NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Uteuzi uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na kumpa Dk. Pindi Chana dhamana ya kuongoza Wizara ya Maliasili na Utalii unaifanya wizara hii iendelee kushikilia rekodi ya kuwa na mawaziri wengi ndani ya vipindi vifupi.

Dk. Chana aliyezaliwa mwaka 1974, anakuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa 24 tangu nchi yetu iwe jamhuri mwaka 1962. Waziri pekee anayeshikilia rekodi ya kudumu kwa muda mrefu kwenye wizara hii ni Zakia Meghji, aliyehudumu kwa miaka kenda. 

Profesa Jumanne Maghembe, yeye ana rekodi ya kuwa waziri kwa nyakati mbili tofauti (2007-2008 na 2016-2017).

Mtiririko wa mawaziri kuanzia sasa hadi mwaka 1962 ni kama ifuatavyo:

24. Dk. Pindi Chana (2022…

23. Dk. Damas Ndumbaro (2020-2022)

22. Dk. Hamis Kigwangalla (2017-2020)

21. Lazaro Nyalandu (2014-2015)

20. Balozi Khamis Kagasheki (2012-2013)

19. Ezekiel Maige (2010-2012)

18. Shamsa Mwangunga (2008-2010)

17. Profesa Jumanne Maghembe (2007-2008)

16. Anthony Diallo (2005-2006)

15. Zakia Meghji (1997-2005)

14. Juma Ngasongwa (1995-1996)

13. Dk. Juma Omar (1993-1995)

12. Abubakar Mgumia (1990-1993)

11. Marcel Komanya (1989-1990)

10. Arcardo Ntagazwa (1987-1989)

9. Getruda Mongela (1985-1987)

8. Paul Bomani (1984-1985)

7. Sir Geogre Kahama (1983-1984)

6. Ali Hassan Mwinyi (1982-1983)

5. Isaack Sepetu (1980 – 1982)

4. Solomon Saibul (1975-1980)

3. Hasnu Makame (1970-1975)

2. Dereck Bryceson (1965-1970) na

1. Tewa Said Tewa (1962-1965)

Swali linalogonga vichwa vya wengi ni kwa nini mawaziri wengi hawadumu kwenye hii wizara? 

Kujibu swali hili sharti kwanza kutambua unyeti, kwa maana ya ukwasi na umuhimu wa wizara hii katika maendeleo ya nchi yetu. 

Ingawa kuna wizara nyingine kama TAMISEMI, Nishati, na hata Madini, nazo zina ukwasi mkubwa, Wizara ya Maliasili na Utalii inaonekana kuongoza kwa vishawishi, lakini pia kwa fitina.

Hii ni wizara ambayo waziri anaweza kuingia na ahadi kemkemu za uadilifu, lakini baada ya muda akatopea kwenye ‘upokeaji zawadi’ na mambo mengine ya aina hiyo.

Wastani wa mchango wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa pato la taifa ni karibia asilimia 20; ilhali kwenye fedha za kigeni wizara inaingiza nchini robo ya fedha zote za kigeni.

Wizara hii ina vyanzo vya fedha vya uhakika vinavyotokana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA).

Kuna Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF), Vyuo vya Taaluma ya Misitu na Ufugaji Nyuki, Mfuko wa Misitu Tanzania, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Idara ya Mambo ya Kale na kadhalika.

Pili, kuna sekta binafsi inayoendesha masuala mbalimbali ya utalii ambayo mara nyingi yamehitaji baraka au mwongozo wa waziri husika. Kwa mfano, katika kutekeleza Ibara ya 67(a)(i) ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020 – 2025 inayoielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kukuza na kuimarisha utalii wa uwindaji wa wanyamapori, wizara imetakiwa ibuni mkakati unaovutia mitaji mikubwa na kwa muda mrefu katika maeneo maalumu ya vitalu vya uwindaji. Mkakati huu unajulikana kama ‘Special Wildlife Investment Concession Area (SWICA)’.

