Na Nizar K Visram

Limekuwa jambo la kawaida kwa vyombo vya habari na serikali zao za Magharibi kuilaani Urusi, wakisema ni uhalifu wa sheria ya kimataifa kwa nchi moja kuivamia nchi nyingine. 

Lakini sheria hiyo hutiwa kapuni pale nchi za Magharibi zinaposhambulia au zinaposaidia kushambulia nchi zingine.

Kwa mfano, mashirika ya utangazaji kama CNN, BBC, VOA, DW, RFI yamekuwa hodari wa kuilaani Urusi lakini ni nadra kuona wakilaani mauaji ya raia wa Yemen, au ubaguzi na ukaburu wa Israel nchini Palestina. 

Hata pale mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu kama Human Rights Watch na Amnesty International yanapofanya uchunguzi wa kina na kuandika ripoti bayana kuhusu ukaburu huo lakini ripoti zao hazitangazwi.

Hawatatangaza jinsi Marekani na majeshi ya NATO yalivyovuruga nchi kama Libya, Iraq, Syria, Somalia, Honduras, Bolivia, Brazil, Venezuela, Nicaragua, Cuba na kadhalika. 

Orodha ni ndefu mno. Hawataeleza ni sheria gani ya kimataifa imeipa Ufaransa haki ya kumiliki Kisiwa cha Mayotte nchini Comoro.

Hawataeleza kwanini barani Afrika kumekuwa na mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na makamanda waliofunzwa na kupewa silaha na majeshi ya Ufaransa na Marekani (AFRICOM). Huu ni unafiki.

Kitu kimoja kimejitokeza wazi katika vita ya Ukraine ni ubaguzi wa rangi katika nchi za Magharibi. Wanaamini kuwa Afrika na kwa Waarabu ndiko watu wanapigana na kuuana. Halafu wanashangaa inakuaje nchi za Ulaya ‘zilizostaarabika’ zinauana, wakisahau kuwa ni hao ndio walioanzisha Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia. Kwamba ni wakoloni kutoka Ulaya ndio walioanzisha vita ya kikoloni katika ulimwengu wa tatu.

Mfano mmoja wa huu ubaguzi tunaozungumzia hapa ni ripoti iliyoandiwa kutoka Kiev, mji mkuu wa Ukraine na Charlie D’Agata, mwandishi wa kituo cha utangazaji cha CBS nchini Marekani. 

Akiwa anahojiwa na CBS kuhusu wakimbizi wa Ukraine anasema: “Tofauti na Afghanistan au  Iraq, Ukraine ni nchi iliyostaarabika, yenye utamaduni wa Kizungu.” Yaani wakimbizi wa Ukraine wamestaarabika zaidi kuliko wale wanaotoka Asia, Uarabuni na Afrika.

Mfano mwingine ni mwendesha mashtaka wa zamani wa Ukraine, David Sakvarelidze. Alipokuwa akizungumza na BBC akasema: “Kwangu mimi ni jambo la masikitiko makubwa kuona Wazungu wenye nywele rangi ya shaba na macho rangi ya buluu wakiuawa kwa makombora, roketi na helikopta za Putin.”

Hii ni mifano ya ukaburu na unafiki. Inaonyesha fikra potofu kuwa vita ni hulka ya watu wa ulimwengu wa tatu, na wala si kawaida ya Wazungu ‘waliostaarabika.’

Ubaguzi wa rangi umeonekana wakati watu kutoka Ukraine wanakimbilia Poland na Bulgaria. Wazungu wanaruhusiwa kuvuka mpaka bila tabu lakini weusi wanazuiwa. Sababu ni dhahiri kwa sababu Waziri Mkuu wa Bulgaria ametamka kuwa wakimbizi wa Kiukrania ni: “Wazungu wenzetu wenye elimu na akili, tofauti na hawa tuliowazoea siku nyingi ambao miongoni mwao kuna magaidi.”

Pia katika gazeti la Uingereza liitwalo The Telegraph, mwandishi Daniel Hannan, amesema: “Wakimbizi wa Ukraine wanafanana na sisi kiutamaduni, jambo linalotusikitisha mno kwa sababu vita ilikuwa ni kawaida ya nchi maskini lakini sasa hali hii inabadilika.”

Yaani alimaanisha kuwa wakimbizi wasio weupe kutoka nchi kama Syria, Afghanistan, Palestina, Nigeria, Somalia, Iraq na Yemen wamezoea vita na migogoro kwa hiyo kwao ni jambo la kawaida.

Katika vita ya Ukraine ubaguzi na ukaburu umejitokeza wazi wazi kiasi kwamba ikabidi Umoja wa Afrika (AU) utoe risala ikisikitishwa kuwa raia wa Afrika nchini Ukraine wanazuiwa kuvuka mipaka ili kujisalimisha. Risala hiyo ya  Februari 28, mwaka huu inasema:

“Kila mwanadamu ana haki ya kuvuka mipaka ya nchi ili kuokoa maisha yake wakati wa mgogoro. Katika vita hii ya Ukraine wakati raia wanakimbilia nchi za jirani, haki hii inapaswa itolewe kwa wote bila ubaguzi wa rangi au uraia.”

