Habari njema kwa wanafamilia wa ukurasa wa TUZUNGUMZE. Mwaka huu nimetoa chapisho langu la kitabu kipya. Kitabu hiki kinaitwa SIRI YA MAFANIKIO KATIKA MAISHA. Ni kitabu kilichojaa hekima, busara, ushauri na matumaini ya maisha yetu. Mpaka sasa mlango wa kupata nakala yako uko wazi. Karibuni sana wanafamilia wa ukurasa huu, Watanzania wote na wasomaji wa gazeti hili makini.

Maisha yanapokuonyesha sababu 100 za kulia, yaonyeshe kuwa una sababu 1,000 za kucheka. Maisha yanapokuonyesha sababu 99 za kuanguka, yaonyeshe sababu 100 za kuinuka. Hakuna binadamu aliyewahi kufanikiwa kiroho, kimwili, kiuchumi, kisiasa, kiuongozi bila ya kuanguka.

Katika vituo kumi na nne vya njia ya msalaba, Yesu alianguka mara tatu. Mtoto anapoanza kujifunza kutembea anaanza kwa kuanguka. Waliofanikiwa walianza kwa kuanguka, wakafanikiwa kwa kuinuka.

Unapoianza safari ya mafanikio ni lazima uanze kwa kuanguka. Ukianguka mara 10 inuka mara 11. Ukianguka mara 99 inuka mara 100. Mwanasayansi Albert Einstein anasema: “Mtu yeyote ambaye hajawahi kushindwa, huyo hajajaribu kufanya jambo jipya.”

Kupata pancha si mwisho wa safari. Biashara yako inapoyumba, usikate tamaa. Unapopata misukosuko katika maisha usikate tamaa. Ni mfu pekee ndiye mwenye haki ya kukata tamaa. Wewe ambaye bado unaishi hauna sababu za kukata tamaa bali una sababu za kushinda. Endelea kupambana mpaka kieleweke. Kesho ni nzuri kuliko jana. Yajayo yanafurahisha.

Unapopata matatizo usiyakimbie. Endelea kupambana nayo. Kulikimbia tatizo si kulitatua. Kulikimbia tatizo ni kuongeza tena idadi ya matatizo. Kulitatua tatizo ni kukabiliana nalo. Kuna askari mmoja katika taifa fulani alijumuika na wenzake kwenda vitani.

Mapambano ya kivita yalianza. Askari huyu baada ya kuona kwamba kikosi chake kinaelekea kushindwa alitoroka na kuwaacha wenzake kwenye uwanja wa mapambano. Alikwenda kujificha pangoni. Akiwa amejificha pangoni aliona sisimizi anapanda kwenye jiwe akiwa anavuta chakula. Sisimizi huyo alidondoka mara tisa, lakini mara ya kumi alifanikiwa kupanda na chakula chake.

Askari huyo aliyekuwa amejificha alishuhudia juhudi za sisimizi aliyeanguka mara tisa, lakini mara ya kumi akafanikiwa kupanda na chakula chake. Askari huyo alitoka pangoni alipokuwa amejificha na kurudi kwenye uwanja wa mapambano. Alipata somo la kutokukata tamaa kutoka kwa sisimizi. Usiyakimbie mapambano yaliyo mbele yako. Kabiliana nayo.

Acha kujiuliza maswali kwa kujilaumu. Kuna baadhi ya watu wanajiuliza maswali mengi si kwa lengo la kujifunza bali kwa lengo la kujilaumu. Kwa mfano: Kuna mtu anajiuliza: Rika langu wanaolewa, lakini mimi sijampata mchumba. Rika langu wana watoto, lakini mimi sina hata mtoto wa kusingiziwa. Rika langu wana magari, lakini mimi sina hata tairi ya baiskeli.

Rika langu ni wahehimiwa, lakini mimi ni maskini. Rika langu wamejenga nyumba za kifahari, lakini mimi bado ninaishi kwenye nyumba za upangaji. Unapojiuliza maswali ya aina hii usitazame upande mmoja tu. Kumbuka: Kuna wanarika lako ambao tayari wamezikwa, lakini bado wewe upo hai.

Kuna wanarika lako wanaumwa kansa, lakini wewe ni mzima wa afya. Kuna wanarika lako wako kwenye vituo vya walemavu, lakini wewe ni mzima. Kuna wanarika lako ni yatima. Usijiulize maswali kwa lengo la kujilaumu. Jiulize maswali kwa lengo la kujifunza. Je, unafahamu njia rahisi ya kuyabananisha maisha? Soma sehemu ya pili ya makala hii wiki ijayo.

98 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!