Hapa tunazungumzia vitalu vya uwindaji. Bahati mbaya si Watanzania wengi wanaoujua huu ‘mgodi’ wa vitalu vya uwindaji wa kitalii. Eneo hili lina mchango mkubwa mno kwenye kuhitimisha ngwe za uongozi za mawaziri wengi. 

Hili ni eneo la matajiri wanaowania kupata maeneo mazuri ya uwindaji kwa maana ya kupata aina adhimu za wanyamapori, mandhari na kadhalika.

Huko nyuma ugawaji wa vitalu ulifanywa na kamati maalumu iliyoundwa na waziri, ingawa mwenye kauli ya mwisho alibaki kuwa waziri mwenye dhamana. 

Mara kadhaa kamati hizo zilivunjwa baada ya kuhusishwa na rushwa, na ndipo ikaonekana huenda ugonjwa huo ukamalizwa kwa kuanzishwa utaratibu wa kugawa vitalu kwa njia ya mnada wa kielektroniki.

Siku za karibuni mnada huo ulifanyika, lakini habari za uhakika ambazo JAMHURI linazo ni kwamba mfumo wa mnada umeingiliwa kwa ushawishi wa matajiri wanaotaka vitalu kwa kushirikiana na baadhi ya wakubwa ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Dk. Ndumbaro ameondoka akijua kuna malalamiko mengi ya wadau wakitaka mnada huo ufutwe na itafutwe njia ya kukomesha rushwa, hasa inapotokea kwamba waendesha mnada wanatoa siri miongoni mwa washindani. 

Haikushangaza kuona, mathalani, aliyetaka kitalu kwa dola 250,000 alinyimwa, lakini akapewa aliyeweka dau la dola 200,000 za Marekani.

Jambo jingine kwenye biashara hii ni kuwa hata watu ambao kuna ushahidi wa ushiriki wao kwenye ujambazi wanapewa fursa ya kushindana na kushinda. Hili linawezekana kwa sababu uhakiki wa kina umepangwa ufanywe baada ya kampuni kushinda zabuni!

Yaani jambazi jangili anapewa kitalu halafu ndipo anachunguzwa kama ni jangili au si jangili! Lakini pia kampuni zinazopewa vitalu haziweki dhamana ya benki, jambo linaloweza kufanya kampuni hizo zikatelekeza vitalu muda mfupi baada ya kuvitwaa na kuua wanyamapori kiholela.

Kusanyiko la wawindaji wa kitalii hufanyika kila mwaka Reno, Nevada nchini Marekani. Kumekuwapo taarifa kwamba mawaziri kadhaa wa maliasili hutumia mwanya huo kukutana na matajiri na ‘mambo yote humalizwa’ huko. Haya yanasemwa na wawindaji wenyewe.

Urasimu unaosababishwa na mifumo mibaya umesababisha kuwapo vitendo vingi vya rushwa. Mara kadhaa wawekezaji wameombwa rushwa na walipotoa hawakutekelezewa masuala yao kwa wakati. Kwa kuona hivyo, wawekezaji hao wamekuwa na ujasiri wa kushitaki moja kwa moja kwenye mamlaka za juu za nchi. 

Mawaziri wawili wa Maliasili na Utalii zama za Awamu ya Nne wanadaiwa kung’olewa baada ya wawekezaji kushitaki kwa Rais.

Wakati fulani Waziri Meghji alipata kuliambia gazeti hili: “Wizara ya Maliasili na Utalii ina vishawishi vingi sana, mimi nilishafuatwa na watu wana briefcase imejaa dola za Marekani, niliwafukuza… ukiwa na roho nyepesi huwezi kufanya kazi za nchi kwenye hii wizara…”

Waziri wa Maliasili na Utalii ni mmoja kati ya mawaziri wachache mno wanaotumia usafiri wa ndege za mashirika yaliyo chini ya wizara kadiri anavyojisikia. 

