la Wahariri na wadau mbalimbali zikiwamo serikali zetu mbili; Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawapongeza kwa uamuzi wa kuweka umuhimu wa pekee katika ajenda yetu ya Uchumi wa Buluu. Ni matumaini yangu kuwa baada ya mkutano wa leo, tutaona na kusoma habari nyingi za Uchumi wa Buluu kwa maendeleo ya taifa letu.

Nazipongeza pia taasisi za serikali na wadau waliochangia kufanikisha mkutano huu ikiwamo NSSF waliotoa posho za siku tatu kwa wahariri kutoka Tanzania Bara; Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar; Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar; ZSSF, ZRA, TRA, TANESCO, CRDB, NMB, ASAS Diaries, TANAPA, Ngorongoro, WCF, NHC, TCRA na TFS. Pia niseme nami nimezipokea shukrani zenu kwa mchango uliotolewa na ofisi yangu kusaidia kufanikisha shughuli hii. Na nawaahidi kuendeleza ushirikiano huu.

Ndugu wahariri na wageni waalikwa, mabibi na mabwana;

Baada ya maelezo haya sasa natamka kuwa Mkutano Mkuu wa Sita wa Jukwaa la Wahariri Tanzania wa mwaka 2022 nimeuzindua rasmi.

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR.

MUNGU IBARIKI TANZANIA.

MUNGU IBARIKI SEKTA YA HABARI NCHINI.

Asanteni kwa kunisikiliza.

By Jamhuri