Mchezo wa soka unahitaji benchi la ufundi lenye watalamu wenye ueledi mkubwa  wenye uwezo wa kuendana na mabadiliko ya soka kadri mda unavyobadilika.

Wakizungumza na JAMHURI juu ya mabadiliko yaliyofikiwa na  klabu ya Simba wachezaji wa zamani na watalamu wa mchezo huo  wamesema  uwekezaji bila ya mipango endelevu unaweza kuja kuwa kaa la moto ndani ya klabu.

Peter Tino mchezaji wa zamani aliyeshiriki  fainali za mataifa ya Afrika  mwaka 1980 nchini Nigeria amesema malengo yanaweza kuwa mazuri lakini pakawepo na msigano katika utekelezaji.

Amesema vilabu nyingi barani Afrika vimeshindwa kupata maendeleo kwa sababu ya ukosefu wa viongozi wenye mipango yenye uwezo wa kuleta tija.

“Simba wanapaswa kupongezwa kwa hatua nzuri waliyofikia lakini wanatakiwa kuwa makini hasa katika masuala ya usimamizi wa sera za kimaendeleo” amesema Tino.

Tino amesema ni kweli mpira unahitaji fedha lakini uwepo wa fedha bila ya kuwa na usimamizi imara ni sawa na kazi bure na matokeo ni migogoro.

Amesema klabu ya Simba inahitaji kuweka mifumo madhubuti tena ya kisasa ya kuendesha klabu hiyo, mifumo hiyo itasaidia weka wazi mipaka ya kiutendaji kati ya viongozi na benchi la ufundi.

“Bila ya uwepo wa mipaka ya utendaji wanaweza wakajikuta wakiendelea na mtindo usajili ndani ya klabu kufanywa na watu wasiokuwa watalamu katika benchi la ufundi,” amesema Tino.

Amesema ni miaka 37 imepita tangu Tanzania iliposhiriki kwenye mashindano ya bara la Afrika, jambo ambalo ni aibu kwa taifa.

Amesema kinachotakiwa ni umakini na nia ya dhati ya kuiona Simba ikiwa moja ya klabu kubwa na yenye mafanikio barani Afrika na hii itategemea mipango.

Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Salumu Madadi, amesema Simba wanatakiwa kuwa makini na mageuzi waliyoyachagua.

“Haya ni mageuzi makubwa yanayohitaji umakini na weledi wa hali ya juu kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa kwa kiwango kizuri”amesema Madadi.

Kocha wa zamani wa klabu hiyo King Kibadeni Mputa amesema mageuzi ndani ya vilabu hayawezi kuepukika katika klabu inayohitaji kuendana na wakati.

Amesema kinachohitajika ni uwepo wa viongozi na wataalamu wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo yaliyokusudiwa ndani ya klabu husika.

Amesema uwepo wa vilabu bora nchini utachangia  uwepo wa timu bora ya taifa, itakayoweza kutoa ushindani katika mashindano mbalimbali.

Katibu wa Baraza la Wazee wa klabu ya Yanga Ibrahim Akilimali amesema uthubutu uliofanywa na  klabu ya Simba ni jambo jema lakini wanapaswa kwenda mbali zaidi ya hapo vinginevyo inaweza kuwa  historia kwao.

Amesema Simba inahitaji kuwa na jopo la wataalamu waliobobea katika masuala ya usimamizi wa fedha na  benchi zuri la ufundi.

“Unajua vilabu vyetu  vinaendeshwa na wanachama ambao wengi hawana utaalamu wa masuala ya soka, watani wasipojipanga vizuri watalia,” amesema Akilimali.

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo Steven Mapunda “Garincha” amesema kuna haja ya klabu kufanya mabadiliko katika maeneo yanayoonekana kuwa na mapungufu.

“Benchi la ufundi  linahitaji kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kuzunguka nchi nzima na nje ya  kutafuta vijana wadogo wenye vipaji kwa ajili ya timu za vijana” amesema Mapunda.

Amaesema wahusika wanapaswa kuwa makini wakati wa usajili na kuachana na utaratibu wa usajilki kufanywa na watu wasiokuwa na weledi katika masuala ya soka.

Amesema uwekezaji wa Mohamed Dewji ni mkubwa unaotakiwa  kuiweka Simba katika anga za kimataifa na kuwa na uwezo wa kushindana na vilabu kama TP Mazembe na vingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

By Jamhuri