DODOMA

Na Profesa Handley Mafwenga

Profesa Honest Prosper Ngowi, mwanafalsafa wa uchumi uliyebarikiwa na Mungu, uliyebarikiwa na ndimi njema za wanazuoni waliopenda maandiko yako, na kupendezewa na ulimi wako uliotema ubora wa masuala ya uchumi, fedha, na biashara.

Profesa usiyechoka, mwenye upendo na watu na usiyekuwa mwingi wa hila; baba mwenye hekima uliyependa kuzichota hekima kwa Mungu mithili ya Mfalme Suleimani ‘Mfalme wa Jerusalemu’.

Profesa usiyechagua na kufanya unyimi wa kipi cha kuwafundisha watu na hadi ukawa Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Muda Mfupi; Mtafiti na Mshauri katika Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki (campus) ya Dar es Salaam. 

Kwaheri mwanzilishi wa taasisi ya ushauri ya ANO Consulting Ltd. 

Mkali wewe, mbunifu wewe, uliyetafiti na kufanya machapisho zaidi ya 80 nikipenda kukuita ‘FDI Guru’ nawe ukiniita ‘Tax Guru’.

Ni juzi tu hapa VETA ukaniita ‘Multi – sectoral’ tukacheka, tukanywa chai pamoja. Kumbe unaniaga Prof?  

Umefanya tafiti nyingi sana zaidi ya 80 na kuandika ripoti lukuki, zaidi ya 300 kwenye majarida mbalimbali.  Baba wa uchumi jumla, biashara za kimataifa, uwekezaji (FDI), ujasiriamali, masuala ya maendeleo ya sekta binafsi, ukuaji wa uchumi na masuala ya ugatuzi ‘regional integration’.

Mtaalamu wa kuchambua midororo ya kiuchumi, mtaalamu wa mafuta na gesi. Kwaheri! 

Profesa Ngowi kwaheri mtaalamu wa ‘The African Centre for Technology Studies – (ACTS)’ ya Nairobi, Kenya. Kenya wanalia, Tanzania wanalia, dunia inalia, lakini Mungu amekukumbatia; unacheka naye. 

Prof, Profesa, Prof! Unakufa kipindi cha Kwaresma, unatoa damu kipindi cha Kwaresma, nahisi umetwambia: ‘Jililieni wenyewe’ na ulipokata roho uliona kiu. Ngowi wewe! wewe! wewe! wewe? 

Ngowi, mjumbe wa Jumuiya ya Wahadhili Waandamizi Chuo Kikuu cha Zambia. Ngowi! Huko nako kilio; na huko Chuo Kikuu cha Bergen, Norway wanalia.

Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda wanakulilia. Chuo Kikuu cha North West Afrika Kusini, wanalia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA) na Chuo Kikuu cha Tumaini ni vilio kaka.

Mkurugenzi katika bodi mbalimbali zikiwamo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), taasisi ya utafiti ya Economic and Social Research Foundation (ESRF), Foundation for Civil Society; kwaheri.

Kwaheri Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Envirocare inayojishughulisha na masuala ya mazingira na haki za binadamu.

Kwaheri Mwenyekiti wa Bodi ya Restless Development; taasisi inayosaidia vijana na kuwaandaa kuwa viongozi, kwaheri.

SWISSAID na Mama Misitu Kampeni ya Tanzania (MJUMITA), taasisi inayojishughulisha na kupiga kampeni kuhusu uharibifu wa mazingira hasa misitu.

Hata kama shetani anasema hautasimama nasi, Mungu wa Ibrahim, wa Isaka, Mungu wa Yakobo atakuinua; kwani udongo na mawe yatashuhudia ulivyoyakanyaga kutafuta riziki.

Sauti za wanafunzi wakati wote zitaongea waliyojifunza kwako. Familia yako haitakuacha. Tanzania, EAC, SADC na dunia nzima watashuhudia ulivyohangaika kujenga taifa hili: hakika haujafa.

Kwaheri bingwa; (tunashukuru kwa kila jambo). Kwaheri mtu wa Mungu (tutaku-miss sana tu). Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe na upumzike kwa Amani. Amen!  

Bwana akubariki na kukulinda; Bwana akuangazie nuru ya uso wake na kukufadhili. Bwana akuinulie uso wake na kukupa amani.

By Jamhuri