Maafisa wa usalama wamesema roketi kadhaa zimefyetuliwa kuelekea kambi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani nchini Iraq.

Duru za usalama za Iraq zimeeleza kuwa roketi nne zimeanguka karibu na kambi ya jeshi ya Ain al-Assad iliyoko mkoa wa Anbar.

Afisa wa Marekani amesema ripoti za awali zimeonyesha kuwa mashambulizi hayo ya roketi yalilenga nje ya kambi walimokuwa japo hayakusababisha majeruhi au uharibifu. Hata hivyo, hakuna kundi lolote lililojitokeza kudai kuhusika na hujuma hiyo.

Mashambulizi hayo yametokea baada ya kufanyika mkutano wa kiusalama wiki hii kati ya maafisa wa Iraq na Marekani mjini Washington kuhusu mustakabali wa muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Marekani nchini Iraq.

Makundi yanayoungwa mkono na Iran yamekuwa yakiushinikiza muungano huo uondoke nchini humo.