Na Nizar K Visram (aliyekuwa Canada)

Februari 11, mwaka huu Rais wa Marekani, Joe Biden, alitoa amri ya kutaifisha dola bilioni saba za Afghanistan zilizokuwa zimewekwa Marekani kama amana katika benki kuu. 

Alisema kati ya fedha hizo dola bilioni 3.5 zitatumika kuwafidia waathirika wa mashambulizi ya New York ya Septemba 11, 2001 (9/11). Hii ni nusu na nusu iliyobaki alisema atazitoa kwa mashirika ya ‘misaada’ yanayoshughulika nchini Afghanistan.

Hizi ni fedha zilizowekwa na Da Afghanistan Bank (Benki Kuu ya Afghanistan) katika Federal Reserve Bank jijini New York. 

Wakati huo Afghanistan ilikuwa imevamiwa na majeshi ya Marekani kwa muda wa miaka 20 hadi Agosti mwaka jana yalipotimuliwa na wapiganaji wa Taliban. 

Aliyekuwa rais, Ashraf Ghani, naye alikimbilia Dubai.

Fedha hizo hazikuwekwa na Taliban, bali na serikali ya Ghani ambayo haipo tena madarakani. Hivyo ni mali ya wananchi wa Afghanistan na zinapaswa zirudishwe kwa wenyewe, badala ya kuwapa waathirika wa 9/11 au ‘mashirika ya misaada’ kama alivyotangaza Biden.

Dola bilioni saba ni fedha chache  kwa Marekani, zinatosha kununulia ndege tatu za kivita aina ya B-2. Lakini kwa Waafghani hizo ni fedha nyingi wanazozihitaji sana kuokoa maisha ya watoto wao wanaoteseka kwa njaa. 

Mamilioni ya watoto wao wamekufa kwa kukosa chakula na matibabu.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosambaza Chakula (WFP), takriban Waafghani  23 milioni (nusu ya raia wote) wanakabiliwa na njaa kali mwaka huu. Na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linasema watoto karibu milioni moja wanaweza kufa njaa.

Haya ni matokeo ya Marekani kuivamia na kuikalia Afghanistan kwa miaka 20. Badala ya kuwafidia kwa hasara walizopata na wanazopata sasa, wanaambiwa eti fedha zao zitatumika kuwalipa waathirika wa 9/11! 

Kwa mfano, mnamo Aprili 2013 mabomu ya NATO yaliwaua watoto wa Jimbo la Kunar. Hawa wamefidiwa?

Kuanzia wakati wa utawala wa Obama hadi utawala wa Trump, idadi ya raia waliouawa kwa mabomu ya NATO iliongezeka kwa asilimia 330. Tangu mwaka 2001 zaidi ya raia 71,000 waliuawa. Hawa nao wamefidiwa? 

Na katika Gereza la Bagram ambako Waafghani waliteswa, walidhalilishwa, waliwekwa wakiwa uchi wa mnyama, nao wamefidiwa na Marekani? Haya yalifanyika katika maeneo kama Kandahar na Helmand. Hospitali ya Kunzur ilipigwa makombora.

Mei 2009 majeshi ya NATO yalishambulia Jimbo la Farah na kuwaua raia 150. Chuo Kikuu cha Brown kimekisia kuwa zaidi ya raia 46,000 wameuawa wakati majeshi ya Marekani yakiikalia Afghanistan. 

Nayo asasi ya Action on Armed Violence (AOAV) nchini Uingereza imesema raia 3,977 waliuawa kutokana na mabomu ya Marekani mwaka 2016 hadi 2020, miongoni mwao ni watoto 1,598.

Mwaka 2010 iliripotiwa kuwa askari wa Marekani waliunda kikosi cha kuua (kill team) katika Jimbo la Kandahar. Kazi yake ilikuwa kuwaua raia wa Afghanistan kisha kuwakata vidole kama ushahidi.

Je, hawa wote wamefidiwa na Marekani?

Mwaka 2020 Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) imependekeza kuwa Marekani ichunguzwe kwa uharamia wa kivita nchini Afghanistan. 

Ilisema ina ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa majeshi ya Marekani yaliua, yalitesa na yalibaka nchini Afghanistan mwaka 2003 na 2004. 

Hata hivyo ICC imeshindwa kufungua mashtaka kwa sababu Marekani imekataa kushirikiana na mahakama.  

Leo hii Benki Kuu ya Afghanistan haina fedha, kwa hiyo biashara imesimama na mishahara ya madaktari na wataalamu hailipwi. Hakuna fedha zinazoingia au kutoka nchini. 

Mzunguko wa fedha umepungua na walioweka akiba katika mabenki wamekwama. Hizo dola bilioni 3.5 ambazo Biden amesema zitatolewa kwa mashirika ya misaada itachukua muda mrefu kama ilivyoelezwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Badala yake Waafghani leo wanaambiwa na Biden eti wawafidie wanafamilia wa watu 3,000 waliokufa mjini New York. Ni mauaji ambayo Waafghani hawakuhusika nayo wala hawakujua.