Licha ya ukaburu pia kuna unafiki katika suala hili la Ukraine na Urusi. Kwa mfano Yair Lapid, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel hakuchelewa kuilaumu Urusi, akisema uvamizi wake wa Ukraine ni uhalifu mkubwa wa kanuni za kimataifa. Akasema Israel imepigana na inaelewa kuwa vita si dawa ya kusuluhisha mgogoro.

Wakati huohuo raia wa Israel waliandamana mjini Tel Aviv huku wakibeba bendera ya Ukraine na kuimba ‘Ukraine Huru.’  Wapalestina waishio Tel Aviv wameshangaa, kwa sababu wao wakiandamana na bendera yao na wakiimba ‘Palestina Huru’ mara moja watakamatwa na polisi, watapigwa marungu na risasi na watawekwa gerezani bila ya kufikishwa mahakamani. Yaani uhuru ni haki ya Ukraine tu, wala si Palestina. 

Baada ya Urusi kuishambulia Ukraine, Waziri Mkuu wa Canada, Justine Trudeau, amesema Urusi ni mvamizi. Akaiwekea vikwazo Urusi na kutuma misaada Ukraine.  

Lakini Canada hiyo hiyo ilikaa kimya wakati Israel ilipowashambulia na kuwaua Wapalestina mnamo miaka ya 2008, 2014, 2018, 2020 na 2021. Wakati Israel inaipiga mabomu Gaza serikali za Canada, Marekani na kadhalika zilikaa kimya. 

Sheria ya kimataifa na kanuni za UN zinatumika kuibana Urusi. Israel inapotumia mabomu na kuwaua Wapalestina wanasema eti ni ‘kulinda usalama wa Israel.’

Mwaka 2014 Urusi iliichukua Crimea iliyokuwa sehemu ya Ukraine. Mara moja Canada ikaja juu na kusema ‘nchi yoyote haipaswi kubadilisha mipaka yake kwa mtutu wa bunduki.’

Mwanasheria wa UN, Profesa Michael Lynk, akasema huo ni unafiki kwa sababu hata majeshi ya Israel mwaka 1967 yalivuka mipaka yake na kuivamia ardhi ya Palestina na sasa inadai kuwa hiyo ni mali ya Israel. 

Vivyo hivyo ikachukua milima ya Golan nchini Syria. Lynk anasema kwa Canada kutoikemea Israel maana yake inatumia vigezo tofauti kwa Urusi na Israel. Ni unafiki.  

Canada na nchi za Magharibi hawakuchelewa kuiwekea Urusi vikwazo vya kila aina, lakini wakati huohuo wanapuuza maazimio ya UN yanayotaka Israel iwekewe vikwazo hadi itakapoheshimu sheria ya kimataifa. 

Si tu Canada imepuuza bali imesaini mkataba wa biashara huria baina yake na Israel (Canada-Israel Free Trade Agreement). 

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imeanza kuichunguza Israel kwa kuwanyima Wapalestina haki za binadamu na haki za kiraia. Serikali ya Canada inajaribu kuzuia uchunguzi huo usifanyike.Wakati huohuo wanazungumzia kumfikisha Putin ICC. Mkuki kwa nguruwe.

Ni vizuri tukajua kuwa wakati majeshi ya Urusi yalipokuwa yakiingia Ukraine wakati huohuo na Marekani nayo iliishambulia Somalia kwa mabomu, Saudi Arabia iliishambulia Yemen kwa mabomu na Israel iliishambulia Syria na Gaza.

Nchi za Magharibi zilishangilia wakati Yugoslavia ilipomeguka, hasa pale Croatia ilipojitenga kutoka Yugoslavia mwaka 1991. Kisha Waserbia nusu milioni wakatimuliwa kwa nguvu kutoka Krajina, Croatia mnamo mwaka 1995. Je, wakati huo nchi za Magharibi zilikuwa wapi?

Kwa muda wa miaka minane majeshi ya Ukraine yalikuwa yakiwashambulia wananchi wa Jimbo la Mashariki la Donbas. Ripoti ya UN inasema kuanzia mwaka 2014 hadi 2021 watu zaidi ya 14,000 waliuawa katika jimbo hilo na 50,000 walijeruhiwa. Wengi walikimbilia Urusi (Rostov). Wakati huo nchi za Magharibi zilikuwa wapi?

Mwaka 2011 nchi za NATO zilianzisha vita ya kumpindua Rais Bashar Assad wa Syria. Hadi leo wameshindwa. Matokeo yake wananchi wa Syria milioni 12 wamekimbilia nchi za jirani wanakoishi kambini wakinyeshewa mvua za barafu. Wamesubiri zaidi ya miaka 10 ili kuruhusiwa kuhamia Ulaya kama wakimbizi. Badala yake, ili kupunguza ‘mzigo’, EU imekubali kulipa dola bilioni 6.6 za Marekani kwa Uturuki ili iwachukue angalau wakimbizi milioni 3.7 kati ya hao wote.

Kwa upande wa pili, wakimbizi kutoka Ukraine haikuwachukua hata wiki moja. Siku nne tu baada ya Urusi kuishambulia Ukraine, takriban watu 400,000 wameruhusiwa kuingia nchi nne za EU zinazopakana na Ukraine. Mamilioni wengine wanatarajiwa kuingia EU wanakopatiwa huduma zote. 

Kama wasemavyo wenyewe, ‘hawa ni wenzetu, wale si wenzetu.’

[email protected] 

0693 555373

By Jamhuri