Zanzibar

Na Mwandishi Wetu

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua nembo na tarehe ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Uzinduzi huo ulifanyika Aprili 8, mwaka huu katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar ambapo Rais alitangaza kuwa itafanyika Agosti 23, mwaka huu kwa maeneo yote Tanzania.

Rais amewataka viongozi wa dini na wengine kuwaelimisha Watanzania ili kuondoa vikwazo vya kimila vinavyoweza kukwamisha shughuli hiyo.

Sensa ya mwaka huu itakuwa ya tano kufanyika tangu nchi ipate uhuru na itahusu matumizi ya dijitali, tofauti na nyingine zilizowahi kufanyika.

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Kitaifa, Kassim Majaliwa, amesema hii ni shughuli iliyopo kisheria na kwamba inafanyika kwa mujibu wa matakwa ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussen Mwinyi, ameipongeza kamati kwa kukamilisha sensa ya majaribio iliyofanywa katika mikoa 18 nchini, ikiwamo mitano ya Zanzibar, akisema itakuwa dira ya kukamilisha kazi iliyobaki.

Rais Mwinyi amesema ni muhimu wananchi wa serikali zote mbili kuiunga mkono sense, kwani itasaidia serikali kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.

By Jamhuri