*Wabunge wakataa ripoti ya kitaalamu, wainyoshea kidole Barrick

*Wananchi nao wawashangaa wabunge, JAMHURI labaini hali tofauti 

TARIME

Na Paul Mayunga

Wakati baadhi ya wabunge wakiikosoa na kuitilia shaka ripoti iliyotolewa wiki iliyopita na serikali, wananchi wa vijiji vilivyopo ukingoni mwa mto huo nao wanawashangaa wabunge.

Ripoti ya kitaalamu iliyowasilishwa bungeni na timu ya uchunguzi iliyoundwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Selemani Jafo, ilipingwa vikali na wabunge.

Timu ya uchunguzi chini ya Profesa Samwel Manyele, ilibaini kuwa chanzo cha vifo vya samaki ndani ya Mto Mara, pamoja na mambo mengine kadhaa, ni uozo wa mimea na wanyama, huku sampuli kadhaa zilizochunguzwa zikionyesha kuwapo kwa chembechembe za mercury (zebaki).

Ripoti ilidai kuwapo kwa tope chafu chini ya mto na mafuta juu ya maji yaliyotokana na uozo wa mimea, hivyo kusababisha upungufu wa oksijeni kwenye maji, hivyo samaki kufa.

Mbali na Profesa Manyele wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Samwel Mafwega (Katibu ), wajumbe walikuwa Dk. Kessy Kitulya, Dk. Charles Kasanzu, Daniel Ndio (Mkurugenzi wa Udhibiti Kemikali) na Renatus Shinhu (Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bonde la Ziwa Victoria).

Wengine ni Baraka Sekadende (Mkurugenzi wa Tafiri Mwanza), Dk. Neduroto Mollel (TPHPA), ofisa kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Yusuph Gobekuwanya (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara) na Faraja Ngengeza (Mkurugenzi Msaidizi Baionuai Ofisi ya Makamu wa Rais).

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa tatizo hilo liliviathiri vijiji vinavyopakana au kuutumia Mto Mara vilivyopo wilaya za Butiama na Rorya na si vijiji vya wilaya za Serengeti na Tarime.

Mto Mara ambao unaanzia nchini Kenya, unapita kwanza katika wilaya za Serengeti na Tarime kabla ya kuelekea Rorya, Butiama na kumwaga maji Ziwa Victoria.

Akizungumza na JAMHURI, mkazi wa Kijiji cha Nyiboko, Samweli Kitome, anathibitisha kutokuwapo kwa athari katika kijiji hicho kilichopo Kisaka, Serengeti.

“Hapa na Tarime tunatenganishwa na Mto Mara, hasa Nyamongo. Hatujaona samaki wakifa wala maji kuchafuka. Lakini ukweli tulipata hofu pia,” amesema Kitome.

Hofu iliongezeka baada ya kuzagaa kwa taarifa kuwa kuna maji machafu (yenye sumu) yamemwagwa mtoni kutoka Mgodi wa Barrick North Mara unaopakana na Kata ya Kisaka.

Kauli ya Kitome inafanana na ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Iseresere, Majimoto wilayani Serengeti, Chacha Ng’ombe, akisema upande wao ambao ndiko maji hupita kwanza kabla ya kuelekea Butiama, hawakuathirika.

“Kama chanzo cha uchafuzi wa mto kingekuwa mgodini, lazima tungekuwa miongoni mwa waathirika. Sawa, uchunguzi unaweza kufanywa kama wabunge wanavyosema lakini sijui watakuja na majibu gani tofauti,” amesema.

Wananchi wa Nyangoto na Matongo, Tarime, nao wanawashangaa wabunge wanaotilia shaka uadilifu wa timu ya Manyele, wakisema kwa nyakati tofauti: “Tatizo lingeanzia mgodini, sisi tungekuwa wa kwanza kupiga kelele. Ndivyo ilivyo siku zote, lakini si safari hii.”

Kwa upande mwingine, waathirika wa uchafuzi wa Mto Mara wanakiri kukutana na wajumbe wa timu ya uchunguzi waliowatembelea na kuzungumza nao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Wegero, Butiama, Silasi Magesa, amesema wameshuhudia samaki wakifa na wananchi kuathirika kwa magonjwa ya tumbo. 

“Sina uthibitisho wa moja kwa moja kama chanzo ni maji na hatuelewi kilitokea nini hasa maana kama maji yangekuwa yanatoka mgodini, Tarime na Serengeti wangeanza kuathirika na huenda wangeathirika zaidi,” amesema.

