KATAVI

Na Mwandishi Wetu

Nchi inazidi kufunguka. Miradi mbalimbali imeanzishwa, inaanzishwa na itaanzishwa huku utekelezaji wa ujenzi wake ukiendelea kwa nia moja tu ya kuhakikisha uchumi wa nchi unazidi kuimarika.

Miongoni mwa ujenzi wa miradi inayoendelea kutekelezwa ni ule wa Bandari ya Karema iliyopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Mradi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na anayeijenga ni Kampuni ya Xiamen Ongoing Construction Group Ltd na mwangalizi ni Kampuni ya M/S Inter-Consult Ltd.

Hakuna shaka kwamba ujenzi wa bandari hiyo utakapokamilika itakuwa ni muhimu hapa nchini. 

Mradi wa bandari hiyo ulioanza Oktoba 25, 2019 unachukua mita 463,740 (sawa na ekari 144) za mraba na kati ya hizo, mita 267,2409 (sawa na ekari 66) ni eneo la nchi kavu na mita 196,500 (sawa na ekari 48) ni ndani ya maji na una thamani ya Sh bilioni 47.9. 

Pamoja na mambo mengine, mradi huo umetoa ajira kwa Watanzania wakiwamo wahandisi, mafundi umeme, madereva, wasaidizi, walinzi na watu wasiokuwa na ujuzi na unawasaidia kuanzia ngazi ya kijiji, tarafa, kata, wilaya, mkoa na hadi taifa.

Huku faida mojawapo ya bandari hiyo ni kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria, hasa reli kutoka Mpanda hadi Karema, kwa kuwa mwananchi atasafirisha mizigo mikubwa kutoka Dar es Salaam hadi Bandari ya Karema, kisha kupelekwa katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). 

Pia itakuwa mlango wa usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na kuunganisha bandari za Moba na Kalemii zilizoko DRC.

Hadi sasa ujenzi wa bandari hiyo umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika Mei mwaka huu. Kimsingi, bandari hiyo ni mpya katika Ziwa Tanganyika chini ya TPA.

Akizungumza mjini hapa hivi karibuni, Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Inter Consult, Eliasante Urassa, amesema ujenzi huo kwa sasa umefikia asilimia 85 huku maeneo makuu ya bandari kama gati, kingo za kuzuia mawimbi na yadi ya kuhifadhia makontena yamekamilika kwa asilimia 98.

“Mradi unaendelea vizuri na tupo kwenye asilimia 85 ya jumla, utakamilika kwa wakati Mei 20 mwaka huu kama ulivyopangwa,” anasema. 

Urassa anasema eneo la kuhifadhi kontena lina ukubwa wa mita za mraba 22,500, gati ina mita 150, kingo ya kuzuia mawimbi ina mita zaidi ya 1,100 na bandari ina kina cha maji cha urefu wa mita 4.5 kutoka kina cha chini cha maji.

Anasema ujenzi huo pia unahusisha jengo la abiria, ghala la kuhifadhia mizigo, ofisi, jengo la

mitambo na miundombinu ya umeme, maji safi na maji taka, vyote hivi vikiwa vimefikia

asilimia 60.

Naye Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Manga Gassaya, anasema mradi huo unajengwa katika eneo la awali la ukubwa wa ekari 15 kati ya 66 za eneo lote la Bandari ya Karema.

Anasema bandari hiyo ikikamilika itaongeza kasi na ufanisi wa kusafirisha mizigo kutoka nchini kwenda nchi jirani za Kusini mwa Afrika ikiwamo DRC na Burundi, kwa kuwa katika eneo lililojengwa kwa sasa litakuwa na uwezo wa kupokea kontena zaidi ya milioni moja na mizigo mingine isiyo ya kontena.

“Kwa kweli tunamshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha inayowezesha kukamilika kwa mradi huu kwa wakati. Yeye akitoa maagizo uzuri wake na fedha anatoa, hivyo niwaombe watumiaji wa bandari zetu wawe tayari Juni, mwaka huu bandari hii ya Karema itaanza kutumika,” anasema.

Gassaya anasema wanafanya utaratibu wa kutafuta eneo DRC ili kujenga bandari kavu wakati wao wakiendelea kuboresha bandari yao.

Kuhusu abiria, anasema zaidi ya abiria 50,000 watasafiri katika bandari hiyo, kwa kuwa jengo la abiria lina uwezo wa kuchukua abiria 100 kwa wakati mmoja.

Pia anasema bado barabara haijajengwa kwa kiwango cha lami kwenda bandarini hapo na reli pia haijafika na amewasiliana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kuhakikishiwa ujenzi utafanyika.

Vilevile anasema matarajio yao ni kwamba ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR hasa kipande cha Tabora – Mpanda kitaleta tija kwa mizigo kufika kwa gharama nafuu.

By Jamhuri