Ana uwezo wa kutumia ndege za TAWA au TANAPA au hata ndege za kampuni za utalii au wawekezaji.

Kwa mfano, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Kigwangalla, alitumia ndege kuchukua wasanii na wakati mwingine kuwasubiri kutwa nzima alimradi tu akutane nao, kisha warejeshwe kwa gharama za umma. 

Waziri Nyalandu yeye alitumia ndege kwa shughuli nyingi binafsi, hali iliyosababisha manung’uniko mengi kutoka kwa watu mbalimbali. Kuna Waziri wa Maliasili na Utalii alikodi vyumba katika hoteli za nyota tano Dar es Salaam na Arusha, na walipaji wakawa ni NCAA na TANAPA. 

Vyumba hivyo vililipiwa hata kama hakulala. Lakini mara kadhaa mawaziri wa maliasili na utalii wametumia ndege na magari ya kampuni za wawekezaji, hali inayozua mgongano wa masilahi.

Waziri Nyalandu anakumbukwa kwa kutumia kibali cha Rais kubariki wanyamapori 704 wauawe na rafiki zake Wamarekani bila kulipa serikalini hata shilingi moja. Ni wakati wake ambao alisafiri na wasanii warembo nchini Marekani ‘kutangaza utalii’. 

Lakini ni wakati wake ambao serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii iliingia kwenye mpango wa kukodisha hifadhi za Tanzania kupitia Kampuni ya African Parks Network ya Afrika Kusini, mpango uliofutwa baada ya JAMHURI kuuanika hadharani. 

Bado wengi wanakumbuka namna alivyoshinikiza zitolewe Sh milioni 560 kwa mashindano ya urembo ya Afrika Mashariki ilhali mamia kwa maelfu ya Watanzania wakihangaishwa na baa la njaa.

Nyalandu huyo huyo Februari 20, 2014 alitoa ahadi ya kufungua mpaka wa Bologonja kwenye kikao cha mawaziri wa utalii na wanyamapori kutoka Tanzania, Kenya na Uganda, kilichoitishwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.

Kwenye kikao hicho kulikuwa na hoja kadhaa, lakini ni hoja moja iliyotawala mjadala wote. Nayo ilikuwa ni ya kufunguliwa kwa Bologonja. 

Ikumbukwe mpaka huu ulifungwa na Rais Julius Kambarage Nyerere miaka ya 1970 ili kulinda masilahi ya kiuchumi ya Tanzania. Hatua ya Nyalandu ilitokana na kukutana na wafanyabiashara na viongozi wa Kenya.

Waziri Maige yeye aliingia kwenye mvutano wa vitalu, lakini baadaye akabanwa kwenye ununuzi wa nyumba jijini Dar es Salaam. Maelezo yake kwamba nyumba hiyo alinunua kwa fedha zilizotokana na biashara ya usafirishaji mizigo, yalielekea kutowaingia wengi.

Wizara ya Maliasili na Utalii kwa miaka minane kuanzia mwaka 2006 iliongozwa na mawaziri sita. Alianza Anthony Diallo, akafuata Profesa Jumanne Maghembe, Shamsa Mwangunga, Ezekiel Maige, Balozi Khamis Kagasheki na Nyalandu. 

Kwa kipindi hicho makatibu wakuu waliopitia wizara hiyo ni Salehe Pamba, Blandina Nyoni, Dk. Ladislaus Komba, na Maimuna Tarishi. 

Kwa miaka minane Idara ya Wanyamapori iliongozwa na Emmanuel Severe, Erasmus Tarimo, Obeid Mbangwa, Profesa Songorwa na Sarakikya.

Fitina

Wizara ya Maliasili na Utalii pengine kutokana na ukwasi wake, imekuwa miongoni mwa maeneo magumu mno kwa viongozi waadilifu. Wale wanaoshindikana kukamatika kwenye rushwa wamekuwa wakikumbana na fitina na ‘songombingo’ za kila namna, alimradi wang’olewe na kuwekwa watakaobariki ufisadi.

