Klabu ya Manchester United ya jijini Manchester nchini England imeanza kupasua mioyo ya mashabiki wake baada ya kupata sare tatu mfululizo ndani ya majuma mawili.

Man United maarufu kama Mashetani Wekundu ilipata sare nyumbani katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya (UEFA) dhidi ya PSV Eindhoven ya Uholanzi, kisha ikafuatiwa sare ya ugenini dhidi ya timu ya Leicester City katika Ligi Kuu ya England na mwisho wa wiki iliyopita imetoka sare ya bila kufungana na Wagonga Nyundo wa London, West Ham United.

Klabu ya Manchester United ambayo tangu kustaafu kwa kocha wa kihistoria wa klabu hiyo, Sir Alex Ferguson imekuwa na wakati mgumu kurudi enzi zake za ubabe wa kugawa vipigo kwa timu mbalimbali hususani mechi ya nyumbani pale uwanjani kwao Old Trafford ambako mashabiki wake walizoea kupaita “machinjoni”. 

Timu hiyo ambayo iliyumba sana ilipokuwa chini ya Kocha David Moyes ilionekana kurejesha matumaini baada ya kukabidhiwa mikononi mwa Luis Van Gaal kutoka Uholanzi. Mwanzo wa Van Gaal ulikuwa na matumaini makubwa sana kwa mashabiki wake kuwa heshima inarejea jijini Manchester. 

Imani ya mashabiki ilikuwa kubwa na ndio maana hata alipoanza kupukutisha mastaa kama Rio Ferdinand, Nemanja Vidic, Patrice Evra, Shinji Kagawa, Chicharito, Luis Nani na wengineo, mashabiki wengi hawakuwa na mashaka yoyote. Imani ikiwa kubwa na hofu huondoka, msimu wa kwanza wa Van Gaal ulikwisha kwa Man United kurejea katika michuano ya Uefa baada ya msimu uliotangulia kuishia nafasi ya saba na kushindwa hata kushiriki michuano ya Europa na hapo matumaini yalirejea kwamba msimu unaofuatia yaani msimu huu wa 2015/2016 Man United itakuwa moto kama enzi za kibabu Fergie lakini mambo hayaoneshi kuwa hivyo. 

Usajili wa gharama na wa kuvunja rekodi umefanyika na mishahara ya kufuru imelipwa hata kwa wapita njia (Radamel Falcao), lakini mambo bado.

Man United inapiga mpira mwingi sana kwa sasa na timu inacheza soka la burudani lakini furaha bado ni ya kupapasa na jeuri ya kuifunga Arsenal watakavyo imekufa.

Mashabiki wengi wa Man United hawana uhakika na kitakachotokea si kwa kuwa soka ni mchezo usiotabirika bali timu yao ndio haitabiriki kama walivyozowea miaka michache iliyopita.

Kilio cha kudumu cha Man United kilikuwa ni tatizo la viungo wakabaji na msimu uliopita lilikuwa suala la beki pia, lakini matatizo hayo hayapo tena msimu huu.

Mwanzo wa msimu ilionekana timu imejiandaa kutafuta ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini sasa hali haionekani kuwa hivyo tena kutokana na ukame wa magoli klabuni hapo.

Kapteni Wayne Rooney aliaminika kuwa akicheka kama mshambuliaji wa kati magoli yatamiminika, lakini sivyo ilivyotokea na usajili wa mwishoni kabisa wa Antony Martial kutua Man Utd ulifufua matumaini kutokana na umahiri wake katika ufungaji mabao. 

Mabao yamekauka miguuni mwa Antony Martial na magoli hayo hayapo kwa Wayne Rooney wala Memphis Depay ambaye amerithi jezi namba 7 kutoka kwa Angel Di Maria aliyetimkia PSG baada ya kushindwa kuonesha makali yake ndani ya Manchester United.

Timu inaonekana imejaa wachezaji nguli katika usakataji soka, lakini mambo bado si ya uhakika klabuni hapo. 

Kila mtu anasema lake, lakini vidole vingi vinamuelekea Kocha Mkuu, Luis Van Gaal ambaye anaonekana kubadili mfumo wa uchezaji wa United ambako hakuna tena kupiga mashuti wala mashambulizi ya kushtukiza ila soka la pasi nyingi na kutawala mchezo kwa asilimia kubwa.

Soka linalopigwa na timu hiyo kwa sasa ndilo linalofanya timu isitabirike tena na ule uhakika wa kuifunga Arsenal hauwezi kuwepo maana timu zote zinacheza soka la aina moja (soka la pasi nyingi), lakini Arsenal ndio wababe wa aina hiyo ya soka.

Jambo linalomuingiza Van Gaal kitanzini ni kuhusu kupungua makali kwa wachezaji wake waliokuwa tishio misimu michache iliyopita kabla ya kocha huyo kutua klabuni Man Utd. 

Kupungua makali ya Wayne Rooney, Angel Di Maria (aliyetimkia PSG), Memphis Depay na Anthony Martial (waliotua klabuni msimu huu) kunaleta maswali mengi kwa mashabiki wenye shauku ya ushindi baada ya usajili wa gharama kubwa.

Wengi wanajiuliza nani alaumiwe kama timu imesajili wachezaji muhimu na waliokuwa vinara wa mabao na pasi za mwisho huko kwao inakuwaje leo wametua Man Utd na kupwaya? Tatizo ni wachezaji, kocha, mfumo au ugumu wa ligi? 

Ukisema mfumo bado tatizo ni kocha na ukisema wachezaji, bado tatizo ni kocha maana wachezaji hao hao ndio waliokuwa katika ubora mkubwa kabla ya kuwa chini ya Luis Van Gaal bado kuna sintofahamu klabuni hapo lakini ni wazi bundi anakaribia, kulia masikioni mwa Van Gaal ambaye anaelezwa kuwa anaishi “kikoloni” sana na wachezaji wake.

Katika soka kuna mengi yanaweza kutokea ndani ya muda mfupi lakini muda ndio hutoa majibu yote, wacha tusubiri.

 

Simu: 0715366010 Barua Pepe: amrope@yahoo.com

1920 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!