Mwanaharakati wa Afghanistan, Bilal Askaryar, amesema: “Wananchi wa Afghanistan hawakuhusika kabisa na mauaji ya 9/11. Sasa anachofanya Biden ni kuwafidia waathirika wa 9/11 kwa kutumia fedha za watu maskini wanaokufa kwa njaa. Huu ni wizi.”

Si tu Biden amechukua fedha za Afghanistan bali ameiwekea nchi hiyo vikwazo ili isiweze kukopa wala kufanya biashara kimataifa.

Anachofanya Biden ni kuwaadhibu Waafghani waendelee kufa kwa sababu wanatawaliwa na Taliban, ingawa utawala huo hawakuuleta wao wala hawana uwezo nao. 

Kama Taliban leo wanatawala Afghanistan basi ni Marekani ndio waliosababisha wao kuichukua nchi hiyo baada ya utawala wa Marekani wa miaka 20.

Hoja ya Biden ni kuwa ni Osama bin Laden ndiye aliyepanga mashambulizi ya 9/11 naye alikuwa akiishi Afghanistan chini ya Taliban. Hata kama ni kweli Osama alihusika, hakuna ushahidi wowote kuwa Taliban au Waafghani walimsaidia au walijua kabla kuhusu mashambulizi hayo!

Kwanza Osama aliyepanga njama alitoka Saudi Arabia. Na wale walioshambulia New York, 15 walitoka Saudi Arabia, wawili walitoka UAE, mmoja Lebanon na mmoja Misri. Kwa nini Biden asizilaumu na nchi hizo badala ya kupora fedha za Waafghani ambao hata hawa wamezaliwa wakati huo?

Kwa vyovyote vile, fedha hizi si mali ya Taliban wala si za Osama. Hivyo kwa nini fedha za Waafghani zitumike kwa ‘kosa’ la Taliban au Osama?  Kwa nini watoto wa Afghanistan waadhibiwe kwa ugaidi wa Osama, bilionea wa Saudi Arabia ambaye alisaidiwa kwa hali na mali na CIA ili kupigana na majeshi ya Urusi (USSR) nchini Afghanistan?

Waliotajirika sana kutokana na uvamizi wa Afghanistan ni kampuni za kuunda na kuuza silaha za kivita. Kuna kampuni tano zinazoongoza nazo ni Boeing, Raytheon, Lockheed Martin, General Dynamics na Northrop Grumman. 

Siku ya Septemba 18, 2001, George W. Bush, aliyekuwa Rais wa Marekani, alitumia silaha za kampuni hizi kuishambulia Afghanistan. Wakati huo hisa zao kama zilikuwa zikiuzwa kwa dola 100 kila moja, leo hii hisa hiyo ina thamani ya dola 1,000! 

Ndiyo maana aliyekuwa ofisa wa CIA, Chalmers Johnson, alisema: “Vita ni biashara yenye faida kubwa na ndiyo maana kila kukicha tunaona vita inaongezeka.”

Naye kamanda wa jeshi la anga amesema: “Waamerika wanaopoteza watoto wao vitani wanajiuliza iwapo vita ina faida, lakini wanasiasa wanaoshirikiana na kampuni za kivita wanapiga hesabu tofauti kabisa.”  

Waathirika wa 9/11 walikwenda mahakamani miaka kama 10 iliyopita na ikaamuliwa kuwa wapiganaji wa Taliban wawalipe fidia. 

Baada ya Taliban kushika madaraka mwaka jana, mahakama ikaamua fidia hiyo sasa itokane na akiba ya Afghanistan iliyowekwa Marekani. Yaani hapo awali mlipaji alikuwa mpiganaji wa misituni Taliban, sasa ni Afghanistan, hata kama Marekani haitambui serikali ya Taliban.   

Katika mashambulizi ya 9/11, Phyllis Rodriguez alipoteza mtoto wake. Yeye alisema ni aibu kwa waathirika wa 9/11 kulipwa fedha za raia wa Afghanistan wanaoteseka kwa njaa kutokana na vikwazo vya Marekani iliyoikalia nchi hiyo kwa miaka 20.

Akaongeza kuwa kuchukua fedha za wananchi wa Afghanistan na kuwalipa waliofiwa katika 9/11 ili kuwaadhibu Taliban ni sawa na kuwaadhibu wananchi wote wa Afghanistan wasio na hatia. 

“Mwananchi wa kawaida wa Afghanistan hahusiki kwa namna yoyote na mauaji ya 9/11 lakini hata hivyo anaporwa akiba yake na utawala wa Marekani,” aliongeza Rodriguez.

Mwathirika mwingine anayepinga uamuzi wa Biden ni Barry Admunson ambaye alimpoteza nduguye katika 9/11. 

Yeye amesema: “Hatuwezi kuwarudisha ndugu zetu waliokufa, lakini tunaweza kuokoa maisha ya Waafghani kwa kutaka Biden awarudishie fedha zao.”

NGO iitwayo ‘Unfreeze Afghanistan’ nayo imetoa wito kwa asasi za kibinadamu zikatae kupokea fedha za ‘misaada’ kwa Afghanistan 

[email protected]

By Jamhuri