Aliyekuwa Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Mhanga, amefukuzwa kazi baada ya kupatikana na hatia ya kuingiza vibarua hewa kazini.

Mwaka uliopita, Gazeti la JAMHURI limechapisha kwa kina ufisadi uliokuwa unaendelea pale bandarini, ambapo ukiacha wizi wa makontena, kulikuwapo wizi wa kalamu wa kutisha bandarini.

“Hatimaye Mhanga amefukuzwa kazi baada ya Kamati Maalumu kufanya uchuguzi wa kina, ikabaini kuwa alitenda makosa makubwa kwa kuingiza vibarua hewa kazini na kupokea malipo kwa njia anazozifahamu yeye.

“Tunampongeza sana Mkurugenzi Mkuu, Injinia Deusdedit Kakoko, kwa kuwa mzalendo na kuonesha uzalendo wa hali ya juu kuitumikia nchi. Amesimamia na amedhibiti wizi hapa bandarini.

“Mhanga alitiwa hatiani kwanza kwa kosa la kukiuka taratibu za mikataba akashushwa cheo kutoka Meneja kuwa ‘Principal’, lakini aliporejea kazini siku ya Jumanne, mwezi uliopita mwanzoni akapewa tena barua ya kusimamishwa.

“Aliitwa mbele ya Kamati inayoundwa na kundi la wajuzi kutoka Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, wizarani na sehemu nyingine nyingi ambao kimsingi hawakumwonea mtu, na naamini hata Mhanga amekubali kilichotokea,” amesema mtoa habari wetu.

JAMHURI lilipowasiliana na uongozi wa TPA, kuhusiana na kufukuzwa kwa Mhanga, walikiri hilo kutokea: “Ni kweli Mhanga amefukuzwa kazi kutokana na kosa la kuingiza vibarua hewa kazini,” amesema Meneja wa Mawasiliano wa Bandari, Janeth Ruzangi.

Uongozi wa Bandari kwa kushirikiana na baadhi ya kampuni binafsi ulikuwa unaingiza vibarua hewa na kuonesha kuwa kwa siku wanaingia kazini hadi wafanyakazi 1,000.

Kutokana na wingi wa vibarua, takwimu zilikuwa zinaonesha kuwa kila vibarua 20 wanasafisha eneo lisilozidi mita tano kwa siku na walikuwa na zamu mbili zinazoonesha walikuwa wanafanya kazi hadi saa 5:00 usiku, wakati uhalisia ofisi zilikuwa zinafungwa saa 11:00 jioni.

Zamu hizo zinaoneshwa kufanywa kuanzia saa 1:00 asubuhi mpaka saa 9:00 alasiri, na zamu ya pili ni kuanzia saa 9:00 alasiri mpaka sasa 5:00 usiku.

Katika ripoti yao ilikuwa inaonesha kuwa vibarua wapatao 1,000 hufanya usafi maofisini, kufyeka majani, kusafisha mifereji na karakana ya Bandari.

Baada ya JAMHURI kuchapisha taarifa hizi, Machi 15, 2016 Mhanga aliwaamuru viongozi wa Baga Investment Co. Ltd kumpelekea nyaraka inayotumiwa kupeleka vibarua bandarini, ikiwa na majina ya vibarua na namba zao za simu (Take-on) pamoja na nyaraka nyingine za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ambazo zilifikishwa ofisini kwake saa tatu usiku.

Machi 16, 2016 vibarua zaidi ya 200 walisimamishwa kazi kutokana na kuhofia mbinu zao za uchotaji wa fedha za umma kugundulika.

Pamoja na kupunguza vibarua hao, bado Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari iliendelea kulipa vibarua hewa hasa kwa wale wanaofanya kazi shifti ya pili wanaodaiwa kufanya kazi mpaka saa 5:00 usiku, jambo ambalo si kweli.

Ulipaji wa vibarua hewa bandarini umekuwa ni mchezo uliozoeleka miongoni mwa watendaji ambao hutumia baadhi ya kampuni zilizopewa zabuni. Vyanzo vililijulisha JAMHURI kuwa Bandari inalipa karibu Sh bilioni 2 hewa kila mwezi.

JAMHURI liliwasiliana na Kaimu Meneja wa Bandari, Mhanga, kuhusiana na taarifa hizo ikiwa ni pamoja na kuelezwa kuwa miongoni mwa wamiliki wa moja ya kampuni hizo, hakutaka kulizungumzia suala hilo zaidi ya kulitaka gazeti liwasiliane na Ruzangi. Baada ya kufukuzwa kazi, JAMHURI limemtafuta Mhanga bila mafanikio.

Mhanga anaongeza idadi ya viongozi waandamizi wa Bandari waliofukuzwa, akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha, Peter Gawile, na Meneja wa Teknohama, Phares Magessa.

2944 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!