DAR ES SALAAM

Na Dk. Felician B. Kilahama

Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ni Alfa na Omega kwa zawadi ya uhai; si kwamba sisi ni wema kuliko waliopoteza maisha; bali ni kwa neema na rehema zake kwetu: Jina lake Mungu wetu lihimidiwe.

Pia ni vema na haki kumshukuru Mungu bila kuchoka: mshukuruni Bwana kila wakati maana fadhili zake kwetu ni za milele. 

Makala hii inahusu mabadiliko ya tabianchi, chimbuko lake na athari zake kwa maisha yetu. Tunaposema mabadiliko ya ‘tabianchi’ maana yake nini?

Je, nchi kama Tanzania inayo ‘tabia’? Au ni Watanzania wenye tabia? Je, mabadiliko ya tabianchi ni yapi na yanatokana na nini? Si rahisi kupata majibu sahihi lakini binadamu ndiye kisababishi kikubwa kutokana na harakati za kujitafutia maendeleo kiuchumi na kijamii. 

Tunaposema ‘tabianchi’ yawezekana wataalamu mbalimbali walidadisi, pengine, tangu kuumbwa kwa dunia yenye bahari iliyosheheni maji; pia kuna maziwa, mabwawa na mito mingi; wakagundua kuna tabia fulani, mathalani majira mbalimbali. 

Mfano, kuwapo joto, mvua, ukame, baridi kali mpaka ‘snow’ na barafu hasa sehemu ya kaskazini na kusini mwa dunia. 

Tanzania kuna nyakati za ‘kusi’ na kasikazi’ vielvile, kila siku kuna jua likitokea mashariki (mawio) na kuishia magharibi (machweo). Tunaanza siku asubuhi, inafuata mchana/adhuhuri, alasiri na jioni. 

Halafu kunakuwa usiku (giza) mpaka usiku wa manane hadi alfajiri na jua kutokea (mawio). Kadhalika, kuna mzunguko wa jua kwenda kaskazini na kusini mwa mstari wa Ikweta unaogawanya dunia katikati kusababisha kuwapo ‘kaskazini’ na ‘kusini’. 

Vivyo hivyo masuala ya mwezi na majira ya mvua (vuli na masika), ukame (kiangazi) pamoja na mwenendo mzima wa upepo (unapotoka na unapokwenda) ni misingi iliyowekwa na Mungu tangu kuumbwa kwa dunia. 

Isitoshe, kuwapo kwa misitu, wanyamapori, ndege angani na viumbe wengi baharini na sehemu nyingine jangwa (hakuna uoto wa asili).

Haya niliyotaja na nisiyotaja vikiunganishwa pamoja vinasababisha ‘tabia’ fulani kwa maisha ya binadamu na viumbe hai wengine. Msingi ukiwa ni ardhi (nchi kavu) na ardhi oevu. 

Ardhi pamoja na watu inakuwa nchi na hatimaye kusababisha ‘tabianchi’. Kazi za binadamu zinaposhamiri zinasababisha kuwapo tunachoita ‘mabadiliko ya tabianchi. Mungu aliumba vyote katika uhalisia wake, akamuweka binadamu amiliki na kutawala. Kuna nchi takriban 200 duniani na kila nchi ina utaratibu wake wa kumiliki na kutawala rasilimali zilizomo ndani ya mipaka yake. 

Kimsingi, ‘mabadiliko ya tabianchi’ yalianza kujitokeza miaka ya 1980 isipokuwa madhara kutokana na mafuriko, ukame au majanga ya asili (vimbunga); yalikuwa kidogo.

Dunia ilianza kushtuka mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Norway, Gro Harlem Brundtland, kutahadharisha kupitia taarifa iliyojulikana kama ‘Our Common Future’

Taarifa hii ilifafanua kuhusu ‘mabadiliko ya tabianchi’ kwamba tunaelekea pabaya maana joto linaongezeka kwa kasi huku maafa yakijitokeza. Kutokana na taarifa hiyo, Umoja wa Mataifa (UN) ukaitisha kikao cha wakuu wa nchi huko Rio De Janeiro, Brazil.

Tanzania iliwakilishwa na Rais wa Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi. Tangu wakati huo vikao vya wataalamu na wakuu wa nchi vimekuwa vikifanyika. Kikao cha 26 kilifanyika mwaka jana huko Glasgow, Scotland na kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan na wataalamu kadhaa. 

Licha ya vikao karibu kila mwaka lakini bado tunashuhudia ndani ya miaka 30 tangu mkutano wa Rio (1992); madhara makubwa kutokana na ‘mabadiliko ya tabianchi’. 

