Ripoti ya mwaka wa fedha wa 2020/2021 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, imeibua madudu mengi katika maeneo ya kiutendaji serikalini.

Mathalani kupitia ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni Aprili 12, 2022 imebainika kuwa mamlaka 24 za serikali za mitaa zilitumia Sh milioni 664 katika matumizi yasiyo na manufaa. 

Mamlaka 61 za serikali za mitaa nazo ziliagiza na kulipa Sh bilioni 8.44 kwa ajili ya bidhaa/huduma ambazo hazikupokewa kutoka kwa wazabuni kwa muda wa hadi kufikia miezi 24 na mamlaka 64 hazikuwa na hati za malipo na viambatisho vya matumizi ya thamani ya Sh bilioni 3.87.

Pia halmashauri tano zililipa Sh milioni 376.48 kwa wafanyabiashara mbalimbali na walipatiwa risiti za EFD za kughushi, ikimaanisha kuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh milioni 57.43 haikuwasilishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Huku halmashauri 71 ziliwalipa wafanyabiashara Sh bilioni 6.07 bila kudai risiti za EFD na 24 hazikukata kodi ya zuio kiasi cha Sh milioni 338.06 kutoka katika malipo ya wafanyabiashara.

Si hivyo tu, ripoti hiyo pia inasema mapitio katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) yalibaini kulikuwa na malipo ya awali ya Sh bilioni 14.89 kwa wazabuni bila mikataba na ushahidi wa upokeaji wa bidhaa.

Mbali na hayo, ripoti hiyo inasema katika mapitio yake, CAG amebaini kuwa katika rejista ya malalamiko ya wateja kwa kipindi cha miaka mitatu – kuanzia mwaka wa fedha wa 2018/2019 hadi mwaka wa fedha wa 2020/2021 mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira inayotunzwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ina jumla ya malalamiko 228 yanayohusiana na ankara. 

Pia mapitio yake ya uendeshaji wa mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira za Dar es Salaam, Dodoma na Mbeya yamebaini kuwa zilitoza ankara kwa baadhi ya wateja wao kutokana na makadirio badala ya maji halisi yaliyotumika.

Kwa mfano, katika Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), CAG, amegundua kuwa wateja 1,207 wa jumla ya Sh bilioni 3.7 walitozwa ankara kwa kukadiriwa kwa mwaka bila ya usomaji wa mita, hali inayoweza kusababisha utozaji wa chini au juu kwa wateja. 

Vilevile katika Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya, amebaini wateja 402 walitozwa Sh milioni 79 kwa bei elekezi ya kukadiria bila usomaji wa mita kwa mwaka mzima.

Pia katika Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Namtumbo, amebaini kuwa jumla ya wateja 1,168 (sawa na asilimia 62 ya wateja wote) walilipishwa Sh 4,500 kwa mwezi (sawa na Sh milioni 63 kwa mwaka) bila kuzingatia usomaji wa mita.

Pamoja na mambo mengine, hiyo ni mifano michache miongoni mwa mingi ya madudu yaliyoibuliwa na CAG na sisi Gazeti la JAMHURI tunasema huu ni wakati mwafaka sasa wa serikali kuwashughulikia mchwa wote waliotajwa katika ripoti hiyo kwa mujibu wa sheria.

Tunashauri sasa isiwe ni mazoea tu kwamba inasomwa halafu watendaji wachache wanaondolewa katika nafasi zao kisha mwaka unaofuata ikija ripoti mpya madudu yaleyale yanajirudia.

Kwamba hapo tatizo si watendaji wanaoongoza taasisi za serikali bali kuna mtandao wa mchwa wanaotafuna fedha za umma na hao wanatakiwa watafutiwe mwarobaini wa kudumu ili kuwamaliza kabisa kwa kuwaondoa katika maeneo yao.