Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kwa kusaidiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mfaume Taka, wameendelea na sanaa yao Loliondo. Wameandika ripoti ndefu iliyojaa hadaa na kuipeleka kwa Waziri Mkuu wakitaka kumwaminisha kuwa ndio makubaliano ya wadau waliounda Kamati ya Kutatua Mgorogoro wa Loliondo.

Magazeti kadhaa yakaibuka na vichwa vya habari ‘Mgogoro wa Loliondo waisha’! Si kweli hata kidogo. Wiki hii nimeamua nipumzike na ya Loliondo. Nitaendelea nayo wiki zijazo.

Lakini itoshe tu kusema Waziri Mkuu si mtu wa mchezo-mchezo. Ni kiongozi makini na mwenye nia njema na uhifadhi. Naamini kwa kutumia vyombo vyake atabaini usanii wa ‘Team Gambo’. Hayo anayoyaita mapendelezo ya wana kamati, si ya wana kamati. Ni yake na wenzake kina Taka, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Michael Laizer; Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Nasha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro; na manabii wote wa NGOs. Ripoti anayopelekewa Waziri Mkuu ni hitimisho la kazi ambazo NGOs zilimkabidhi Gambo.

Unapoona kiongozi wa Serikali ambaye kimsingi anapaswa kuwa mtetezi wa maslahi mapana ya uhifadhi anakuwa upande wa wanaoipinga Serikali, hata kushiriki kuandaa maandamano ya kuipinga Serikali, hapo kuna jambo kubwa. Huhitaji kuwa na sifa ya PhD kujua kilichojificha nyuma ya mpango huu.  

Tuliache hilo. Leo tujadili hila zinazofanywa na Wakenya wakilenga kutuumiza kiuchumi.

Wameibuka tena kudai kufunguliwa kwa mpaka wa Bologonja ulioko mkoani Mara.

Mkakati huo unafanywa baada ya kukwama mwaka juzi licha ya juhudi kubwa zilizokuwa zikifanywa na Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Lazaro Nyalandu.

Nyalandu alifikia hatua ya kusafiri hadi Kenya na kuwahakikishia ‘watani hao wa jadi’ kuwa mpaka ungefunguliwa. Huo ulikuwa usaliti mkubwa kwa Taifa kwa kuwa sababu za kufungwa kwa mpaka huo bado zikingali hai.

Mpango huo ulikwama baada ya kufichuliwa siri hiyo kulikofanywa na gazeti hili.

Juhudi zetu zilisaidia kufutwa kwa kikao kilichoitishwa na Wizara ili ‘kubariki’ hatua hiyo yenye athari mbaya kwa uchumi wa nchi.

Mpaka wa Bologonja unaotenganisha Tanzania na Kenya, ulifungwa mwaka 1977 kwa amri ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kuzingatia maslahi mapana ya kiuchumi na kimazingira ya Taifa.

Mei 2, mwaka juzi, Deogratias Mdamu, kwa niaba ya Katibu Mkuu, aliwaandikia barua wadau kadhaa wa utalii akiwapa taarifa ya kikao kilichokuwa kimepangwa kufanyika Mei 7, katika Wizara ya Maliasili na Utalii, ukumbi wa Selous, ghorofa ya nne kuanzia saa 3:30 asubuhi.

Waalikwa wakuu walikuwa ni Shirika la Hifadhi Tanzania (TANAPA), Mkurugenzi Mwendeshaji, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB); Mhifadhi Mkuu, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA); Katibu Mtendaji Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT); na Chama cha Wakala wa Utalii Tanzania (TATO).

 

Gazeti la JAMHURI baada ya kufichua mpango huo uliotajwa kuwa ni mkakati wa Nyalandu wa kuwafurahisha Wakenya, waalikwa walipigiwa simu Mei 6 na kuambiwa mkutano umeahirishwa hadi watakapopewa taarifa. Hadi leo mwaka 2017 mkutano huo ulikuwa haujaitishwa!

 

TATO wakasema wazi kuwa hawako tayari kuona mpaka huo ukifunguliwa, na wakatishia kuegesha magari yao yote endapo Nyalandu atashinikiza kufunguliwa kwa mpaka huo.

Wakasema kama Wakenya wanataka, waje washindane na Watanzania hapa hapa. Wajisajili kwenye Kituo cha Uwekezaji (TIC) kama wawekezaji, walipe kodi zote, wapambane na urasimu wote, waje washindane; lakini siyo kuwafungulia Bologonja.

