Ndugu Rais, sijaja hapa kumlilia Wilson Kabwe, la hasha. Nimekuja hapa ndugu Rais, kumzika Wilson Kabwe. 

Katika kitabu cha Julius Kaizari kama kilivyotafsiriwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, imeandikwa, “Mtu akifa huzikwa na mazuri yake yote. Mabaya yake hubaki yakizagaa duniani. Basi na iwe hivyo kwa Kaizari.” Ndugu Rais, na mimi nasema basi na iwe hivyo kwa Wilson Kabwe.

Ndugu Rais, sikupata kumfahamu Wilson Kabwe katika uhai wake, na madhali amefariki, basi sitamfahamu tena katika uhai wangu. 

Wakati George Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), akisema Tanzania imepoteza kiongozi mahiri na mwaminifu aliyeitumikia nafasi yake kwa umakini na weledi mkubwa kwa manufaa ya wananchi; aliyemchongea anasema Wilson Kabwe alikuwa fisadi aliyefanya ufisadi mkubwa. 

Wakati waziri anasema, “Kwa ngazi aliyokuwa amefikia Wilson Kabwe ni sawa na Katibu Mkuu wa Wizara, leo hii ukiizungumzia Mwanza inayosifika kwa usafi na miundombinu, huwezi kuacha kumtaja Wilson Kabwe.”

Aliyemchongea anasema hayuko tayari kufanya kazi naye, kauli ambayo haikumwachia nafasi Rais wa nchi ya kukataa. 

Haya mamlaka makubwa hata kumwamuru Rais, vijana wanayapata wapi? Kama Wilson Kabwe alifanya ufisadi mkubwa, basi na kudhalilishwa darajani huku nchi nzima na ulimwengu vikitazama, ilikuwa ni adhabu kubwa. 

Sababu ya kifo cha Wilson Kabwe wanadamu tunabahatisha tu, lakini Mwenyezi Mungu anajua kilichomuua.

Ana Wilson Kabwe, kama baba yake, simfahamu, lakini ujasiri aliouonesha huku maiti ya baba yake ikiwa mbele yake, ni wa kuigwa na kila aliye mwema. Akiwa katika wakati mgumu kabisa kwa wanadamu walio wengi, aliyakataa majaribu ya shetani, akaucha uovu upite zake.

Nitamheshimu sana binti huyu kwa kuukana unafiki hadharani. Ni watu wachache sana hapa duniani wanaoweza kusimama katika kweli wakati wa majaribu magumu kama yale.

Katika hili, Ana alisimama peke yake kama akinukuu maneno ya Bwana Yesu alisema, “Nenda zako shetani!”

Ana alinirudisha enzi za utoto wangu kabla nchi yetu haijapata uhuru, na kwa umri aliokufa nao baba yake, alikuwa hajazaliwa. Tuliishi katika imani za kichawi. 

Mtu alipofariki, yule aliyedhaniwa kuwa ndiye aliyesababisha kifo hicho alipofika msibani, waombolezaji walimkamata, wakamfunga majani mwili mzima, wakamchoma moto.

Ndugu Rais, inakuwa vigumu kwa wengine kuelewa ni kipi kilichoipeleka  Serikali katika msiba wa Wilson Kabwe. Timamu wamekwambia usiende. Unaenda kwa kutegemea bunduki za polisi zilizonunuliwa kwa fedha iliyotokana na kodi ya wananchi akiwamo Wilson Kabwe na

wanawe. Kifo chake kilikupendezesha nini mpaka umtake wakati huu akiwa mfu? 

Ubabe wa kitoto ni ujinga

Viongozi, someni maandiko katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Yaliyoandikwa ukurasa wa 98 yangetimia. Imeandikwa, “Wananchi wenye

hasira walimpatia kisago cha nguvu…lakini aliokolewa na polisi. Hata hivyo, mpaka anafikishwa mbele ya Mwalimu Mkuu alikuwa tayari hana macho wala masikio. Sehemu zake muhimu za mwili wake, wananchi

walibaki nazo kama kumbukumbu.”

Mikosi inaiandama nchi

Ndugu Rais, mcha Mungu wakweli hawezi kutetea ufisadi wala mafisadi. Kazi unayofanya ya kutumbua majipu ni kazi njema na kwa hili ubarikiwe

sana. Ukitaka kumpendeza Mwenyezi Mungu kwa kazi hii, usichague ya kutumbua. Tumbua yote; waliowema watakuombea lakini ukweli unapotuumbua tukubali.

Ni ukweli uliowazi kuwa wananchi hawakupewa nafasi ya kumsikiliza Wilson Kabwe akijitetea. Mshitaki wake hakuwaonesha wananchi ushahidi wowote, na alipomaliza tu kumsomea mashtaka, Wilson Kabwe alihukumiwa palepale bila kupewa nafasi ya kujitetea.

Bora hata Wayahudi waliomshtaki Yesu walikuwa na ushahidi japo ulikuwa ni wa uongo. Ndugu Rais mwenyewe umetamka, “Najua watu wanawachukia sana vijana, ila nitawaongeza.” 

Baba, watu timamu hawawachukii vijana kwa ujana wao. Watu makini wanawachukia wahuni – wawe wazee au wawe vijana. 

Watu wa Mungu katika nchi hii hawawezi kusahau lile kundi la wahuni waliomshambulia mzee Joseph Sinde Warioba alipokuwa anatetea maoni aliyopewa na wananchi wenyewe ili yaingizwe katika Katiba mpya.

Manyang’au waliyatupa wakawatuma wahuni wakamshambulie aliyekuwa anawatetea maskini wa Mungu. Baba, ni wanyonge gani tunaosema

tunawatetea? Siwajui watu wale lakini kama walikuwa ni wazee, ni wahuni,  kama walikuwa ni vijana ni wahuni. Wahuni ni wahuni tu hawatakiwi katika jamii iliyostaarabika. Na kwa kuwa ni wahuni, kama jana walitumwa kwa Warioba, leo kwa Kabwe, kesho watatumwa kwako. Mungu akulinde baba.

Ndugu Rais, nani amesahau ufisadi mkubwa uliokuwa unafanywa na baadhi ya viongozi wa juu wa awamu ya nne, wakiwatumia viongozi wa chini kwa manufaa yao na familia zao? Kama Wilson Kabwe alizihifadhi nyaraka zilizotoka kwa wakubwa wake zikimwamuru afanye yale anayotuhumiwa kwayo, nani sasa atazionesha naye amekwishakufa? 

Mbona tumesikia madudu ya UDA? Na sasa si Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi? Ndugu Rais, kwanini Wilson Kabwe hakupewa nafasi ya kujitetea? Baba, achana na wahuni ili umpe Mungu nafasi ya kukubariki.

Ndugu Rais, vilio vya wananchi wako vilivyoijaza hewa ya nchi hii wakikwambia kuwa hapo Ikulu ulipo ni mahali patakatifu, uvue viatu hivi, vitakoma lini? 

Mwenyezi Mungu alipomuumba mwanadamu alimuumba na masikio mawili, lakini akampa mdomo mmoja tu. Alitaka asikilize zaidi kuliko kusema. Usipowasikiliza sasa, Mwenyezi Mungu atawasikiliza.

By Jamhuri