Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanikiwa kumuua fisi aliyeua watu wawili na kujeruhi watano (5) katika Wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi.

Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Kusini Mashariki, Abraham S. Jullu amesema mnamo tarehe 11 Mei, 2023 majira ya Saa kumi na mbili asubuhi Ofisi yake ilipokea simu kutoka kwa Mtendaji wa Kata ya Milola akitoa taarifa kuwa fisi amejeruhi watu watatu (3) katika Kijiji Cha Rutamba, watu wawili (2) Kijiji Cha Ng’apa na kusababisha vifo vya watu wawili (2).

Amewataja waliojeruhiwa na fisi huyo kuwa ni Suleman Mtambo, Hadija Said, Alpha Ibrahimu, Maria Sabuni na mwingine aliyetambulika Kwa jina moja (Steven) ambao wote walipelekwa Hospitali ya Sokoine Mkoani Lindi huku waliofariki walitambulika Kuwa ni Abilahi Pokosoi (50), na Saidi Makolela (75).

Kamanda Jullu amesema baada ya kupokea taarifa hiyo mara moja alituma kikosi cha Askari wapatao watano kwaajili ya kumsaka fisi huyo ambapo baada ya msako mkali majira ya mchana Askari hao walifanikiwa kumuona na kumuua.

Aidha, Kamanda Jullu amesema taratibu za kuwasaka fisi wengine katika maeneo mbalimbali ikiwemo Milola na Vijiji vya Wilaya ya Ruangwa zinaendelea na kuona namna bora ya kuwahamisha na kuwapeleka maeneo ya hifadhi.

Hata hivyo, TAWA inatoa pole kwa wahanga wa tukio hili na inatoa rai kwa wananchi wote kutoa taarifa mapema pale wanapowaona Wanyamapori Wakali na Waharibifu katika maeneo yao ili kuwawezesha Askari kuchukua hatua za kuwadhibiti mapema kabla hawajasababisha madhara kwa maisha ya watu na mali zao.

Vilevile, wananchi wanasisitizwa kuchukua tahadhari ikiwemo kuepuka kutembea nyakati za alfajiri na usiku, na kutofanya shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na ufugaji pembezoni mwa hifadhi na maeneo ya mapito (Shoroba) ya wanyamapori

By Jamhuri