Taifa Stars-1Unapozungumza suala la soka hapa nchini kwa wiki hii bila kuitaja timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), bado unakuwa hujaeleza kile kilichotawala vichwa vya wanamichezo.

Pamoja kipigo cha Taifa Stars cha mabao 7-0 bado kuna hekima ya kujifunza kutoka kwa mchezaji Elius Maguri ambaye alifunga goli katika mechi hiyo na kukataliwa. 

Maguri aliyekuwa anakipiga kwa wekundu wa Msimbazi akitokea Ruvu Shooting na sasa akiwa anakipiga chini ya kocha Patrick Liewig pale Stand United ameonesha hekima ya hali ya juu sana katika soka.

Maguri ndio kinara wa mabao katika Ligi kuu ya Vodacom iliyosimama kupisha michuano ya Kombe la Chalenji.

Ukinara wa Maguri katika upachikaji wa mabao ni matokeo ya hekima ya utulivu katika soka maana kutoka kuvuma Ruvu Shooting mpaka kusajiliwa Simba kwa mbwembwe na kuachwa kwa kuvunjiwa mkataba ni jambo linaloumiza sana na kuvunja moyo.

Tumeona wachezaji wengi wazuri na wenye vipaji wakiangamia mara baada ya kuachwa na timu kubwa za Simba na Yanga.

Kupotea kwa viwango kwa wachezaji hao waliotemwa na timu hizo baada ya usajili wa mbwembwe kumechangiwa sana na kukosa utulivu na hali ya kukamia.

Wapo walioachwa na kuamua kupiga makelele na tambo za kutosha kwamba watazikomesha timu zilizowaacha mara watakapokutana nazo na wengine wameshinda kwenye vyombo vya habari kuporomosha tuhuma kwa timu zilizowaacha na kusahau kuwa kazi yao ni soka.

Nimeandika hapa mara kadhaa kuwa mambo ya kusemasema sio kazi ya wachezaji maana wao wanapaswa kuongea kwa miguu wala sio midomo.

Maguri ameonesha kile ambacho wengi wameshindwa kukionesha kwa miaka mingi, maana mchezaji akiachwa timu kubwa kama Simba, Yanga na sasa Azam anaona mwisho wa maisha yake ya soka umefika badala ya kutuliza akili na kucheza soka ili watu wasikie malalamiko yake ya kuachwa kwa kuonewa kutoka katika miguu yake. 

Wachezaji chipukizi wenye vipaji wanaosajiliwa timu kubwa hapa nchini wanapaswa kuelewa kuwa kwa tabia ya timu zetu hizi wao wanasajiliwa ili wakacheze mpira na kuleta matokeo na si kama wanasajiliwa ili wakavumiliwe. 

Maguri ameiona hekima akaamua kutulia na kusakata kabumbu na leo ukitaja Ligi Kuu ya Vodacom bila kumtaja yeye unakuwa umekosea, unapotaja ubora wa Taifa bila yeye unakuwa umeharibu na unapotaja mchezaji anayezitoa udenda timu kubwa huko nje ukimuacha Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe bila Maguri bado utakuwa hujatenda haki. 

Hekima ya Magurini utulivu na kuchukulia changamoto kama sehemu ya mafunzo na sio lawama kama wengi wanavyofanya.

Katika mazingira ya kuachwa na timu kubwa kama Simba ilihitaji utulivu tu ili kuonesha kile kilichofanya akaachwa na Simba.

Wapo wanaochwa Simba na kwenda Yanga na kuachwa Yanga kwenda Simba na wakaonesha makali yao, lakini sio kutoka timu kama hizo na kwenda timu ndogo au mpya katika ligi.

Leo TP Mazembe wanapomuhitaji Maguri lazima tuitazame hekima ya utulivu wa Maguri ambayo ilimfanya asisikilize makelele na kubezwa kwa aina yo yote kwa madai ya kushuka kiwango.

Makelele hayo nayafananisha na yale ya waarabu wa Algeria ambao waliamua kuzomea wakati wimbo wa Taifa wa Tanzania unaimbwa, lakini pamoja na makelele hayo ni yule yule Maguri asiyesikiliza makelele ya kuzomea akafunga goli lililokataliwa.

Ukomavu wa hekima ya Maguri ndio unanifanya niseme kwamba Taifa Stars ilihitaji hekima kama ya Maguri. 

Nimemsikia Kocha Mkuu wa Taifa Stars- mzalendo Charles Boniface Mkwasa akieleza kwa masikitiko hila walizotendewa na Waalgeria wale katika mechi ya marudiano.

Ninaelewa kuwa kocha kama mtaalamu wa ufundi lazima imuume sana hasa katika nyakati hizi ambazo Watanzania wamempokea kama nuru ya ushindi katika soka la taifa letu.

Suala ninalojiuliza hapa ni kuhusu huu ugeni wetu usiokwisha kwa matendo ya mataifa ya kiarabu katika soka letu. Nani asiyeelewa fitina za Waalgeria, Wamisri, Wamoroco na wengineo?

Ina maana tulitarajia kwa kandanda lile lililopigwa hapa Bongo dhidi ya Waalgeria kwamba tungekwenda kwao na wangetupokea kwa furaha na upendo?

Sisi ni wageni wa hao Waarabu au ndio tumekuwa kama wale wachezaji wanaosajiliwa na Simba na Yanga kwa mbwembwe na kuachwa baada ya muda mfupi kishaw akaingia mtaani na kulalamika eti hawakupewa muda wa kuvumiliwa waoneshe vipaji vyao kana kwamba wao ni wageni wa timu hizo?

Bado tulihitaji hekima ya Maguri hata Taifa Stars maana maelezo ya manyanyaso yale yale baada ya mechi dhidi ya timu zilezile ni ishara kuwa hatufanyi tathmini wala kujipanga baada ya kufanya vibaya kwa sababu mbalimbali.

 

Simu: 0715366010

Baruapepe: [email protected]

By Jamhuri