Wiki iliyopita, TATO wamerejea msimamo huo huo. Imani yetu ni kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitapoteza muda kujadili jambo hili.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Aloyce Nzuki, anatajwa kuwa mmoja wa watu waliopinga mpango huo kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake. Upinzani huo unawekwa kwenye sababu zilizotumiwa na Nyalandu kushinikiza Nziku aondolewe kwenye nafasi hiyo. Bahati nzuri Serikali ya Awamu ya Tano imetambua na kuheshimu uwezo wake, na sasa ni Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kwanini tunapinga Bologonja kufunguliwa? Endapo mpango huo utafanikiwa hiyo ina maana watalii kutoka katika Mbuga ya Maasai Mara, wataingia katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kisha kurejea Kenya huku wakiiacha Tanzania na Watanzania wakiwa hawafaidi lolote la maana.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, licha ya urafiki wake wa dhati na Nyalandu, walau hili la kufunguliwa kwa Bologonja alimpinga rafiki yake.

Mwaka 1977 mpaka huo ulifungwa kutokana na uchunguzi uliothibitisha kuwa watalii kutoka Maasai Mara walikuwa wakiingia Serengeti, na wakati huo huo malipo yote ya malazi, vyakula na huduma nyingine vikifanyika upande wa Kenya. Tanzania ikabaki na jukumu la kuwaandalia Wakenya mahali pa wao kuingia na kuchuma fedha na kisha kurejea kwao wakiwa na watalii. Tanzania ikawa sehemu ya kuandaa ‘vyoo vya wageni’, lakini mapato yote makubwa yakaishia kwa Wakenya.

Akiwa Ujerumani kwenye maonesho ya utalii Machi, 2014 huu Nyalandu alisema atahakikisha Bologonja inafunguliwa. Habari hizo zilipokewa kwa shangwe na Wakenya wanaotaka wapiti hapo mpakani ili kupunguza urefu wa safari za wageni wao.

Mwaka 2009, Serikali ya Tanzania, kwa mara nyingine, ilizuia ufunguaji mpaka wa Bologonja.

Pamoja na hoja njema za kiuchumi, hoja nyingine ilikuwa kwamba kufunguliwa kwa mpaka huo kungehatarisha mazingira na huenda kuiua Hifadhi ya Taifa Serengeti, kwani watalii wengi kutoka Kenya wangeitumia njia hiyo.

TTB wakati huo ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Peter Mwenguo, ilishikilia msimamo huo na kusema kwa sababu hizo mbili- za kiuchumi na kimazingira- kamwe isingekubaliana na mnapendekezo au uamuzi wa kufunguliwa mpaka huo.

Chama cha Waongoza Watalii Kenya (KATO) kimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Bologonja inafunguliwa.

Mwaka 2009, Ezekiel Maige, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema Serikali ya Tanzania haikuwa na dhamira yoyote ya kufungua mpaka huo, na kwamba msimamo huo ulikuwa ukijulikana kwa viongozi wa Kenya.

Hifadhi ya Serengeti yenye ukubwa wa kilomita za mraba 14,763; ndiyo makao makuu ya msafara wa nyumbu zaidi ya milioni moja na pundamilia zaidi ya 200,000 wanaosafiri kati ya Hifadhi hiyo na Maasai Mara. Kati ya miezi 12, nyumbu huwapo Serengeti kwa kipindi kirefu cha miezi 10.

Hadi mwaka 2014 kulikuwa na hoteli za kitalii zisizozidi 15 ndani ya Serengeti, loji na kambi kadhaa. Hatia hiyo ya kuwa na hoteli na kambo chache inaelezwa kuwa inalenga kuepuka wingi wa watalii hifadhinin ambao unaweza kuchangia uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wa Kenya kuna hoteli na kambi za watalii zaidi ya 50 na loji tisa ndani ya Maasai Mara ambayo ukubwa wake ni kilomita za mraba 1,510 pekee.

Mwaka 2014 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilieleza hofu yake juu ya kuongezeka kwa vitendo vya kibinadamu ndani ya Hifadhi ya Serengeti vilivyosababishwa na wingi wa vituo vya kuingia na kutoka hifadhini humo. Chanzo cha wingi huo kilielezwa ni idadi ya watalii na vitendo vya kibinadamu kwenye hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya.

Baada ya Wakenya kuona wamesharibu kwao, sasa wanaitazama Tanzania kama sehemu pekee ya wao kuitumia kuwaridhisha wageni wao.

Hatuna budi kuwapongeza viongozi wetu wa wakati huo na wa sasa waliosimama imara kupinga hila hizi za Wakenya za kufunguliwa kwa Bologonja. Tunapoelekea kuwapata wabunge wetu katika Bunge la Afrika Mashariki, hatuna budi kuwapeleka watu wenye uwezo wa kusimama kidete kutetea maslahi ya nchi yetu kama baadhi yao walivyoonesha. Sharti tuwe makini katika kukabiliana na njama zote za majirani zetu za kutuumiza kiuchumi.

By Jamhuri