Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar ea Salaam

Chama cha ACT Wazalendo kimetoa wito kwa Serikali na vyombo vyake vya dola kupunguza muda wa uendeshaji wa kesi za ukatili dhidi ya watoto na wanawake.

Chama hicho kimependekeza muda wa uendeshwaji wa mashauri hayo usizidi miezi miwili hadi kumalizika kwake ili haki ionekane kutendeka.

Ushauri huo umetolewa leo Oktoba 11, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri kivuli wa Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, Janeth Rithe, ambapo amesema ukatili dhidi ya watoto wa kike bado upo katika jamii, zetu hivyo zinahitaji mbinu mbalimbali za kuukabili ikiwa ni pamoja na kesi zinazohusu vitendo hivyo kukamilika kwa muda mfupi tofauti na sasa ambapo zinachukua muda mrefu kukamilika.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, ikiwa ni Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike Duniani, amesema changamoto kubwa zinazowakabili watoto wa kike ni pamoja na ndoa za utotoni, ubakaji, ulawiti na udhalilishaji mitandaoni.

“Athari za vitendo vya ukatili kwa makundi hayo kijamii, kiuchumi na hata kiafya ni kubwa sana. Vilevile, ukatili unapalilia kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii baina ya mtoto wa kike na wa kiume.

“Hapa nchini Tanzania tunaona bado watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi sana ambazo zinakwamisha ustawi na maendeleo yao.”amesema Rithe.

Rithe ambaye pia ni Naibu Katibu wa habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho,ameongeza kuwa kutokuwepo mazingira salama na rafiki kwa mtoto wa kike shuleni ikiwamo kukosa vifaa vya kujisitiri (taulo za kike), maji ya uhakika pamoja na kutokuwekwa wazi sheria zinazowalinda waathirika wa mimba za utotoni kuendelea na masomo.

Amesisitiza kuwa kuendelea kuwapo kwa changamoto  hizo sambamba na unyanyapaa ni moja ya visababishi vya kuzuia fursa kwa watoto wa kike kupata haki zao na kutimiza malengo yao. 

“Katika kuadhimisha siku hii, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuongeza jitihada kwa kuunganisha nguvu katika kupiga vita ndoa za utotoni, ukeketaji na mimba za utotoni.

“Serikali iongeze usalama na stadi za maisha kwa watoto mashuleni kwa kupanua na kuanzisha mabaraza ya watoto, klabu za watoto na kwa upekee kabisa kutoa bure vifaa vya kujistiri na hedhi kwa wasichana” alisisitiza Rithe.