Hali ya joto duniani inazidi kupanda kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu. Mathalani, katika mataifa yaliyoendelea (ikiwamo China); kutokana na uzalishaji mkubwa viwandani; kiwango cha ‘gesiukaa’ kimekuwa kikiongezeka sana. 

‘Gesiukaa’ (CO2) ikiwa nyingi angani inaathiri kwa kiasi kikubwa utando ‘ozone layer’ ambao ni muhimu katika kupunguza nguvu za mionzi ya jua. Kuharibiwa utando huo na ‘gesiukaa’, kunasababisha joto kuongezeka na kuleta ‘mabadiliko ya tabianchi’. 

Hayo yakiwa yanajiri angani kutokana na ongezeko kubwa la shughuli za viwandani kwa kutumia nishati isiyo rafiki kwa mazingira kama makaa ya mawe, mafuta ya viwandani pamoja na ongezeko katika sekta ya usafirishaji (magari, treni, ndege) vyote hivyo vinachangia ongezeko la joto na mabadiliko ya tabianchi. 

Kwa upande wa mataifa yanayoendelea kama Tanzania; uzalishaji wa gesiukaa ni wa chini. Hata hivyo shughuli nyingi hasa za kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu, viwanda, utalii, usafirishaji, biashara na uchumi kwa ujumla zimeathirika sana kutokana na ‘mabadiliko ya tabianchi’ ikiwamo kuchanganyika na ‘mabadiliko ya tabiabinadamu’. 

Shughuli nyingi zinazofanyika Tanzania: kijamii na kiuchumi, si rafiki kwa mazingira kutokana na wengi wetu kutaka kupata fedha nyingi haraka bila kujali madhara yatokanayo na shughuli zinazofanyika zisizoendelevu. Hali hiyo ikichanganyika na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, wananchi tunaathirika sana kimaisha.

Sasa ‘mabadiliko ya tabianchi’ siyo kitu cha ‘kufikirika’. Ni janga kubwa kwa maisha yetu. Mfano, hali ya hewa ya sasa inachanganya wakulima, wafugaji na wahifadhi. 

Mathalani, mvua zinaponyesha nyingi nje ya msimu wakulima wanaduwaa maana inanyesha bila kutarajiwa. Ukame unapozidi wafugaji wanachanganyikiwa, hawajui la kufanya: mifugo inakufa. Vilevile kwa wahifadhi, wanyamapori kukosa maji na chakula na hatimaye kufa. Misitu kukauka sana na kupoteza uwezo wake wa kiikolojia na hatimaye kuteketezwa na ‘moto kichaa’.

Pamoja na hayo tusikate tamaa, tuchukue hatua thabiti, mfano, kuboresha mbinu za kilimo ikiwa ni pamoja na kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua kwa matumizi nyakati za ukame. 

Mbinu na utaalamu wa kilimo viwe rafiki kwa mazingira (mkazo uwe kilimo/ufugaji kijani). Mathalani, kilimo/ufugaji viwe jambo endelevu kwa kutumia eneo dogo na kupata mavuno mengi kuliko kufyeka misitu au kulima/kufuga hovyo na kupata mavuno kidogo; wakati huo huo udongo unapoteza rutuba kutokana na mmomonyoko usiodhibitiwa.

Kuwapo kwa uoto wa asili ni suala muhimu ili kuwezesha maji mengi ya mvua kuingia ardhini. Eneo likiwa wazi mvua ikinyesha udongo mwingi wenye rutuba unapelekwa mabondeni na mwingine kujaa katika mabwawa ya kuzalisha umeme; kwenye mito hadi kusababisha vina vyake kupungua. 

Vina vya mito vikisheheni tope/mchanga husababisha mafuriko kutokana na mito kama Msimbazi kujaa maji haraka, yakasambaa nje ya kingo zake, hivyo kusababisha mafuriko hata kama mvua haijanyesha eneo hilo lakini mvua iliyonyesha mbali ikasababisha mafuriko sehemu nyingine. 

Tuongeze juhudi za kupanda miti na kutunza misitu ya asili kwa faida ya wote. Misitu ya asili katika maeneo mbalimbali nchini inahitaji usimamizi madhubuti ili tuondokane na dhana ya kuiona ni ‘shamba la bibi’ kwa watu wengi kuingia na kufanya wanavyotaka, hivyo kuharibu uoto wa asili.              

Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician B. Kilahama, ni Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki.

By Jamhuri