Fitina hizi huchagizwa zaidi kwa wale wasiokuwa tayari kuyumbishwa kwenye utendaji haki na uzingatiaji wa sheria.

Ikitokea waziri amekuwa mtenda haki na akionekana hataki kufuata matakwa ya ‘walioikamata wizara’, basi hapo huanza kuundiwa majungu ambayo mwishowe hufika ngazi za uteuzi.

Waziri Kagasheki anatajwa kuwa mmoja wa viongozi waliosimama imara kwenye wizara hiyo, lakini akanaswa kwenye fitina ya Operesheni Tokomeza iliyoongozwa na vyombo vya dola ambavyo yeye kama waziri hakuwa na mamlaka navyo.

Lakini licha ya wabunge kutambua ukweli huo, waliungana na baadhi ya watu kuhakikisha Kagasheki anang’oka. Baadaye ilibainika kuwa baadhi ya wabunge waliosimama kidete kutaka ang’olewe walikuwa na maelfu ya mifugo waliyoilisha kwenye maeneo ya hifadhi, ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Wanasiasa

Wanasiasa ni sehemu nyingine chungu kwa mawaziri wengi wa Maliasili na Utalii. Kazi mojawapo ya waziri wa hii wizara ni uhifadhi. Imetokea wanasiasa hasa wakati wa uchaguzi kuendesha kampeni na ahadi za kuwapatia wananchi maeneo ya malisho, maji, kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu.

Walipoingia madarakani walishinikiza matakwa yao yatekelezwe, lakini waligonga mwamba kwa sababu waziri hana mamlaka ya kutengua sheria zilizotungwa na Bunge. 

Waziri anayesimamia sheria za uhifadhi mara zote ameonekana mbaya na imekuwa kawaida kwa waziri wa aina hiyo kuundiwa ‘zengwe’ ili hatimaye ang’olewe.

Woga wa mamlaka za uteuzi

Mara nyingine mamlaka za uteuzi zimeingizwa woga na kuamua kuwatoa ‘kafara’ baadhi ya mawaziri wa maliasili na utalii wanaoonekana kuwa kwenye mvutano na wananchi au makundi mengine.

Kwa mfano, mwaka 2014 Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kwa namna ya kutaka kuwafurahisha wananchi wa Ngorongoro, alitengua uamuzi wa kisheria wa Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo wa kutenga eneo la kilometa za mraba 1,500 katika Pori Tengefu la Loliondo.

Uamuzi huo, si tu kwamba ulimvunja nguvu waziri, bali ulitoa mwanya wa kumfanya aandamwe na aonekane asiyestahili kushika wadhifa huo. Hali hiyo imeifanya migogoro mingi idumu, na haishangazi kuona hata baada ya Dk. Ndumbaro kuondolewa, kuna watu walishangilia.

Waziri Chana 

Dk. Chana amepewa nafasi ya kuongoza Wizara ya Maliasili na Utalii wakati ambao inakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji ubunifu na ujasiri.

Anakabiliwa na kazi kubwa ya kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ya kuwa na watalii milioni 5 inatekelezwa. Idadi hiyo inapaswa iende sambamba na ongezeko la mapato yanayotokana na watalii na shughuli za kitalii. Hii ni kazi ngumu kutokana na vizingiti vilivyowekwa na UVIKO-19, na sasa vita kati ya Urusi na Ukraine.

Kazi nyingine inayomkabili Dk. Chana ni ya kuiokoa Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro (NCA), na Pori Tengefu la Loliondo.

Japo kazi hii inaonekana ngumu, uzuri wake ni kwamba inazo baraka zote za Amiri Jeshi Mkuu na Mhifadhi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan. Rais amekwisha kusema bayana kuwa ni wakati wa kuamua, ama Ngorongoro ibaki, au ife. Ni wazi hakuna ambaye angependa kuona ikifa.

