*Mhandisi Kasekenya aeleza mikakati kukabiliana na athari za mvua kubwa Vwawa

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songwe

Songwe, moja ya mikoa ya kimkakati nchini, imedhamiria kuziunganisha wilaya zake nne kwa mtandao wa barabara za lami.

Mkoa huo unaoiunganisha Tanzania na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia mipaka na nataifa ya Malawi na Zambia, mbali ya kuwa miongoni mwa vinara wa kilimo, pia umejaliwa kuwa na rasilimali nyingi na muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Ni kutokana na umuhimu wa Songwe kiuchumi na kijamii ndio maana sasa serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, imeandaa mkakati kuhakikisha miji mikuu yote ya wilaya zake inaunganishwa kwa lami.

Wilaya zinazounda Mkoa wa Songwe ni Mbozi, Ileje, Momba na Songwe.

Miongoni mwa barabara zinazojengwa kwa zege katika milima ya Ileje kama suluhisho la kudumu la usafiri na usafirishaji wilayani humo.

“Tayari miji ya Vwawa (uliopo makao makuu ya mkoa, wilaya ya Mbozi) na Itumba (wilaya ya Ileje) imekwisha unganishwa kwa lami,” anasema Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga alipozungumza na JAMHURI wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya wiki iliyopita.

Bishanga anasema miji ya Mkwajumi (Wilaya ya Songwe) na Chitete (Momba) kuwa nayo ipo kwenye mipango ya kuunganishwa kwa barabara za lami na Vwawa, makao makuu ya mkoa.

Muunganiko wa mtandao wa barabara za lami mkoani Songwe unategemewa kuongeza ufanisi katika shughuli za kiutawala, kiuchumi na kijamii, hivyo kuchochea maendeleo ya mkoa.

Mkoa wa Songwe una wilaya nne ambazo ni Mbozi, Ileje, Momba na Songwe; zikiwa na utajiri wa ardhi ya rutuba, dhahabu na kubwa zaidi gesi ya ‘helium’ iliyogundulika Bonde la Ziwa Rukwa.

Shughuli nyingine za kiuchumi ni kilimo cha mahindi, maharage, mpunga, ndizi, ufuta, kahawa, karanga, mananasi, iriki na mboga.
Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Songwe, Kasekenya amesema kukosekana kwa muunganiko wa mtandao wa barabara kati ya wilaya hizo huwalazimisha wananchi kupita Mbalizi, mji mdogo uliopo mkoani Mbeya, ili kufika makao makuu ya mkoa wa Songwe.

Waathirika wakubwa na wananchi wanaosafiri kati ya Vwawa na Mkwajuni; Makao Makuu ya Wilaya ya Songwe.

Miongoni mwa barabara zinazojengwa kwa zege katika milima ya Ileje kama suluhisho la kudumu la usafiri na usafirishaji wilayani humo.

“Safari hiyo (kati ya Vwawa na Mkwajuni) ya kupitia Mbalizi inaongeza umbali kwa kilometa 64 sambamba na gharama ya uendeshaji,” amesema Kasekenya ambaye pia ni Mbunge wa Ileje wakati akitembelea miradi mbalimbali ya ujenzi ambayo ama inatekelezwa au inategemewa kuanza.

Naibu Waziri ameitumia ziara yake kuwaondoa wananchi hofu kwa kuwaeleza namna wizara inavyojiandaa kukabiliana na athari zitakazotokea kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha msimu huu.

Kukatika kwa mawasiliano ya barabara na maporomoko ya udongo (land slide) maeneo ya milimani (hasa wilayani Ileje) ni miongoni mwa athari zinazotarajiwa kusababishwa na mvua kubwa.

Ni changamoto kama hizo iwapo hazitadhibitiwa mapema ndizo husababisha kupanda kwa gharama za maisha na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi, kiutawala na kijamii si kwa Songwe pekee, bali nchini kote.

Chitete yalipo Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, nako kunakosekana muunganiko wa moja kwa moja wa barabara ya lami kati yake na Vwawa pamoja na Tunduma, mji maarufu wa kibiashara na kimkakati uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia, ambao ni sehemu ya wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa TANROADS, mtandao wa barabara za Songwe na Mbozi ni ile itokayo Vwawa kupitia NAFCO, Magamba, Galula hadi Mkwajumi.

Hii itakapokuwa imewekwa lami itapunguza umbali kwa kilometa 64 ikilinganishwa na inayotumika sasa ya Vwawa kupitia Mbalizi hadi Mkwajuni, hivyo kuongeza ufanisi katika utawala, shughuli za kiuchumi na kijamii.

Utofauti huo wa umbali unathibitishwa na taarifa ya Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Bishanga, inayonyesha kuwa umbali wa kupitia Mbalizi hadi Chang’ombe inapoishia barabara ya Mbeya ni km 128; wakati barabara ya Vwawa kupitia Magamba hadi Chang’ombe una urefu wa ni km 64 tu; hivyo kufanya tofauti ya km 64.

Kana kwamba haitoshi, Songwe inafaida nyingine kwa uchumi wa Tanzania, kwa kuwa ndipo lilipo lango kuu la SADC kupitia Tunduma.

Hii maana yake miundombinu bora ya barabara itachangia katika ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na nchi za SADC.

Miradi iliyotembelewa na Naibu Waziri, Mhandisi Kasekenya katika ziara yake mkoani humo ni pamoja na barabara ya Ruanda Nyimbili – Hasamba – Izyla – Itumba; Mahenje – Hasamba – Vwawa na Ruanda – Idiwili.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (kulia) akikagua maeneo ‘korofi’ ya barabara yanayoimarishwa kwa kuwekwa zege katika Kijiji cha Mbalula wilayani Ileje, ikiwa ni maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kutokea kutokana na mvua kubwa zinazotaraniwa kunyesha msimu huu.
 

Nyingine katika kiwango cha lami, ni Barabara ya Msangano – Utambalila na sehemu ya Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, Chitete, barabara ya Chang’ombe –Mkwajuni – Patamela – Makongorosi na sehemu ya Mkwajuni, Makao Makuu Wilaya ya Songwe.

Ipo pia miradi ya matengenezo ya kawaida na muda maalumu kwa barabara za Chang’ombe – Patamela na Galula – Namkukwe, na matengenezo ya muda maalumu ya Daraja la Songwe katika barabara ya mkoa ya Galula – Namkukwe.

By Jamhuri