Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga amesema Serikali kupitia Shirika hilo inatarajia kujenga minara 54 kwenye Kata 104 na vijiji huku wakiendelea kutoa huduma hiyo kwa Kata 130 na kueleza kuwa huduma hiyo itaboresha mawasiliano na kuwa kichocheo kiuchumi.

Mkurugenzi huyo ameeleza hayo leo Mei 13,2023 mara baada ya hafla ya makubaliabo ya kutia saini mikataba ya kupeleka huduma ya mawasiliano vijijini baina ya UCSAF na watoa huduma za mawasiliano iliyofanyika Jijini hapa.

Amesema katika minara hiyo Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) walishinda zabuni katika kata 104 na watajenga minara 104, Vodacom Tanzania amelishinda kata 190 watajenga minara 190, Airtel Tanzania walishinda kata 161 na watajenga minara 168 , Tigo walishinda zabuni katika kata 244 na watajenga minara 262 na Haloteli walishinda zabuni katika kata 34 na watajenga minara 34.

Katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Shirika limeingia makubaliano na Shirika la Posta kwa ajili ya kutoa huduma za uwakala mkuu wa T-PESA, usambazaji wa vocha na usajili wa wateja wapya wa TTCL.

Amesema huduma za TTCL zinapatikana kila palipo na ofisi za Shirika la Posta na kuendelea kufanya maboresho ili
kuhakikisha huduma linazotoa zinakidhi viwango kwa kuboresha mitambo na kuongeza vituo vya huduma kwa wateja.

Kwa upande wa huduma kwa wateja amesema maboresho yaliyofanyika ni pamoja na kuhakikisha kituo cha huduma kwa wateja (call center) kinakuwa thabiti na kupatikana ndani ya muda stahiki;

” T-PESA imeanzisha namba maalum ya kupiga bure (toll free number)0800 110095 kwa ajili ya kuwahudumia Mawakala wake ili kupunguza msongama na kuchelewesha kupata huduma kwa wakati na kuongeza vituo vya huduma kwa wateja (customer service centers) katika mikoa na wilaya ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kote nchini kwa ukaribu zaidi,”amesema.

Sambamba na hayo amesema shirika linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kutumia huduma ya mawasiliano na kutoa
huduma ya njia ya mawasiliano (capacity service) na huduma ya maunganisho (interconnect) nje ya nchi na kufanikiwa kutanua wigo wa huduma kwa wateja ambao ni Airtel Malawi, Bharti Airtel ya Uingereza, MTN Global, Apelby na AT&T ya Marekani na kwamba Juhudi zinaendelea ili kupata wateja wapya.

Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF Justina Mashiba amesema katika kuhakikisha wanafikisha huduma ya mawasiliano vijijini wanaenda kujenga minara 758 katika kata 713.

Amesema katika mkataba huo wanaenda kuongea nguvu katika minara 304 ambayo ilikuwa inatoa huduma ya 2G sasa itaanza kutoa huduma kwa 3G na maeneo mengine 4G.

“Lengo kubwa la kuanzisha UCSAF ni kupeleka mawasiliano maeneo ya vijijini na kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya mawasiliano bila vikwazo ambapo katika kuhakikisha hilo hadi sasa tumeshajenga minara nchi nzima .

Aliongeza kuwa :”USCAF Imepeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za umma ambapo hadi sasa tumepeleka katika shule 4750.pia tunaendelea na mradi wa tiba mtandao lengo ni kuhakikisha watanzania wanapata huduma bila kwenda Hospitali.

By Jamhuri