MOROGORO

Na Everest Mnyele

Tumekwisha kuzungumzia kwa ujumla nini maana ya katiba thabiti na inapaswa kuwa vipi. Leo tutazame umuhimu wake kwa uchumi, ustawi na furaha ya kweli kwa wananchi; furaha (ya kweli) ikiwa ndicho kipimo cha juu kabisa cha mafanikio ya binadamu.

Tukubaliane kwamba ni matamanio kwa taifa kwa wananchi wake kuishi kwa amani, haki, kuwa na uchumi imara, ustawi na hivyo kuwa wenye furaha. 

Safari ya kufikia huko hutegemea kuwapo kwa mazingira bora, mifumo thabiti ya uendeshaji na usimamizi wa shughuli za nchi na watu wake. 

Mifumo hii haitoki hewani bali msingi wake ni kuwapo kwa (nyaraka) katiba thabiti inayotoa mwelekeo wa namna nchi ijitawale na kujiongoza. 

Katiba thabiti ina mchango wa moja kwa moja kwenye maendeleo ya uchumi, ustawi na furaha ya kweli.

Mpaka kufikia hapa naamini wengi wetu, hasa wenye dhamana ya kuongoza taifa tunafahamu umuhimu wa katiba thabiti, japo kuna wachache wanaweza wasione umuhimu. 

Nchi hii ni nzuri na inahitaji nguvu kidogo tu ya mifumo itokanayo na katiba thabiti kufikia uchumi imara, ustawi na furaha ya kweli kwa wananchi.

Kinachokosekana ni utashi wa dhati wa kisiasa, vinginevyo nchi yetu ikisimamiwa vema tunaweza kuwafikia Finland na Sweden wanaoongoza kwa kuwa na furaha duniani.

Furaha ya kweli ndicho kipimo cha juu cha mafanikio ya binadamu (unaweza kujiuliza furaha ya kweli ni ipi? Nitatoa mfano baadaye).

Kwa sababu katiba ndio msingi wa maendeleo, na kutokana na maendeleo ambayo dunia imefikia, Tanzania inapaswa kupata katiba itakayokidhi na kuweka mazingira ya kufikia haraka uchumi imara, ustawi na furaha ya kweli. 

Tujifunze kutoka kwa nchi zilizofika huko na kutengeneza katiba itakayoendana na mazingira yetu. Ni suala la kuamua tu na tunaweza. 

Ni wajibu wa viongozi na wasomi kubangua bongo kupata mwongozo na mawazo ya kutupatia katiba thabiti.

Ni namna gani katiba thabiti itatupatia uchumi thabiti, ustawi na furaha ya kweli?

Mfano; mwekezaji mwenye mtaji. Inatakiwa huyu akifika nchini apokewe na kuelekezwa kwa mujibu wa sheria na kufanikisha lengo lake bila vikwazo wala haja ya kumfahamu yeyote!

Mwishowe apate faida au hasara kulingana na umahiri wake katika kuendesha shughuli zake na si vinginevyo. 

Kwa mwananchi wa kawaida kuwepo mazingira ya kufanya shughuli na kupata kipato, chakula, kusomesha watoto, huduma za afya na kijamii bila vikwazo.

Mtumishi wa umma awekewe mazingira mazuri, awahudumie wananchi kwa upendo, mwishowe apate ujira wa kumwezesha kukidhi mahitaji yake na kufurahia kazi zake. 

Hii ni mifano ya kawaida kabisa. Makundi haya matatu hayawezi kuchangia uchumi imara, ustawi na kufikia furaha ya kweli kama mifumo ya kuendesha na kusimamia shughuli zao haitokani na katiba thabiti.

Tanzania ina viongozi na watumishi wanaofanya kazi kwa woga, si kwamba wanataka, bali kuna ‘Simba wa Yuda’ wanayemwogopa (kauli ya Rais Samia). 

Hivyo mifumo ikiwa imara, basi kila mtu atatimiza wajibu wake bila woga na kuliletea taifa mafanikio tajwa hapo juu.

Nchi ambayo wananchi wake watahakikishiwa kikatiba na kisheria kuwa haki itatendeka, na wananchi kuwa huru kufanya shughuli zao bila vikwazo, itakuwa njia nyepesi kufikia uchumi imara, ustawi na furaha ya kweli. 

Kunapokuwapo mifumo katika nchi ambayo inasimamia na kuwaongoza wananchi kutimiza wajibu wao bila vikwazo, uwezekano wa kuwa na uchumi imara, ustawi na furaha ya kweli unakuwa mkubwa, la sivyo safari kufikia mafanikio ya kweli itakuwa ndefu na ngumu. 

Tanzania tuna tatizo la mifumo ya utendaji na usimamizi. Tusidanganyane, ni ngumu kwa mwekezaji, mwananchi na mtumishi kufikia malengo yake bila kukumbana na vikwazo.

Tunahitaji kufikiri zaidi na kuona jinsi gani tutaipata mifumo imara ya kutufikisha tunakotamani.

Nilimsikiliza kwa makini Rais Samia alipozungumzia uwepo wa Simba wa Yuda. 

Sijui kama suala hapa ni nidhamu ya woga au hofu ya maisha kwa watumishi. Nalizungumzia hili kwa kuwa watumishi wa umma ndio watu muhimu katika kusimamia mifumo ya uendeshaji na usimamizi wa shughuli zote za kuifikisha nchi tunakotamani kufika. 

Kundi hili lisipokuwa imara nchi haiwezi kuwa salama. Tuanze kwa kuwa na katiba itakayoweka uwajibikaji mbele badala ya uwepo wa Simba wa Yuda. 

Tuna tatizo kwenye utumishi wa umma, tujiulize; je, watumishi wanalipwa kukidhi gharama za kawaida za maisha? Wanapata motisha na kupenda kazi? Wanatendewa haki? Na je, wana ari? Wanafurahia kazi zao? 

Viongozi wanapaswa kujiuliza maswali haya kabla hatujawa na katiba thabiti na kujenga taasisi na mifumo imara. 

Unaweza kuona kama ninakuchanganya kwa kuzungumzia watumishi wa umma na uhusiano wao na katiba thabiti; ukweli ni kwamba watumishi wa umma ndio watekelezaji wakuu wa katiba na sheria zote zinazotungwa. Hivyo hawa ni muhimu sana. 

Ifahamike kwamba kuwa mtumishi wa umma ni dhamana kubwa ambayo wananchi huwapatia wachache miongoni mwao. 

Hivyo, pamoja na kuwapo katiba thabiti na taasisi na mifumo, bila kuwa na watumishi wa umma wenye nidhamu wenye kuheshimu dhamana waliyopewa, safari yetu itabaki kuwa ndoto tu na tutakuwa na wananchi wanaolalamika siku zote. 

Watumishi wa umma kiongozi wao mkuu ni Rais. Rais Samia anatambua vema umuhimu wa kundi hili ndiyo maana amekuwa akisisitiza umuhimu wake. 

Rais ana nia njema na Tanzania, anatamani kuona amani, haki, uchumi imara na furaha ya kweli kwa Watanzania vinafikiwa. Viongozi na wasomi tushirikiane kuipata katiba thabiti kwa ajili ya uchumi imara, ustawi na furaha ya kweli. 

Sisi Watanzania tunaweza kufikia matamanio hayo kwani tuna mazingira mazuri. Tusijidanganye kwamba tumefika; bado tuna safari ndefu. Tukumbuke maneno ya Rais Samia: “Nchi hii ni yetu sote, tushirikiane kuijenga.”

By Jamhuri