Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Pwani

Jamii mkoani Pwani ,imeaswa kujenga tabia ya kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao ngazi ya shule za awali hadi msingi ,ili kuwajengea uwezo wa kujua Kusoma ,Kuandika na Kuhesabu .

Hatua hiyo ,itasaidia kupunguza changamoto ya watoto kufeli elimu ya msingi kwa kutojua KKK.

Akielezea mikakati ya mkoa kuinua ufaulu kwa mwaka 2023 pamoja na utekelezaji wa Mradi wa Shule Bora uliofikia mwaka mmoja tangu uzinduliwe April mwaka 2022, Ofisa elimu Mkoa wa Pwani, Sara Mlaki anasema ,anaamini changamoto zinazosababisha kushuka kwa ufaulu zitapungua ama zitakwisha na kubaki historia.

“Moja ya sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika elimu ya msingi ,ilikuwa ni baadhi ya wanafunzi Kumaliza wakiwa hawajui Kusoma, Kuandika na Kuhesabu hasa wale wanaohamia shule za mkoa wetu wakiwa hawajui KKK” anasema.

Sababu nyingine ni baadhi ya walimu kutotimiza majukumu yao katika ufundishaji kama vile kutokuwa na maazimio ya kazi,maandalio ya somo,nukuu za somo,zana za kufundishia na utoro kazini na udhaifu wa usimamizi na ufuatiliaji kwa baadhi ya maafisa elimu kata hali inayochangia ufundishaji na ujifunzaji kuwa wa kiwango cha chini.

Sara anafafanua pia ,baadhi ya shule kukabiliwa na msongamano wa wanafunzi hali inayosababisha tendo la ufundishaji kuwa gumu .

Anaeleza ,hizo ni kati ya changamoto zilizosababisha kiwango cha ufaulu kwa mwaka 2022 kimeshuka kwa asilimia 83.162 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2021 ambao ulikuwa ni asilimia 84.91 .

Sara anaeleza, mradi wa Shule Bora tangu umezinduliwa Kitaifa na Kimataifa katika shule ya msingi Mkoani iliyopo Mkoa wa Pwani, umekuwa mkombozi kwani umeboresha Mazingira ya ufundishaji kwa walimu na kuboresha elimu jumuishi kwa makundi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum , kuboresha ufunzwaji kwa wanafunzi.

Anasema,mradi huo unakusudia kuondoa changamoto zinazowakabili watoto kushindwa kusoma, kuandika na kuhesabu, kuondoa tatizo la utoro na utawapa fursa watoto wenye mahitaji maalumu katika kuendelea na elimu ya sekondari .

Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Ofisa Elimu msingi Halmashauri ya Mji Kibaha,Bernadina Kahabuka anasema ,shule zilizo katika mradi ni 44 , wanaishukuru Serikali kwani tatizo la utoro na kutokujua KKK linapungua mashuleni.

Anaeleza, ndani ya mwaka mmoja wa Mradi huo , awali wazazi walikuwa hawashirikishwi hivyo kusababisha mahudhurio Kuwa madogo kwa wanafunzi,kwasasa mahudhurio ni mazuri.

Nae Mwanafunzi wa shule ya msingi Mkoani,darasa la Saba Ramadhani Juma anasema,anajivunia Mradi huo kuzinduliwa shuleni hapo,na kwa hakika umeboresha elimu na anaamini tatizo la kushindwa Kusoma Kuandika na Kuhesabu kwa wanafunzi kuanzia awali, hadi darasa la Saba itabaki historia.

Katika Halmashauri ya Chalinze, Ofisa Elimu Awali na Msingi Chalinze Miriam Kihiyo, anaeleza,kwasasa wanakabiliana na changamoto ya wazazi kuwa na mwamko wa elimu ya watoto wao kwani ndio changamoto kubwa.

“Kwa Chalinze Shule Bora iko kwa shule zote za Serikali 108, mradi umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa Shule zote zinatekeleza yale yote yaliyoelekezwa ikiwemo Ufundishaji wa KKK, Utengenezaji wa zana, Utoaji wa Chakula shuleni na Uanzishaji wa Ushirikiano wa Wazazi na Walimu UWaWa .

Akichangia makala hii fupi ,anaeleza Utoro wa Wanafunzi unapungua kwa kiasi kikubwa ambapo Usalama wa Mtoto unasisitizwa kwa Wazazi na Walimu na jamii kwa ujumla.

Pamoja na hayo Kihiyo anabainisha,Halmashauri hiyo imetoa mafunzo ya kujenga ujuzi wa kuibua hadithi za mafanikio katika ufundishaji na ujifunzaji kwa Walimu wa Shule za Msingi .

Kwa upande wake ,Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, anahimiza wazazi wapewe elimu kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wao na walimu wasichoke kuongea na watoto kuhusu athari ya kufeli .
“Tuendelee kutoa elimu ya malezi kwa watoto na wazazi waendelee kupewa elimu ya kuthamini elimu kwa watoto wao bila kuchoka” mkoa huu una tamaduni zake ,kutokana na hilo tuongee na wazazi bila kuchoka hadi watakapobadilika “

Kuhusu lishe ,anahimiza elimu itolewe kuhusu lishe kwa manufaa ya watoto na vizazi vijavyo.

Vilevile Kunenge anahamasisha jamii kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi ili kupambana na changamoto ya mahudhurio ya wanafunzi shuleni, kuboresha Mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa Halmashauri kuweka kwenye bajeti fedha za ujenzi wa miundombinu.

Mkuu huyo wa mkoa,anasisitiza mkoa utasimamia utekelezaji wa mikakati inayopangwa ili kuinua kiwango Cha ufaulu na kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo.

Tarehe 4 april mwaka 2022,” Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza ilizindua mpango wa elimu bunifu wa shule bora wenye thamani ya Shilingi bilioni 271 ,utakaosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia, ujumuishi na usalama kwa wasichana na wavulana katika shule za msingi nchini.

Katika Uzinduzi huo, alikuwepo Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika,Latini Amerika na Caribean, Vicky Ford ambae anasema mradi huo utawanufaisha wanafunzi milioni nne katika mikoa hiyo hususani watoto wa Kike, wenye mahitaji maalum na wale wanaotoka kwenye mazingira magumu na hatarishi.

Mradi wa Shule Bora,unatekelezwa kwa msaada wa Serikali ya watu wa Uingereza “UKaid” wakishirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) ,katika mikoa Tisa ya Tanzania Bara ikiwemo Pwani, Tanga,Dodoma, Singida, Kigoma, Katavi, Simiyu, Mara na Rukwa.

By Jamhuri