Jambo linapoitwa la Muungano Maana yake Nini
3.2.11 Jibu la rahisi ni kuwa jambo linapoitwa la Muungano ni kuwa Zanzibar haina uwezo wa kulisimamia kisera, kiutawala na kisheria. Hata hivyo suala hili ni gumu kuliko linavyoonekana. Kabla ya kuja sera za biashara Huria mashirika kama vile Air Tanzania, Shirika la Posta na Simu na Benki ya Taifa ya Biashara n.k yakijulikana kama mashirika ya Muungano. Katika vikao kadhaa ilikubaliwa kuwa Zanzibar ishirikishwe katika uendeshaji wa mashirika hayo ya Muungano. Mashirika hayo mengi yamebinafsishwa.

3.2.12 Hisa za mashirika ama zinamilikiwa na HAZINA ya Serikali ya Muungano ama zimeuzwa kwa ‘Strategic Investors” au hata kwa wananchi. Zanzibar haikupewa hisa. Kuna hoja kwamba zile hisa za Serikali ya Muungano ndio pia za Zanzibar. Hoja hii haina uzito kwani katika Muafaka baina SMT na SMZ ilikubaliwa kuwa suala hilo lizungumzwe upya baina ya Serikali mbili (Uk. 46, dondoo la 18.4.3 la Muafaka).

Kwa kadri ya ninavyofahamu suala hilo halijazungumzwa tena na Zanzibar imekosa haki zote katika mashirika hayo yaliyokuwa ya Muungano. Tatizo kama hilo lilijitokeza katika Benki Kuu. SMZ ilipodai kuwa na hisa ambazo
ilizilipia kupitia Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, Zanzibar ilielezwa na SMT kuwa haiwezi kuwa na hisa katika Benki Kuu lakini inaweza kupewa mafao kwa kima cha asilimia 4.5.

3.2.13 Kwa upande wa pili, taasisi ambazo ni za Muungano kama vile TRA, TPDC, TCRA, TCAA, n.k zinaonekena ni za Muungano katika ngazi ya Bodi ya Wakurugenzi. Hata hivyo katika ajira vigezo vinavyotumika ni vya Tanzania Bara. Kwa mfano anayeomba kuajiriwa katika Taasisi hizo kama Mwanasheria, lazima awe ni Wakili wa Mahkama Kuu ya Tanzania (Bara) ingawa Mahkama Kuu ya Zanzibar na Tanzania (Bara) zina mamlaka sawa, lakini kuwa wakili wa Mahkama Kuu, Zanzibar hakutambuliwi.

Aidha Makao Makuu ya taasisi zote hizo yapo upande mmoja wa Muungano. Mashirika haya sio tu kuwa yanatoa fursa za ajira lakini yanatumia fedha nyingi sana kufundisha wafanyakazi wake kuliko fedha zinazotumiwa na bajeti ya SMZ kufundisha watumishi wake. Hivyo kama taasisi hizo ni za Muungano kwa nini Mshirika mmoja asifaidike na fursa hizo?

Maelezo haya yanaweka bayana suala ambalo
halijapatiwa jibu la nini maana ya jambo la
Muungano?

By Jamhuri