Simba mfukoni mwa Morrison

DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU 

Hakika Bernard Morrison ananifurahisha kutokana na mwenendo wake wa ndani na nje ya uwanja. Mchezaji huyo wa Simba ambaye ni raia wa Ghana ana vituko, analijua soka, kisha ana akili. 

Sijui kama wengi tunamuelewa Morrison wa hizi mechi tatu. Dhidi ya Ruvu Shooting kule Mwanza, Red Arrows na Geita Gold hapa Dar es Salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. 

Ni Morrison wa tofauti na mechi nyingi za Simba.  Ndiyo. Hatuwezi kujua labda pengine tofauti yake imekuja baada ya kushinda mgogoro wake dhidi ya timu yake ya zamani ya Yanga. 

Morrison wa hizi mechi tatu alikuwa makini na msumbufu mno uwanjani dhidi ya mabeki wa timu pinzani aliokutana nao. Ndiyo. Alicheza mpira wa matokeo akapunguza mambo ya ajabu nje ya kiwanja. Sijui kama tunamuelewa.

Wiki mbili zilizopita ametoka kushinda kesi yake na Yanga. Kama kawaida yake alijirekodi video fupi akifanya mzaha kwa Yanga.

Hata hivyo, baada ya tukio hilo, kesho yake akatoa waraka mfupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram akiwashukuru Yanga kwa kila kitu akisema kila jambo lina mwanzo na mwisho wake. 

Machweo yameshaanza kujiri na mwisho wa kila kitu ni kwamba Morrison anaelekea ukingoni mwa mkataba wake pale Msimbazi. Ni hapa alipowaweka Simba katika ‘mfuko wake wa shati’.

Ile shukrani yake kwa Yanga na Kocha raia wa Ubelgiji, Luc Aymael (alitimuliwa kazi baada ya kutoa maneno ya kashfa) aliyependekeza asajiliwe klabuni hapo ina maana kubwa. Kwamba, shukrani hiyo hajaitoa kwa bahati mbaya kwa Yanga. Lakini ubora wake na Simba kwa hivi sasa ndiyo una maana kubwa zaidi. 

Hadi kufikia Januari, mwakani, Morrison ataanza kusikiliza ofa ya timu zinazohitaji huduma yake. Ndiyo na tusije tukashangaa akahama Simba na kwenda katika timu nyingine endapo kama ofa nono itamjia mikononi mwake! Hakuna anayeijua kesho!  

Ni hapa anapojitenga na akili za wachezaji wetu wengi wa hapa nchini wanaokuwa na kazi mbili katika timu zetu; kwanza, wachezaji, pili, wanajipa kazi ya ushabiki.

Hawa wachezaji kutoka nchi za Afrika Magharibi hawako hivi. Morrison hana mapenzi hayo na Simba, Yanga wala Azam FC. Kwanza, hajazaliwa katika vitanda vyetu vya hospitali za Mwananyamala, Amana, Mloganzila wala Muhimbili. Amezaliwa Ghana vijijini. 

Morrison ni mfanyabiashara. Umewahi kusikia stori yake na yule Injinia Hersi wa Yanga kuhusu kukataa dau la usajili pindi aliposajiliwa na kutaka kulipwa mshahara tu kisa hakucheza mpira kwa muda wa miezi sita kwa kuwa alikosa timu ya kumsajili? Ingekuwa mchezaji wa Kitanzania hadi leo Morrison angekuwa mlipa fadhila wa Yanga lakini kwake stori ni tofauti.

Simba walipokuja na dau nono akasahau kila kitu kuhusu Injinia Hersi na sasa ni staa wao mkubwa pale Msimbazi.

Haya ndiyo maisha ya wacheza soka wa Afrika Magharibi. Huwa hawana adui wa kudumu wala rafiki wa kudumu. Wanaishi na wewe kwa sababu. Hawaishi kijamaa.

Wachezaji wengi wa Kitanzania wamekufa maskini, wengine tuko nao mitaani wanaishi katika tope zito la ugumu wa maisha. Kwanini? Kwa sababu tu walijigeuza mashabiki wa timu hizi. 

Huko aliko bosi wa Simba atakuwa anajikuna kichwa kuhusu mkataba mpya wa Morrison. Ingekuwa staa wa Kitanzania, hawa kina Barbara vichwa visingewauma pia wala wasingejipa sana muda wa kuwaza.

Katika muda ambao Simba inajitafuta kiwanjani, ghafla Morrison amegeuka kuwa staa wa timu. Kinachotokea sasa, tukutane Mei.

Shukrani yake kwa Yanga inakwenda kusafisha kila kilichopita. Unadhani kuna shabiki au mwanachama wa Yanga asiyetamani kumuona tena Morrison Jangwani? Sidhani kama kuna mtu huyu.

Ndani ya Tanzania, pengine Morrison hana ndugu wala jamaa. Amekuja kama walivyokuja mastaa wengine kutoka nje, ambao baadaye wanarudi makwao. Usishangae Morrison kurudi Yanga. 

Kuna baadhi ya mastaa wetu walipozichukia hizi timu kubwa baada ya kutoka wamezichukia moja kwa moja. Hawakuwa na muda wa kugeuka nyuma.

Lakini Morrison huyu juu ya ‘upuuzi’ wake anajua kuna kesho haitabiriki wala haijulikani kitatokea kitu gani.