Pamoja na kila mgombea kujitangaza mshindi katika uchaguzi wa urais nchini Gabon, hatimaye Tume ya Uchaguzi ya Gabon (CENAP) imemtangaza Rais Ali Bongo kuwa mshindi wa uchaguzi kwa kujipatia asilimia 49.85 ya kura ikilinganishwa na mpinzani wake Jean Ping aliyepata asilimia 48.16 ya kura.

Waziri wa Mambo ya ndani wa nchi hiyo, Pacome Moubelet-Boubeya, Jumatano iliyopita alitangaza matokeo ya mwisho na kubainisha kuwa Rais Bongo alikuwa ameibuka mshindi kwa kupata asilimia 49.80 ya kura dhidi ya mpinzani wake wa karibu Jean Ping aliyepata asilimia 48.23.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, upinzani ukiongozwa na Jean Ping ulitaka kura hizo kuhesabiwa upya, katika mkoa wa Haut Ogooue ambako wanahisi udanganyifu umefanywa na tume ya uchaguzi kwa kushirikiana na serikali.

Kabla ya matokeo kutangazwa, msemaji wa chama tawala cha Gabonese Democratic Party (PDG), Austin Boukoubi, alitoa wito kwa tume kuwa na matokeo ya kuaminika ili kuendelea kudumisha amani ndani ya nchi.

Wakati tume ikiwa tayari imemtangaza Ali Bongo kuwa ni mshindi, kumekuwa na ghasia nyingi zinazoendelea nchini humo, huku kukiripotiwa kutokea uharibifu mkubwa ikiwamo kuchomwa moto kwa majengo mbali mbali ya serikali likiwamo jengo la Bunge.

Baada ya matokeo ya uchaguzi, Rais Ali Bongo anasema amekulia ndani ya uongozi kwa muda wa karibu miaka 50 na kudai kuwa amekulia ndani ya utawala huo na anaufahamu vyema kwa msingi huo, yeye ni chaguo sahihi.

Amesema anafahamu ni maeneo gani yanafanya vyema ili aweze kubeba jukumu la kuleta mabadiliko nchini, kwa sababu fikra na mitazamo aliyonayo ni kuangalia jinsi ya kutatua matatizo ya wananchi wa nchi yake.

Wakati Rais Ali Bongo akitoa matamshi hayo, kiongozi wa upinzani nchini humo anadai ameshinda kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika siku wiki iliyopita, huku akimtaka Rais Ali Bongo akubali kushindwa na kuruhusu chaguo la wananchi kuheshimiwa.

Jean Ping, Mkuu wa zamani wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, anasema takwimu zilizopo zinaonesha kwamba ameshinda kiti cha urais hivyo anachotaka ni Rais Bongo akubali kwamba, ameshindwa katika uchaguzi huo.

Umoja wa Ulaya kupitia waangalizi wake wameonya kuwa matokeo ya kila kituo cha kupigia kura yanapaswa yawekwe wazi, ananukuliwa msemaji wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo, Federica Mogherini, katika taarifa yake.

Wakati hali ikiwa hivyo, raia wengi wa nchi hiyo wana hofu ya kutokea tena vurugu kama ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi wa mwaka 2009, hofu hii imetokea baada ya uchaguzi wa siku ya Jumamosi ambako wagombea wote walidai kushinda uchaguzi huo.

Nchi hiyo ambayo hivi karibuni tu imejiunga tena na Shirika la Nchi zenye kuzalisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC) baada ya kutokuwapo kwa miongo miwili, pato lake la jumla la taifa kwa kila mtu kwa mwaka ni dola 10,000 na kuifanya nchi hiyo kuwa mojawapo ya nchi tajiri kabisa barani Afrika.

By Jamhuri