Kinachoonekana kutatiza Ngorongoro ni kasi ndogo za mamlaka za nchi katika kumaliza kadhia hii ili wananchi mamia kwa maelfu walio tayari kuhama, wapate fursa hiyo.

Kwa upande wa Loliondo tafiti zote za kisayansi zimekwisha kuainisha umuhimu wa kuhifadhi eneo la kilometa za mraba 1,500 kati ya kilometa za mraba 4,000. Madai ya kwamba serikali inawapoka wananchi eneo lao si ya kweli kwa sababu eneo lote hili ni mali ya serikali, na sasa imeamua kuachia kwa wananchi kilometa za mraba 2,500 ili wazitumie kwa kilimo, uhifadhi na shughuli nyingine za kibinadamu.

Kilometa za mraba 1,500 ni muhimu kwa sababu ndipo mazalia ya wanyamapori, ndipo kwenye vyanzo vya maji asilimia 50 yanayoitunza Serengeti, na ndipo kwenye njia ya wanyamapori walio kwenye mzunguko wa ikolojia ya Serengeti – Maasai Mara.

Dk. Chana hatakuwa na kazi ngumu endapo mamlaka za uteuzi zitakuwa zimeamua hii kazi ifanywe na kukamilika ndani ya muda mfupi ili Watanzania waendelee kujadili masuala mengine ya kimaendeleo.

Pia waziri huyu anakabiliwa na kazi kubwa ya ulinzi wa rasilimali wanyamapori na misitu kutokana na wimbi kubwa la ujangili na athari zinazotokana na ongezeko la idadi ya watu na mifugo.

Ukataji misitu ili kuchoma mkaa umekuwa mwiba mchungu kwenye uhifadhi, lakini pia uvamizi wa vyanzo vya maji na maeneo oevu kama Kilombero ni mambo yanayompasa asimame kidete bila kuyumba. Zaidi ya yote, akifanya kazi kwa haki na kwa weledi, hii wizara ataimudu pasi na shaka.

Wasifu wa Dk. Pindi Chana

*Mwaka 2013 Dk. Chana alipata Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu Mzumbe

*Mwaka 2003 alihitimu Shahada ya Uzamili (LL.M) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

*Alipata Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B) mwaka 1991 katika Chuo Kikuu cha Lumumba, Moscow nchini Russia

*Mwaka 1993 Dk. Chana alihitimu Kidato cha Sita SHYCOM, Shinyanga

*Kidato cha Nne alihitimu mwaka 1991 Shule ya Sekondari Kigurunyembe, Morogoro

Ajira

Dk. Chana amefanya kazi Tanzania Research Education and Environmental Care kama Mwanasheria kati ya mwaka 2000 hadi 2010; pia amewahi kufanya kazi Manispaa ya Iringa kama Mwanasheria kabla ya hapo, mwaka 1997 hadi 1999 alikuwa sekretari wa Law Firm ya Uingereza.

Dk. Chana amewahi kufanya kazi Barclays Bank, UK (1995 – 1998); Coca Cola (1996 – 1997).

Uzoefu Kisiasa

Ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2005 – 2010; kisha 2020 hadi sasa.

Mjumbe wa Baraza la MUHAS (2008 – 2013)

Mjumbe wa Baraza la Mwalimu Nyerere Memorial Academy (2009 – 2010)

Balozi wa Tanzania nchini Kenya (2017 – 2020)

Mwenyekiti SADC Heads of Mission, Nairobi Chapter (2019 – 2020)

Mwakilishi wa Kudumu wa UN HABITAT, Kenya (2017) 

Katibu Uhusiano Kimataifa wa CCM (2016)

Mjumbe wa Baraza wa Mbeya University of Science and Technology (2012 – 2013)

Mjumbe wa BASATA (2009 -2013)

By Jamhuri