Na Bashir Yakub

  1. 1. Mjue mtu anayekuuzia. Na hapa unapaswa kujitahidi kumjua sana, wanasema kumchimba. Unaweza kumjua kwa kuuliza majirani, kupitia aliyekutambulisha kwake na namna nyingine yoyote itakayokuwezesha kumjua zaidi. Lakini pia hakikisha unajua makazi yake.
  2. 2. Onyeshwa ardhi na ijue historia ya ardhi unayotaka kununua. Hapa pia unaweza kuwatumia majirani wa ardhi unayotaka kununua, kumtumia mtu mwingine yeyote anayeijua ardhi hiyo, pia waweza kuwatumia maofisa wa Serikali za Mitaa.

Serikali za Mitaa watumie katika kujua historia ya eneo na si katika kusimamia na kuandika mikataba ya mauziano.

  1. 3. Siku ya kwanza kuonyeshwa eneo na muuzaji isikutoshe, tenga tena muda wako mwingine nenda peke yako bila muuzaji, kagua na uliza majirani na watu wengine kama wapo.

Yawezekana siku ulipokwenda na muuzaji waliogopa kukwambia jambo fulani.

Fanya hivyo mara mbili, tatu, na kadiri uwezavyo kabla ya kununua, huenda siku nyingine ukamkuta mtu mwingine kwenye eneo akidai naye ni lake.

  1. 4.  Baada ya hapo, muulize maswali muuzaji kuhusu umiliki wake, alipataje eneo hilo (kwa njia ya kununua, alirithi, alipewa zawadi nk), muulize ikiwa kuna mgogoro wowote, muulize kama ameweka rehani popote, muulize kama ana mke/mume, muulize historia ya jiografia ya eneo hilo (mafuriko, vimbunga nk), muulize na kingine chochote ambacho unahisi ni muhimu kukijua.
  2. 5. Baada ya mahojiano akuonyeshe nyaraka za umiliki. Kama naye alinunua akuonyeshe mkataba wa mauziano, kama alirithi akuonyeshe fomu namba 1 inayomtambua kama mmoja wa warithi, kama ni msimamizi wa mirathi akuonyeshe fomu namba 4 ya usimamizi wa mirathi, kama alipewa zawadi akuonyeshe hati ya zawadi (deed of gift), na kama alipewa kama fidia na serikali akuonyeshe nyaraka za fidia.
  3. 6. Juu ya hilo, japo ardhi haijasajiliwa ni vema pia kuulizia maofisa ardhi wa wilaya husika kujua ikiwa kuna mradi au mpango wowote wa mradi maeneo hayo, na mambo mengine pia.
  4. 7. Jiridhishe na mengine zaidi ambayo yatakutia wasiwasi katika huo mchakato. Hii ni kwa sababu ardhi ambayo haijasajiliwa haina maeneo rasmi ya kupitia kujiridhisha.
  5. 8. Baada ya hapo mtasaini mikataba na kwenda kwenye malipo. Isipokuwa mikataba ya ardhi ambayo haijasajiliwa haitaambatana na fomu namba 29, 30, na 35.

Aidha, ikiwa muuzaji ni mwanandoa, hakikisha huyo mwanandoa mwingine ambaye hajasaini kama muuzaji anaandaliwa na kusaini nyaraka iitwayo ridhaa ya mwanandoa.

Na kama muuzaji ni msimamizi wa mirathi hakikisha warithi wote wanasaini ridhaa ya warithi.

Malipo ni muhimu na inapendeza yakifanywa kwa njia ya benki ili kuacha alama ya ushahidi.

  1. 9. Baada ya hayo yote ununuzi halali, salama, na wa kisheria utakuwa umefanyika. Kadhalika unashauriwa kumtumia wakili katika hatua hizi zote.

Epuka Serikali za Mitaa kusimamia mkataba wako, na zaidi tunakumbusha kuwa asilimia 10 wanayoomba serikali za mitaa haipo kisheria.

By Jamhuri