Hakutaka kuzungumza kwa kina kuhusu uwezekano wa chembechembe za zebaki kuwapo kwenye sampuli zilizochukuliwa na timu ya Manyele kuwa zimetokana na matumizi ya kemikali hiyo yanayofanywa na wachimbaji wadogo waliopo eneo lake, akisema uchimbaji mkubwa upo Wilaya ya Serengeti.

JAMHURI linafahamu kwamba tatizo la samaki kuonekana wakielea baada ya kufa lilianza kuonekana maeneo ya Marasibora, Kwibose, Kuruya na Kirumi.

“Utafiti wa kwanza ulibaini kuwa mafuta mazito yamemwagwa mtoni. Kama hivyo ndivyo ilivyokuwa, basi ni huko huko Butiama na Rorya. Mgodi wa North Mara uko mbali sana.

“Mimi nawashangaa waheshimiwa kuikataa taarifa ile wakati kwa sasa sisi huku tatizo ni kama limekwisha na watu wanakula samaki na kutumia maji kama kawaida,” anasema Thomas Joseph, mkazi wa Rorya.

Taarifa kutoka ndani ya timu

Mjumbe mmoja wa timu ya uchunguzi ameliambia JAMHURI kuwa walitumia helikopta kuzunguka maeneo yote na kuchukua sampuli za maji yakiwamo yanayotoka mgodini.

“Upande wa mgodini tulikuta wananchi wanayatumia maji pamoja na mifugo yao. Kirumi kuna maingiliano ya maji, yapo yanayotoka Tarime na yanayotoka Wegero. Hapo pia tulichukua sampuli na maji yalionekana kuwa machafu hata kwa macho.

“Kuna maeneo tulikuta watu wanaishi wakijijengea himaya katikati ya magugu maji wakiwa na mifugo, hasa kondoo na mbuzi wengi sana. Hapo ni majini,” anasema mjumbe wa timu (jina tunalihifadhi).

Ni maeneo kama haya ambayo uchunguzi wa Profesa Manyele, mtaalamu aliyewahi kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali, unaonyesha kusababisha uozo (decomposition) wa mimea na wanyama ulioleta tatizo la mto kuchafuka hasa baada ya kukosekana kwa mvua ambayo ingeusafisha.

Taarifa ya Profesa Manyele inasema kiwango kikubwa cha kinyesi cha mifugo, mkojo na uozo wa mimea vamizi kama magugu maji na matete ndani ya mto vimesababisha kupungua kwa oksijeni kwenye maji na kubadili rangi yake pamoja na kutoa harufu kali. 

Utafiti ulibaini kuwapo kwa zaidi ya tani milioni 1.8 ya kinyesi; lita bilioni 1.5 za mkojo uliotokana na ng’ombe zaidi ya 300,000 walioko katika eneo hilo oevu la Mto Mara kwa zaidi ya miezi minane.

Ng’ombe mmoja hutoa kilo 25 za kinyesi na mkojo lita 21 kwa siku.

Kutoka Mgodi wa North Mara

Mgodi wa North Mara upo zaidi ya kilometa 80 kutoka maeneo yaliyoathiriwa na uchafuzi mtoni na wananchi wanasema kama ni madhara, basi yangeanzia maeneo jirani.

Tangu  mwaka 2019 mgodi huu unaendeshwa kwa ubia kati ya wawekezaji na serikali chini ya Kampuni ya Twiga Minerals Corporation.

“Kwa hiyo ni mali ya umma. Kuna maofisa wa serikali hapa. Maana yake haiwezekani kufanya vitendo kinyume cha sheria kama kutumia kemikali haramu kama zebaki au kuchafua mazingira,” amesema ofisa mmoja wa North Mara.

Amesema si sahihi hata kuidhania kampuni hiyo kuchafua mto, kwa kuwa huo ni sawa na uhujumu uchumi, na kwamba maji machafu hudhibitiwa kitaalamu.

“Tupo tayari kupokea wachunguzi na kuwapa ushirikiano ili ukweli ujulikane,” amesema huku akisikitishwa na kauli ya kuhongwa kwa timu ya uchunguzi.

Taarifa iliyotolewa na Menaja wa Barrick nchini, Georgia Mutagahywa, siku chache baada ya taarifa za kuchafuka kwa Mto Mara (nakala tunayo), inaweka wazi kuwa zebaki si sehemu ya vitendanishi vinavyotumiwa na mgodi huo.

Amesema Mamlaka ya Bonde la Maji ya Ziwa Victoria huukagua mgodi na kuchukua sampuli za maji mgodini na maeneo jirani.

By Jamhuri