New Delhi, India

Wizara ya Afya Tanzania na Taasisi za Afya nchini India zimeingia makubaliano ya ushirikiano ya kuboresha huduma za afya na uzalishaji wa bidhaa za afya nchini Tanzania.

Shughuli ya kusaini hati za makubaliano hayo imeshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo kwa Wizara ya Afya Katibu Mkuu Dkt. John Jingu amesaini hati za makubaliano na Taasisi za Afya nchini India.


Rais Samia amezitaka pande zote zilizoingia makubaliano kuheshimu na kutekeleza masharti ya makubaliano hayo kwa manufaa ya nchi zetu mbili

Makubaliano hayo yataiwezesha Wizara ya Afya Tanzania kushirikiana na  
Hospitali ya Huduma za Kibingwa Bobezi za Magonjwa ya Watoto ya Rainbow kwa ajili ya kuwezesha Wataalamu wa Magonjwa ya Watoto Tanzania kupata Mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi.

Wizara ya Afya Tanzania kushirikiana na Hospitali ya Huduma za kibingwa bobezi ya Max Healthcare Group kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ubingwa bobezi (hususani Upandikizaji wa Ini na Upandikizaji wa Figo wa marudio)

Wizara ya Afya Tanzania kushirikiana na Kampuni ya Hester Bioscience ya nchini India kwenye uwekezaji wa Kiwanda cha Dawa za Binadamu na Wanyama nchini Tanzania wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 24.

Hafla ya kusainiwa kwa hati hizo imeshuhudiwa pia na Mawaziri mbalimbali, akiwemo Waziri wa Afya Mhe. Ummy A. Mwalimu na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe.  Nasoro A. Mazrui