Na Salma Lusangi, JakhuriMexia, New York

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewawezesha wanawake kupata fursa za manunuzi ya umma kwa kutoa mafunzo ya kiufundi ili kuongeza uwezo wa zabuni na matumizi bora ya mifumo ya ununuzi wa kielektroniki.

Taarifa hiyo ametoa wakati akifunga kikao cha pembeni (side Event) huko katika ukumbi wa Umoja wa Mataifa, New York, Nchini Marekani. Amesema Serikali imefanya juhudi hiyo ili kuwezesha kila raia wa Tanzania kumudu faida sawa kutokana na fursa za manunuzi, hasa zile zinazohusiana na biashara ndogo ndogo zinazoendeshwa na kumilikiwa na wanawake.

Amefahamisha kwamba jitihada hiyo inafanywa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs).

Alieleza Serikali yaTanzania inasisitiza matumizi ya mfumo wa kitaifa wa ununuzi wa kielektroniki ili kuweka mazingira mazuri ambayo pia yanaiwezesha Serikali kufuatilia idadi ya mikataba ya manunuzi inayotolewa kwa wanawake.

Pia alisema ili kuhakikisha wanawake wanawezeshwa na ujuzi mdogo wa lugha ya Kiingereza, Serikali inatayarisha na kuhakikisha nyaraka za zabuni zimeandikwa katika Lugha yetu ya Taifa (Kiswahili) ili ziweze kueleweka kwa urahisi na kunufaisha makundi maalum fursa za manunuzi.

Mhe Riziki alifahamisha kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza safari ya ubunifu wa kuendeleza Dira yake mpya ya Maendeleo 2050 itakayoendesha Ajenda ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka 25 ijayo ili kuhakikisha maono yanafafanuliwa vyema na mienendo ya kijamii na kiuchumi pamoja na mitazamo ya kijinsia, itazingatiwa.

“Safari ya ubunifu wa kuendeleza Dira yake mpya ya Maendeleo 2050 itakayoendesha Ajenda ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka 25 itasaidia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana katika mipango ya maendeleo ya kitaifa “ Alisema Pembe.

Aidha waziri huyo ametoa shukrani za pekee kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali, maafisa wa Umoja wa Mataifa, Taasisi za Utafiti na wadau wa elimu juu, sekta binafsi na vyombo vya habari kwa kufanikisha mkutano huo.

Mapema akifungua kikao hicho Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika masuala ya Wanawake na Makundi Maalum Bi Sophia Mjema alisema Tanzania Bara na Zanzibar, imeandaa sera, mikakati, mipango, na programu kadhaa za kuwawezesha wanawake na wasichana na kuhakikisha usawa wa kijinsia katika shughuli mbali mbali.

Alielezea Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003 imetaja haja ya “kuunga mkono ushirikishwaji wa wanawake katika michakato ya maendeleo ya biashara kupitia upatikanaji wa usawa zaidi wa mali za uzalishaji, hasa ardhi yenye hati miliki, miundombinu, fedha, elimu na ujuzi”.

Pia, kuongeza mafunzo na kurekebisha taratibu za uendeshaji ili kuruhusu na kukuza matumizi ya mfumo wa manunuzi ya umma; kushughulikia vikwazo vya kifedha na upatikanaji wa taarifa za manunuzi ya umma.

Mkutano wa Hadhi ya Wanawake (CSW68) ulianza tarehe 11 hadi 22 Machi 2024, New York nchini Marekani ambapo ya kikao cha pembeni kilikuwa na mada isemayo Kufadhili Usawa wa kijinsia: Kuwawezesha Wanawake na Wasichana Kupata Huduma za Umma na Kuendeleza Ahadi za Kizazi chenye Usawa nchini Tanzania.